Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yametimiza miaka 25. Huu ni umri wa mtu mzima na hili linajionyesha wazi kule Rwanda, asilimia 60 ya watu wa Rwanda ni vijana na wengi wao ni miaka 25 na kwenda chini. Wengi wamezaliwa baada ya mauaji haya ya kinyama.

Aprili 7, 2019 Rwanda ilifungua siku mia moja za maombolezo ya kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari. Kwa Kinyarwanda inaitwa ‘Kwibuka 25’. Umekuwa ni utamaduni wa Rwanda wa kukumbuka siku hizi ambazo mwaka 1994, Watutsi zaidi ya milioni moja waliuawa kinyama kutokana na siasa mbaya ya Serikali ya Rwanda ya wakati huo.

Mataifa mengi ikiwemo Tanzania iliyowakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mzee Mkapa na Mama Anna Mkapa na mwandishi wa makala hii walialikwa kushiriki.

Kabla ya ufunguzi wa siku za kumbukumbu, Rwanda iliandaa kongamno la kimataifa la siku mbili lililowakutanisha washiriki zaidi ya 400 kutoka dunia kote ili kujadili jitihada hizi ambazo wamezifanya kwa kipindi cha miaka 25. Mada kwenye kongamano hili ilikuwa: ‘Tunza kumbukumbu, tanguliza ubinadamu.’

Msimamo wa Rwanda ni kwamba ili taifa lisonge mbele ni lazima kusamehe kwa gharama kubwa yale yaliyotokea wakati wa mauaji ya kimbari, lakini ni muhimu sana kukumbuka ili kuhakikisha matukio hayo katika historia ya mwadamu yasitokee tena.

Hoja kubwa hapa ni kile tunachojifunza kutoka Rwanda, kwamba siasa mbaya ni mauti na kwamba siasa mbaya daima itatafuta kulipiza kisasi. Lakini siasa nzuri, inasamehe kwa kuutanguliza ubinadamu, lakini inatunza kumbukumbu. Hili ni somo kubwa, ambalo linahitaji tafakuri na utulivu wa akili.

Na hii ndiyo hoja kubwa ya makala hii: ‘Kumbuka, tanguliza ubinadamu.’ Swali hapa ni je, dhana hii inaweza kuwa ya watu wote? Inawezekana kwingineko duniani kwenye visasi na kulipiza, watu wanashindwa kutanguliza ubinadamu? Wanakumbuka, lakini wanashindwa kutanguliza ubinadamu?

Waswahili wa kwetu wanasema: “Samehe na kusahau!” Lakini Wanyarwanda, wao wanasema: “Samehe, lakini usisahau.” Labda tunaweza kukaribia kupata jibu la kwanini? Maana aiingii akilini, mauaji yale yalikuwa ni ya kinyama kweli. Na hapa uzito mkubwa ni kwa watoto wadogo. Kwanini waliuawa watoto wadogo? Na vifo vyao vilikuwa vya kikatili sana. Walikuwa wakipigwa ukutani hadi vichwa vyao vinapasuka, na wengine walitwangwa kwenye vinu, kama vile kutwanga kisamvu au karanga hadi wanakufa! Inakuwa vigumu kuelewa chuki hii, ya kuuweka ubinadamu pembeni ilitoka wapi?

Rwanda ina vituo vingi vya Makumbusho ya mauaji ya kimbari, hapa nitaje viwili  tu, kituo cha Nyamata na Ntarama. Vituo hivi viko kwenye eneo la Bugesera, ambako kulikuwa na Watutsi wengi.

Historia ni kwamba baada ya ile vita ya 1959, watawala wa Kihutu waliamua Watutsi wapelekwe Bugesera ili wafe kwa kushambuliwa na mbung’o. Walikufa wachache wakati ule, maana walipata mbinu za kupambana na mbung’o mpaka mauaji ya kimbari yalipowakuta.

