‘Rediscovering Africa’ ni jina la kipindi kinachorushwa na televisheni ya taifa ya China (CCTV). Maana ya jina hilo kwa lugha ya Kiswahili ni “Igundue tena Afrika”.

CCTV huwafikia Watanzania kupitia baadhi ya vituo vya televisheni vya hapa nchini ikiwamo Televisheni ya Taifa (TBC1).

Katika kipindi hicho cha ‘Redicovering Africa’, kuna mambo mengi ya Afrika yanayooneshwa. Lakini nilichofanikiwa kuona hivi karibuni ni Wachina wakiwafundisha wananchi wa Malawi kuhusu namna ya kulima pamba.

Bila shaka unaweza ukadhani kwamba nimeanza kuleta mambo ya ubaguzi wa rangi hapa, la hasha. Lakini jina hilo la kipindi hicho limenikumbusha wakati Wazungu wakifanya ugunduzi (exploration) wa Bara la Afrika kabla ya kuhamia.

Afrika iligunduliwa, Amerika iligunduliwa, Afrika Kusini iligunduliwa na Mto Niger pia uligunduliwa. Kumbuka, katika jamii ya Wahausa (kabila moja lililopo kaskazini ya Niger), Mto Niger tangu enzi hizo ulikuwa na jina lake la asili ambalo ni Mto Kwara.

Lakini wakati Wazungu wanaligundua Bara la Afrika, mto huo waliubatiza kwa jina la Niger. Hakuna ugunduzi hapo. Wenyeji (Wahausa) walitambua uwepo wa mto huo hata kabla ya wao kuja na ndiyo maana ulikuwa linaitwa Mto Kwara.

Wakati Bara la Afrika likigunduliwa, jamii nyingi zilikuwa zikiishi maisha ya ujima au kwa lugha nyingi maisha ya ukale. Wengi walikuwa wakitembea uchi. Baadhi walikuwa wakila nyama mbichi. Wengi pia waljishughulisha na masuala ya dini. Kilimo, mitindo ya ujenzi wa nyumba nazo hazikufanana na zile zilizokuwa barani Ulaya enzi hizo.

Baada ya Wazungu kuwa wameshagundua Bara la Afrika muda mrefu uliopita, Wachina nao wakaona ni vyema nao sasa waanze kuigundua Afrika kwa mara nyingine tena – ‘Rediscovering Africa’  ili wapate nafasi ya kudhihirisha uhodari  wao duniani.

Baada ya miaka mingi ya uhuru na kuwapo kwa wasomi wengi, bado mataifa ya Afrika yanaishi maisha ya ujima kiasi cha kutegemea Wachina kuja kuwagundua!

Katika ukanda wa Afrika Mashariki na sehemu nyingine za Afrika, kuna miundombinu yenye hadhi ya juu sana, ambayo kwa namna moja ama nyingine ina hadhi sawa na ile iliyopo katika nchi za Ulaya, Uingereza ikiwa ni mojawapo. Lakini cha ajabu, Wachina hawataki kugundua hayo. Wapo radhi kutafuta yale mambo machache ambayo wao wanaamini ni mabaya ili wawasaidie Waafrika ili mwishowe wapate kitu cha kwenda kuwaonesha watu wao huko China, ambako watapata sifa na heshima.

Je, ulishawahi kujiuliza ni nani wa kukaa chini na kusubiri kulishwa kama mkimbizi? Ni mtu mweusi. Je, unajua ni nani wa kuoneshwa namna ya kuboresha kilimo? Ni mtu mweusi. Je, unajua ni akina nani wanapigana vita isiyoisha? Ni mtu mweusi. Angalia Syria nao wameshaingia kwenye orodha ya mataifa yanayozalisha wakimbizi duniani.

Lakini endapo Syria itakuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya haitafanana na Sudani Kusini iliyovalia nguo chakavu? Hapana. Moja kwa moja wao na watoto wao watazama humo moja kwa moja: kwa namna ya kuvaa na hadhi ya maisha kwa ujumla. Nisingependelea kuzungumzia juu ya rangi kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyejichagulia rangi yake ya ngozi.

