Shamba la Lyamungo mali ya KNCU – Waziri

Mvutano unaoendelea kuhusu nani mmiliki halali wa shamba la kahawa la Lyamungo baina ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) na Chama cha Ushirika wa Mazao (AMCOS) cha Lyamungo unatokana na Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kutochukua hatua.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba suala hilo lilikwisha kuamuliwa miaka 14 iliyopita na aliyekuwa Waziri wa Ushirika na Masoko (wakati huo), Sir George Kahama, katika barua yake ya Oktoba 21, mwaka 2005.

JAMHURI limefanikiwa kupata nakala ya barua hiyo yenye kumb. Na. CFA. 64/207/01/18 iliyotumwa kwa mwenyekiti na wajumbe wa Bodi ya Chama cha Msingi cha Ushirika Lyamungo kwa wakati huo.

Barua hiyo ya Kahama ilikuwa ikijibu rufaa ya chama hicho iliyokatwa dhidi ya uamuzi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini wa Machi 26, mwaka 2005 ulioipa haki KNCU kuwa mmiliki halali wa shamba hilo.

Msingi wa shamba hilo kuwa mali ya KNCU ni chama hicho  ambacho kwa wakati huo kikijulikana kwa jina la New Machame  Lyamungo Co-operative Society  kupewa mkopo  Sh 210,000 kutoka KNCU  kwa ajili ya ununuzi wa shamba hilo.

“Kwamba baada ya mawasiliano ya muda mrefu kuhusu namna ya kurejesha mkopo huo, chama chenu kiliwasilisha kwa KNCU Ltd utaratibu wa kulipa deni la shamba ambapo mlipendekeza kulipa deni hilo kidogo kidogo kwa miaka mitano kuanzia 31/12/1967  hadi 31/12/1971.

“Kwamba mapendekezo yenu yalijadiliwa na kukubaliwa kwenye kikao cha Halmashauri ya KNCU Ltd cha tarehe 25-27/10/1967 na hatimaye kuwekwa saini tarehe 16/12/1967,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Barua ya Waziri Kahama inaainisha kuwa hadi kufikia mwaka 1972 baada ya muda wa kulipa deni kumalizika, chama hicho kilikuwa kimeweza kulipa Sh 34,000 tu kama marejesho ya mkopo wa shamba.

Inafafanua kuwa, kutokana na makubaliano ya Desemba 16, 1967 kukiukwa, KNCU iliitisha mkutano mkuu uliofanyika Julai 14 na 15, 1972 na kupitisha azimio kuwa shamba la Lyamungo lichukuliwe na KNCU na kwamba Chama cha Msingi Lyamungo kirejeshewe Sh 34,000 ambazo kilikuwa kimelipa kwa KNCU.

Waziri Kahama anaeleza katika uamuzi wake kuwa baada ya mkutano huo wa KNCU, chama hicho cha Lyamungo kupitia kwa aliyekuwa mwenyekiti wake, Shemikaeli Nikodemo, kilisaini hati ya kuhamisha umiliki wa shamba hilo kwenda KNCU Agosti 20, 1973 na kuanzia hapo shamba hilo likaorodheshwa kwenye mizania ya KNCU.

Barua hiyo ikasisitiza kuwa, ni dhahiri kuwa mabadiliko ya umiliki wa shamba la Lyamungo kutoka kwenye chama hicho  kwenda KNCU Ltd yalizingatia taratibu na sheria ya vyama vya ushirika ambapo uamuzi hufanywa na wanachama kwenye mikutano mikuu.

“Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 52(6) ya kanuni za vyama vya ushirika 2004, nakubaliana na uamuzi wa mrajis wa  tarehe 29/3/2005 kuwa shamba la Lyamungo ni mali ya KNCU Ltd. Kwa hiyo, kwa barua hii mnaelekezwa kuondoa vikwazo vyovyote vile mlivyokuwa mmeweka ili KNCU waendelee na umiliki wa   shamba hilo na kulitumia kadiri watakavyoona inafaa,” inahitimisha barua hiyo.

Hata hivyo chama hicho kupitia kwa Mwenyekiti wake wa sasa, Gabriel Ulomi, kinasisitiza kuwa shamba hilo ni mali yake na kwamba KNCU walighushi nyaraka na kujimilikisha shamba hilo.

Mwenyekiti huyo wa Lyamungo AMCOS, anasema katika taarifa yake kuwa shamba hilo lilinunuliwa kutoka kwa raia wa Ugiriki, Philip Filios, mwaka 1965 na kilichokuwa chama cha ushirika kilichoitwa New Machame Lyamungo Co-operative Society.

Amesema chama hicho ambacho kwa sasa ndicho kinaitwa Lyamungo AMCOS, kilipewa stakabadhi ya malipo namba 1150 kutoka kwenye kampuni moja ya udalali ya Z. Ramzan baada ya shamba hilo kununuliwa kwa njia ya mnada.

“Mwaka 2003 wanachama na wananchi wa Lyamungo walipigwa na butwaa walipoona gazetini kuwa shamba lao litauzwa kwa njia ya mnada chini ya kampuni ya udalali kutokana na deni la Sh milioni 500 lililokopwa na KNCU kutoka Benki ya KCBL,” amesema Ulomi.

Mwaka 2007 aliyekuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. A. K. Kashuliza alikiandika barua chama hicho cha Lyamungo na kukipa siku 21 kuondoa zuio lake mahakamani lakini hadi sasa chama hicho hakijafanya hivyo.

Katika barua yake ambayo JAMHURI inayo nakala yake  ya Agosti 23, mwaka 2007 yenye Kumb. Na. FA. 64/207/04/79 kwenda kwa mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya chama hicho, mrajis huyo alionyesha kusikitishwa na hatua ya chama hicho kukataa kutekeleza maagizo hayo ya serikali.

“Hii ina maana kwamba kati yenu kuna kundi la watu ambao wanapinga amri halali ya serikali na wangependa kuendeleza migogoro inayokwamisha juhudi za maendeleo ya wananchi wa Kilimanjaro,” inasema barua hiyo.

Pamoja na mrajis huyo kutishia kuchukua hatua kama uongozi wa chama hicho usingetoa zuio hilo mahakamani, ni mwaka wa 12 sasa ofisi ya mrajis imeshindwa kuchukua hatua kama ilivyoonya katika barua yake ya Agosti 23, mwaka 2007.