Nyamata ilikuwa ni parokia ya Kanisa Katoliki na Ntarama kilikuwa ni kigango cha Parokia ya Nyamata. Ndani ya kanisa la Nyamata, waliuawa watu elfu kumi (10,000) na miili ya watu hawa imetunzwa kwenye kanisa hili. Kigango cha Ntarama waliuawa watu elfu tano (5,000) na miili ya watu hawa na vitu vyao kama vile nguo, viatu, magodoro, vifaa vya maji bado vinatunzwa kwenye kanisa hili dogo.

Vifaa vilivyotumika kwa mauaji, kama mapanga, nyundo na vijiti walivyokuwa wakiwaingizia wanawake sehemu za siri hadi vinatokea mdomoni, bado vimetunzwa.

Damu zilizotapakaa kwenye makanisa hayo bado zinaonekana, hasa sehemu ambapo watoto wadogo walikuwa wakibamizwa hadi vichwa vinapasuka, damu iliyokauka inaonekana kwenye ukuta na kuashiria kwamba watoto wengi walikufa kwa kubamizwa kwenye ukuta.

Makanisa haya mawili hayatumiki tena kwa ibada. Yamebaki kama vituo vya makumbusho ya mauaji ya kimbari. Wamejitahidi kuacha kila kitu kilivyokuwa mwaka 1994, ingawa kwenye kanisa la Nyamata wamejenga kaburi kubwa chini ya kanisa, kutunzia mabaki ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbari.

Pia nje ya kanisa la Nyamata, wamejenga kaburi kubwa ambalo mtu unaweza kuingia na kushuhudia mwenyewe mabaki ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbari.

Mwili wa mwanamke, aliyebakwa na wanaume 20, na baadaye kuteswa hadi kufa kwa kuwekewa kijiti sehemu za siri na kutokea mdomoni umetunzwa kwenye kanisa la Nyamata.

Mauaji na mateso ya kutisha yalitokea kanisani na kuna ushahidi kwamba watu wengi waliuawa juu ya altare, meza ambayo kila Jumapili padri wao alikuwa akisimama na kugeuza mkate kuwa mwili wa Bwana, na divai kuwa damu ya Yesu; watu wote wa Nyamata, waliouawa na walioua walikuwa kila Jumapili wakikutana kwenye kanisa hilo kusali pamoja.

Watu walikimbilia kanisani kupata ulinzi. Miaka ya nyuma makanisa ndiyo yalikuwa kimbilio. Waliamini hakuna baya linaweza kutokea kanisani. Wauaji walitumia mbinu hiyo kuwahadaa Watutsi kukimbilia kanisani ili wapate njia nzuri ya kutekeleza mauaji yao.

Baada ya kuhakikisha idadi kubwa imeingia kanisani, walitoa taarifa kwa jeshi. Hivyo kwa kiasi kikubwa mauaji ya Nyamata na Ntarama, yalifanywa na jeshi. Mabaki ya risasi na mabomu kwenye kanisa la Nyamata, matundu ya risasi kwenye kuta, milango na paa la kanisa hilo ni ushahidi wa kutosha kwamba mauaji hayo hayakutekelezwa kwa mapanga na nyundo tu bali hata kwa risasi na mabomu.

Risasi hazikuangalia Mwili wa Kristu, maana kwenye kanisa hilo la Nyamata, kisanduku (Tabenakulo) kinachotumika kuhifadhi mwili wa Kristu, kilicharazwa risasi, na ni wazi hostia (Mwili wa Kristu) zilimwagika chini. Bwana Yesu, akawaacha watu wake kuchinjana mbele yake! Sanamu ya Bikira Maria, mama wa shauri jema, mama wa huruma na upendo, kwenye kanisa hilo nayo ilicharazwa risasi! Sanamu hiyo bado ipo hapo kanisani na ‘majeraha’ yake! Hapana shaka kwamba ukatili wa kutisha ulifanywa kwenye kanisa hilo.

