Wapendwa wasomaji, ninawasalimu kwa salamu za upendo. Naamini kwamba wengi wenu mnaendelea kufurahia, kushangaa, kupigwa na bumbuwazi ama kuchanganyikiwa kwa hatua mbalimbali zinazochokuliwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, au kama anavyojulikana zaidi JPM.

Kabla sijaendelea na uchambuzi wangu wa leo, ninapenda kuwajulisha habari njema juu ya uwepo wa tovuti iliyojikita katika habari, taarifa, uchambuzi, na mtandao wa fursa za uchumi, ujasiriamali, biashara na uwekezaji. 

Tovuti hii yenye anuani www.bungelauchumi.com tuna visheni ya kuifanya kuwa kituo bora na cha kwanza chenye kuaminiwa kwa maarifa na mambo ya uchumi na fedha; hapa nchini Tanzania na katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Sasa tuendelee. Marekebisho ya uchumi mkubwa (macro-economic) huwa yana chemba tatu, chemba ya kwanza ni uchumi wenyewe, chemba ya pili ni saikolojia za wapiga kura na chemba ya tatu ni mwelekeo wa siasa za wakati husika.

Athari za marekebisho ya kila chemba zinatofautiana, na hatua za marekebisho huweza kufanyika kutegemea nini unataka kitokee baada ya marekebisho unayoyapitisha.

Kiuchumi tunasema kwamba chemba hizi tatu zina uhusiano hasi (inversely proportional), kwa maana kwamba unapolipa unafuu jambo moja, maana yake unaliadhibu jambo jingine. Lakini kama ukitaka kuleta msawazo, ni vigumu sana kutokea kwa mabadiliko ya kushtua ama kukonga nyoyo. 

Wataalamu wa uchumi huwa tunasema mambo (variables) mengi katika uchumi ni kama “mashetani” wanaoshirikiana, ukimfunga huyu, basi yule kule anaendelea kutamba zaidi! Ndugu msomaji, usipate tabu ngoja nikueleweshe sasa kwa mifano halisi.

Katika uchumi ni kwamba moja ya mambo yanayomimina fedha katika mzunguko ni matumizi ya serikali. Kadiri serikali inavyomimina fedha nyingi mitaani kupitia miradi na shughuli zake, ndivyo mwananchi wa kawaida anavyokuwa na nafasi ya kupata fedha zaidi na zaidi. Mathalani, mahali fulani wanapokuwa wakijenga barabara, kunakuwa na wingi wa wafanyakazi ambao watahitaji kula, kulala, kusafiri, kuvaa na mengineyo.

Kwa hiyo, kwa kupeleka mradi wa barabara katika maeneo hayo utabaini kuwa mama lishe atauza chakula, mwenye nyumba atapata kodi, mwenye bustani atauza mboga zake na mnyororo huo unaendelea na kuendelea. Vivyo hivyo, watu wanapolipwa posho kwenye semina, warsha ama makongamano, fedha zile wanakwenda kuzitumia mtaani; mwenye bucha anapata fedha, mwenye duka la nguo anauza, mwenye, genge naye anauza.

Tatizo lililokuwapo katika uchumi wa Tanzania wakati wa awamu ya nne, siyo kumimina fedha mitaani kupitia matumizi ya serikali; isipokuwa shida imekuwa ni namna gani fedha hizi zinamiminwa. Tatizo kubwa limeonekana kuwa ni umiminaji wa fedha usio na tija kiuchumi (kwa matumizi yasiyozingatia thamani ya uchumi) pamoja na ufisadi ambao mara zote huwa unawapeleka watu wachache kuhodhi fedha, ndiyo kama yale tunayosikia mtu amekutwa nyumbani kwake na mamilioni ya shilingi.

Dk. Magufuli ameanza kushughulikia uchumi kutoka katika pembe ya saikolojia ya wapiga kura, yaani kushughulika na mambo ambayo yatarudisha ari na morali wa wananchi. Tunaposema saikolojia ni yale mambo ambayo yameonekana kuwaudhi wananchi kwa muda mrefu na hatua zozote zinazochukuliwa ni lazima zifute hasira zao na ziwapatie furaha.

Ukimsikiliza Rais Dk. JPM utagundua anasisitiza sana suala la wananchi kuanza kufanya kazi. Kwanza, ni kwa sababu anafahamu kwamba kiutamaduni  Watanzania wengi siyo watu wa kufanya kazi kwa mtindo wa “kufa na kupona” hivyo anajaribu kuipandikiza hulka hii.

