Aprili 26, mwaka huu taifa litaadhimisha miaka 55 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Umri huo wa miaka 55 ya Muungano si haba, changamoto na mafanikio kadhaa yamekwisha kujidhihirisha na kubwa zaidi kwa upande wa mafanikio kuimarika kwa mshikamano baina ya raia wa pande hizo mbili za Muungano.

Serikali zote mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi (SMZ) kupitia viongozi wake zimekuwa zikichukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto zinazokwaza ustawi wa Muungano.

Kwa mfano, hivi karibuni akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira bungeni, Waziri wa wizara hiyo, January Makamba, amesema katika kushughulikia masuala ya Muungano, Februari 9, mwaka huu 2019 jijini Dodoma kilifanyika kikao ambacho hoja mbalimbali za Muungano zilijadiliwa.

Kikao hicho kilihusu pia mapendekezo ya utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano; mwongozo wa ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda na hoja za fedha na biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Amesema kikao hicho kilikuwa na mafanikio kadhaa ambayo ni pamoja na kupitishwa kwa utaratibu  wa vikao  vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano wenye  lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi wa vikao  vya Kamati ya Pamoja, ikihusisha kufuatilia maagizo na maelekezo yanayotolewa na kamati  hiyo.

Utaratibu  huo  pia,  Makamba anasema umeainisha kamati mbili ambazo ni Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na  Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala zilizopewa jukumu la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazohitaji utatuzi wa  haraka badala ya kusubiri utaratibu wa  kawaida wa vikao vya Kamati ya Pamoja  vya SMT na SMZ.  Amesema kamati hizo zitawasilisha taarifa  za  utekelezaji  katika vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

“Katika kikao hicho pia ulipitishwa mwongozo kuhusu ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya kimataifa na kikanda. Mwongozo huo umezingatia  maeneo ya mikutano ya kimataifa na kikanda, nafasi za masomo ya elimu ya  juu na mafunzo mengine nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada na mikopo  ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Makamba.

Lakini wakati waziri akiwa amebainisha hatua hizo, vilevile kumekuwa na changamoto kadhaa za Muungano, na katika changamoto hizo anasema: “…kuna changamoto ya ongezeko la  gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.”

Hata hivyo, anasema changamoto hiyo ilipatiwa ufumbuzi na imekubalika kuwa kodi ya ongezeko la thamani haitatozwa  kwenye umeme unaouzwa na TANESCO.

“Malimbikizo ya deni la VAT lililokuwa limefikia Sh bilioni 22.9 kwa Shirika la  ZECO kwenye umeme uliouzwa na TANESCO limefutwa. Kikao cha Kamati ya Pamoja pia kilijadili na kuzipatia ufumbuzi hoja za biashara baina ya   Zanzibar na Tanzania Bara ambazo ni gharama za kushusha mizigo, viwanda vya Zanzibar kupata leseni kutoka Wakala wa Usajili na Utoaji Leseni za Biashara (BRELA),” amesema.

Waziri huyo amesema katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kupata gawio la asilimia 4.5 ya fedha za misaada ya kibajeti, faida ya  Benki Kuu, Mfuko wa  Maendeleo ya Jimbo na kodi ya mapato yatokanayo na ajira. Hadi kufikia Machi, 2019 jumla ya Sh bilioni 36.79 zimepelekwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 14.00 ni PAYE, Sh bilioni 1.4 ni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Sh bilioni 5.64 ni fedha za Misaada ya Kibajeti (GBS) na Sh bilioni 15.75 ni gawio la Benki Kuu,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share