Ni unyama mkubwa uliotendeka. Na sasa inapotimia miaka 25, Wanyarwanda wanatwambia: “Kumbuka, tanguliza ubinadamu.” Kumbukumbu hiyo kwa maoni yao ni lazima iwe endelevu kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana waliazimia kufanya kongamano la kimataifa kujadili jambo hili la ‘Tunza kumbukumbu, tanguliza ubinadamu’, wakati wa kumbuku ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari. Hivyo, mada mbalimbali zilizojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na changamoto za vijana, elimu ya kihistoria, haki na maendeleo.

Washiriki na  wachokoza mada katika kongamano ya kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari walizungumza mambo mengi kuhusu tukio la mauaji ya kimbari na namna Wanyarwanda wanavyoishi kwa amani. Kwamba pamoja na yote, Rwanda inasonga mbele – ina amani na mshikamano.

Rwanda inakumbuka yaliyotokea, lakini kwa uongozi bora na siasa safi, inasonga mbele.

Mjumbe wa Tume ya Taifa ya maridhiano, Edouard Bamporiki, alisema katika kongamano hilo kwamba kizazi cha sasa kimekuwa katika mfumo wa watu kuishi kwa haki sawa na kupata elimu sawa.

“Ni kweli watu wataendelea kupata maumivu kwa kile kilichotokea, msongo wa mawazo, lakini maisha ya amani ni ahadi…Kwa pamoja tunaweza kujiponya,” alisema Bamporiki.

Pia akaongeza kwamba: “Mauaji hayo yalitokea wakati nikiwa na umri wa takriban miaka 10. Nilikuwa hospitalini na niliona mtu akikatwa kichwa pembeni mwa kitanda changu…Nilikuwa sijui kwa nini kikundi kimoja kilikuwa kinaua kingine.” Sasa anatambua umuhimu wa kuulinda ubinadamu na kuutetea kwa gharama yoyote ile.

Naye mchangiaji kutoka Afrika Kusini, Musupyoe Boatamo, alisisitiza juu ya elimu ya  watoto na wajukuu kuhusu mauaji ya kimbari, kwa sababu familia zao ni waathirika wa mauaji hayo.

“Mtazamo wangu ni kwamba, mnapaswa kuwaelimisha watoto na si kukaa kimya…lazima mtengeneze mazingira mazuri, kwa sababu maumivu ya ndani kwa ndani ni hatari,” alisisitiza Boatamo.

Wazo hili la kuwafundisha watoto na kutokaa kimya juu ya mauaji ya kimbari lilisisitizwa na wachangiaji wengi. Hata hivyo linaenda pia na msimamo wa Rwanda, wa kukumbuka na kutanguliza ubinadamu.

Mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Ufaransa, Jean Dupaquie, aliyekuwa mmoja wa wachokoza mada katika kongamano hilo alisema kwamba katika jamii vijana wanapaswa kuambiwa ukweli juu ya historia yao. “Nakumbuka kabla ya mauaji ya kimbari, nilihudhuria mkutano wa Rais Habyarimana na waandishi wa habari huko Paris…nilizungumzia makala niliyosoma kuhusu Kangura, iliyokuwa na kichwa cha habari: “Kuamsha wito kwa Wahutu,” na kupewa jibu kwamba: “Rwanda, hiyo ni kama uhuru wa kujieleza.”

Haya ni majibu tunayoyashuhudia sehemu mbalimbali, hasa katika nchi za Afrika, magazeti yanayoiunga mkono serikali hata yakifanya makosa na kuandika vitu vya hatari au uchochezi vinafumbiwa macho na kupewa sifa ya  “uhuru wa kujieleza”. Vyombo vya habari vilivyofumbiwa macho na Serikali ya Rwanda ya wakati ule, vilisababisha mauaji makubwa.

Tunapowapongeza Wanyarwanda kwa kufikisha miaka 25 baada ya mauaji ya kimbari, tujifunze kutoka kwao kwamba siasa mbaya ni mauti na siasa nzuri ni maendeleo. Lakini pia tujifunze kutunza kumbukumbu na kuutanguliza ubinadamu. Tuwasamehe wanaotutendea mabaya, lakini kamwe tusiyasahau matendo yao!

Please follow and like us:
Pin Share