Unaweza ukajiuliza kwa nini wao Waarabu hawaonewi? Na kwa nini Waafrika wa vijijini hawana furaha? Jibu ni ukosefu wa elimu. Waarabu wana historia ya zaidi ya miaka 2000 wakijifunza. Wakati fulani mababu zao walitikisa dunia. Lakini, kama una tatizo lolote, liwe la kurithi au la namna yoyote, ujue hakuna wa  kumlaumu isipokubali kuliweka wazi.

Kiukweli, sijui huyu mrembo anayejiita Umoja wa Afrika (AU) atakuwa anafananaje! Wengi wanasema anavutia sana ukimtazama. Lakini ukweli amelala usingizi wa pono. Naomba unisamehe kama kauli yangu imekukera. Lakini ukweli ni kwamba kazi anayoifanya AU duniani haionekani. 

Je, inawezekana ikawa siyo sehemu ya majukumu yake kuwabembeleza Waafrika usingizi kiasi cha kuja kuamshwa na Wachina? Wakati fulani alionekana akitoa ulinzi kwa treni za mwendo kasi za China. Je, siyo kwamba aliteuliwa kufanya hivyo ili kushawishi serikali za nchi za Afrika kununua hizo treni, serikali ambazo hata hazitaki kuboresha maisha ya watu wao?

Mpaka sasa Tanzania ina jumla ya vyuo vikuu 52, vyuo kadhaa vya ufundi, shule za sekondari pamoja na shule za msingi. Lakini bado sehemu kubwa ya Watanzania wanaishi maisha ya ujima kiasi cha kuwapa mataifa mengine nafasi ya kutusukumia misaada. Kwa nini viongozi wetu wanashindwa kuona masaibu yetu? Kwa nini wao wanadhani wakishavalia suti zao zinazotengenezwa nje ya nchi, basi wanajikuta wamekuwa bora kuliko wale ‘malofa’ wanaoishi maporini wakiendelea kutumia zana za kale? Kwa nini taasisi zetu haziwajibiki ipasavyo kwa wananchi?

Maendeleo hayaletwi kwa siku moja. Pia, inawezekana hata sisi ambao ni wasomi tupo katika lile kundi la wanaoishi maisha ya ujima tunasubiri kuja kufumbuliwa macho na Wachina. Kwa upande mwingine, maendeleo tunayo.

Lakini maendeleo ya ukweli yatakuja pale tutakapokubali kujitambua na kutenga muda wa kutosha wa kuwekeza katika kutoa elimu bora kwa watu wote. Tukubaliane kwamba baada ya muda fulani hakutakuwa na Mtanzania anayetumia jembe la mkono kulima shamba lake, kwa muda wa miaka thelathini hatutakuwa na mwanamke wa Kitanzania anayepika kwa kutumia kuni. Tukifanya hivyo maana yake ni kwamba kama Mzungu atataka kumuona ‘tumbiri’ akilima shamba lake kwa kutumia zana za kale, kamwe hatamuona tena.

Maendeleo kama hayo yanayofanywa na Waafrika, ndiyo na sisi waandishi wa habari tunapaswa kuzitangaza. Nasikitishwa sana na hizi programu za Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya  zinazojidai kutoa misaada ya kusaidia Afrika. Imani yao ni kwamba Waafrika hawawezi kujisaidia wenyewe, ni lazima tuwasaidie.

 Lakini kitu ambacho Waafrika tunaweza kufanya kwa umahiri wa hali ya juu ni kuuana wenyewe kwa wenyewe. Kuna mtu mweupe yeye kazi yake ni kutengeneza silaha kwa ajili ya kutumika katika vita, halafu anamtuma mwandishi wake aje kurekodi jinsi wanavyouana. 

Tanzania, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sudan bila shaka nao wangefaa kuwa wagunduzi wa Malawi lakini hapana. Ngozi yao haina hadhi ya kufanya hivyo. Wanajisikia furaha kazi hiyo ikifanywa na mtu mweupe wakisherehekea mchanganyiko wa rangi ya ngozi.

Je, unaweza kushangazwa na mwigizaji mmoja katika filamu moja ya Kihindi aliyemtusi mwigizaji mwenzake mashuhuri kwamba anafanana na ‘tumbili’ wa Kiafrika? Alikuwa na uhakika kwamba huyu mwenzake siyo tumbili, lakini ni binadamu mwenye tabia zinazofanana na za tumbili. Hili halikubaliki kamwe. 

2602 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!