 La pili ni kwamba anatambua wazi kuwa hatua anazochukua na atakazoendelea kuchukua siyo rafiki hata kidogo kwa watu walegevu katika kazi na katika kufikiri. Uamuzi wa Dk. Magufuli ni msumeno unaokata wale unaofikiri unawakata lakini unakata na wale ambao hujawadhania kama watakatwa.

Rais ameamua kuanza na mambo mawili; la kwanza ni kupunguza matumizi ya Serikali na la pili ni kuzirejesha fedha zilizopo mitaani. Unapopunguza matumizi ya Serikali maana yake unasababisha fedha kuwa adimu mtaani. Unapokaza katika eneo la ukusanyaji kodi maana yake unataka kila fedha utakayoiingiza mtaani, sehemu yake irudi serikalini ikiwa tayari imeshazalisha thamani fulani. Tunakwenda sawa hadi hapo? Sasa ngoja nikupe tafsiri ya haya yote yatakavyokuathiri kwa miaka hii mitano ya JPM.

Kwa miaka hii mitano ni kwamba fedha itakuwa adimu sana katika uchumi, yaani kuipata noti mikononi mwako itakuwa ni mbinde sana ama itabidi utumie jasho zaidi. Watu wengi wamekuwa wakisema kuwa awamu ya nne mambo yalikuwa magumu kifedha. Lakini ni lazima mfahamu kuwa kwa staili na utamaduni wa kazi na fikra waliokuwa nao wengi wakati wa awamu ya nne, kama utabaki hivyo hvyo; basi upatikanaji wa fedha kwa awamu hii utakuwa mgumu maradufu ya ilivyokuwa kwa JK.

Jambo jema ni kwamba vitu vingi vitashuka bei kwa sababu thamani ya shilingi itaongezeka na mianya ya kuvujisha fedha itazibika. Kwa hiyo, sasa hivi unaposhangilia kwamba Serikali imepunguza matumizi kwa kufuta semina, kufuta matumizi yasiyo ya lazima n.k; basi utambue kuwa hayo ni maandalizi ya kuiadimisha shilingi mtaani na ukata huo unaweza kukukuta ikiwa utakuwa hujajiandaa vya kutosha!

Muda si mrefu kuanzia sasa; utajionea namna itakavyokuwa ngumu sana kushika walau shilingi elfu moja huku mtaani. Tunafurahi kisaikolojia lakini kuna maumivu yetu yanatusubiri kiuchumi. Ingawa (nikiri wazi kuwa) hakuna namna nyingine ya kuuokoa uchumi huu unaochechemea isipokuwa kuchukua hatua hizi.

Katika uchumi kuna makundi mawili – wazalisha thamani na watumia thamani. Kundi la wazalisha thamani (value creators) linaundwa na wazalishaji mashambani, wajasiriamali wanaoongeza minyororo ya thamani kwa bidhaa na huduma na wafanyabiashara. Kundi la watumia thamani (value consumers) linajumuisha wafanyakazi na walaji wa mwisho. 

Ili uchumi wa nchi usonge mbele, ni lazima wazalishaji thamani wazalishe thamani inayozidi mahitaji ya watumiaji thamani. Kama watumia thamani wakiwa na matumizi makubwa kuliko uwezo wa wazalishaji maana yake ni kwamba uchumi unaingia matatani na kinachotokea ni kwamba kunakuwa na ukosefu wa kutisha wa ajira, thamani ya shilingi inaporomoka, Serikali inapoteza uwezo wa kununua na kulipa na watu wanakuwa na fedha nyingi kuliko thamani wanazozalisha.

Katika hali ya namna hii, unapotaka kuuokoa uchumi ni lazima uwageukie wazalishaji thamani, uwabebe na kuwasaidia ili wawaokoe watumia thamani na pia wauokoe uchumi kwa ujumla. Unapowageukia wazalisha thamani lazima uchague kifundo utakachofungia nanga yako ya kuanza kuuvuta uchumi. Kifundo hiki ama vifundo hivi ni sekta utakayoitumia kama kituo cha uhuishaji wa uchumi. Serikali ya awamu ya tano imechagua sekta ya viwanda vyenye muunganisho na kilimo, uvuvi na ufugaji katika juhudi za kuuhuisha uchumi.

Tafsiri ya hatua hizi ni kwamba miaka hii mitano itakuwa migumu sana kwa watumia thamani na itakuwa ya neema kubwa sana kwa wazalisha thamani. Kwa lugha  nyepesi kabisa ni kwamba miaka hii mitano itakuwa migumu sana kiuchumi na kifedha kwa wafanyakazi wanaotegemea mishahara pekee kwa asilimia 100, lakini itakuwa na vicheko vingi sana kwa wajasiriamali (wazalisha thamani). Vile vile miaka hii haitakuwa rafiki kwa mlaji wa mwisho hasa ikiwa hana uzalishaji wowote anaoufanya/anaouingiza katika uchumi.

Nadhani wafanyakazi wa sekta ya umma, mmeshaanza kushuhudia kwamba safari zinafutwa, semina zinaondolewa, warsha na makongamano hakuna. Siyo kwamba Rais hawapendi wafanyakazi, la hasha, hizi ni hatua za kiasili kabisa (natural trends) katika uchumi ambazo hazina budi kuchukuliwa katika kuuokoa uchumi. Tatizo kubwa walilonalo wafanyakazi wengi (hasa wa sekta ya umma) ni kwamba huzitazama ajira zao kama kiwanda cha kuzalisha fedha. 

Uhalisia ni kwamba ajira ni sehemu panapokupatia “mbegu” (yaani mshahara) ili ukapande zaidi (yaani uutumie mshahara kuzalisha fedha nje ya mshahara). Ndiyo maana Dk. Magufuli anaposema “hapa kazi tu” kuna watu wanadhani anajifurahisha ama wanadhani anawalenga watu fulani. Neno “hapa kazi tu” lina mantiki kubwa sana katika uchumi wa kila mmoja wetu kiuchumi kwa nyakati za sasa.

Usalama wa mfanyakazi kwa sasa upo katika kufanya kazi maradufu. Yaani ukitoka kazini, kama unataka usalama wa kiuchumi na kifedha huna budi isipokuwa kurudi nyumbani na kufuga walau kuku, kulima bustani au hata kuanzisha kiwanda kidogo. Kwa tafsiri nyingine ni kwamba lazima uhakikishe sehemu yako inakaa katika upande wa wazalisha thamani. Huu ni wakati wa kujitoa sadaka kwa kufanya kazi “kama kichaa” zaidi ya ulivyozoea, ni muda wa kufanya kazi zaidi ya moja, vinginevyo utanyolewa ‘mazima’

Na kama kuna wakati inabidi uhusishe matumizi makubwa ya fikra/akili, basi ni sasa kwa sababu kazini utabanwa zaidi ya ulivyozoea na wakati huo huo uchumi unakulazimisha uzalishe zaidi ili uwe salama na ‘kibano’ kinachokuja na kitakachokuwapo. Ndiyo maana nimesema awali kwamba sijui ni wangapi wanamwelewa Dk. Magufuli anaposisitiza kwamba Watanzania ni lazima tufanye kazi!

Hiki ni kipindi kigumu sana kwa wale waliozoea kufanya kazi kwa mazoea, wale wazembe, wale wavivu wa kutenda na wavivu wa kufikiri pia. Mazoea ya kutoka nyumbani asubuhi, kwenda kazini na kurudi nyumbani kulala kwa sasa yatakugharimu. Uzembe wa kufikiria kuwa mshahara pekee utakutatulia changamoto zako katika kipindi hiki utakuweka selo ya umasikini! 

Dk. Magufuli amekuja na kibano na kibano hiki kinakwenda kuwaminya vya kutosha wavivu wa kufikiri, wazembe wa kufanya kazi na wale waliozoea ukawaida. Na kwa kuwa Watanzania wengi siyo watu wa kufanya kazi kwa mtindo wa “kufa na kupona” nina wasiwasi kwamba kibano hiki kitawatandika watu wengi sana muda si mrefu.

Hata hivyo, kufuatia awamu hii kuamua kuifunga nanga kwenye viwanda vyenye mnyororo wa thamani katika kilimo, ufugaji na uvuvi; maana yake ni kwamba kutakuwa na fursa nyingi na nzuri sana katika kilimo, ufugaji na uvuvi. Kama hukuwahi kufikiria huu ndiyo muda wa wewe kwenda kuchimba bwawa la samaki. 

Huu ndiyo muda wa kwenda kutafuta mapori na kuanza kufuga nyuki, huu ndiyo muda wa kwenda mashambani na kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo. Kwa awamu hii; ukifanya uzalishaji katika maeneo haya maana yake wewe unakuwa kwenye upande wa wale watakaosalimika na kibano na tena unakuwa mmoja wa watakaofanikiwa sana kiuchumi katika awamu hii.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi

By Jamhuri