Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kuahidi kuwa kuanzia makala ya leo nitaanza kuzungumzia kodi na tozo mbalimbali katika biashara. Katika makala hii ya Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania, kupitia vitabu na sheria mbalimbali nilizosoma, nimebaini kuwa kuna kodi za msingi saba na ushuru wa aina tatu.

Kodi hizi ni kodi ya mapato (mtu binafsi), kodi ya makapuni, kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE), kodi ya kuendeleza ujuzi (SDL), kodi ya zuio, kodi ya faida kubwa (capital gains tax) na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Pia kuna ushuru wa aina tatu; ushuru wa forodha, ushuru wa stempu na ushuru wa michezo ya kubahatisha.

Sitanii, kwa kuzitaja hizi kodi mtu anaweza akadhani ni rahisi, ila kumbe zina mfumo wake na taratibu za kulipika. Kwa mantiki hiyo, kuepusha kumwacha hewani msomaji, nitafafanua moja baada ya nyingine. Ikumbukwe kodi hizi si pekee katika biashara, maana zipo kodi za pango, huduma za miji/halmashauri au jiji na nyingine nyingi.

Kodi ya Mapato (mtu binafsi)

Katika biashara watu binafsi wanagawanywa katika makundi mawili. Kuna kundi la wale wafanyabiashara wadogo wasiolazimika kutunza hesabu zilizokaguliwa kulingana na mapato yao kwa mwezi (mzunguko wa fedha) na wafanyabiashara wa kati wanaopaswa kutunza hesabu zilizokaguliwa.

Wafanyabiashara wadogo wanatozwa kodi hii ya mapato kwa utaratibu wa makisio (presumptive tax system), lakini hawa wafanyabiashara wa kati wanaotunza hesabu zikakaguliwa wanatozwa kodi kulingana na faida wanayopata kwa mwaka baada ya kufunga hesabu zao.

Utaratibu wa makisio ya kodi unatumika kumkadiria kiasi anachopaswa kulipa mfanyabiashara mdogo kulingana na mzunguko wa fedha katika biashara zake kwa mwaka mzima (turnover). Mfanyabiashara wa ngazi hii halazimiki kuandaa hesabu zilizokaguliwa na kuziwasilisha TRA. Lakini pia mfanyabiashara huyu anaweza kuamua kutunza hesabu zake na zikakaguliwa, hivyo akalipa kodi kutokana na faida anayoipata mwisho wa mwaka.

Sifa za kulipa kwa makadirio

Kwa mfanyabiashara kupata sifa ya kulipa kodi kwa njia ya makadirio anapaswa kuwa mwananchi mkaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzunguko wake wa fedha kwa mwaka usizidi Sh milioni 20, biashara inapaswa kuwa ndiyo chanzo pekee cha mapato kwa mwaka kufikia kiwango hicho. Fedha kwa mfano zinazotokana na mshahara wa ajira haziwezi kuingizwa kwenye makisio.

Kodi ya mapato ya mtu binafsi inapaswa kutokana na mapato ya biashara zinazofanyika ndani ya Tanzania pekee. Hii ina maana kama unafanya biashara ya kimataifa, basi unapaswa kutunza hesabu zako ambazo zitakaguliwa na kulipa kodi kutokana na faida uliyoipata.

Viwango vya Kodi

Unapofanyiwa makadirio kuna viwango vilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria unavyopaswa kulipa kama mlipakodi binafsi. Viwango cha kodi unayopaswa kulipa vitatokana na kiwango cha mzunguko wa fedha katika biashara unayofanya kwa mwaka. Ikiwa hakuna kumbukumbu sahihi, basi Kamishna wa TRA atakukadiria kiasi unachostahili kulipa.

Viwango vimeainishwa ambapo kwa mtu mwenye mzunguko wa fedha usiozidi Sh 4,000,000 kama walivyo wamachinga halipi kodi hata senti. Ni katika hatua hiyo Rais John Magufuli ameamua kuwapa wamachinga vitambulisho vya Sh 20,000.

Mzunguko unapozidi Sh milioni 4, lakini hauzidi Sh milioni 7.5, kodi yake ni Sh 150,000 kwa mwaka kwa mtu asiyetunza hesabu na asilimia 3 ya kiasi kinachozidi Sh milioni 4 kwa anayetunza hesabu. Mzunguko wa fedha kwa mwaka katika biashara yako ukiwa Sh milioni 7.5, lakini hauzidi Sh milioni 11.5, basi utalipa Sh 318,000 kwa mfanyabiashara asiyetunza hesabu na Sh 135,000 + 3.8% ya kiasi kinachozidi Sh milioni 7.5.

Sitanii, ikiwa mzunguko wako wa biashara ni Sh milioni 11.5, lakini haizidi Sh milioni 16, basi utalipishwa Sh 546,000 kama hutunzi hesabu na kwa anayetunza hesabu atatozwa Sh 285,000 + 4.5% ya kiasi kinachozidi Sh milioni 11.5. Ikiwa mzunguko wako unazidi Sh milioni 16, lakini hauzidi Sh milioni 20, basi utatozwa Sh 862,500 kama hutunzi hesabu au Sh 478,000 + 5.3% ya kiasi kinachozidi Sh milioni 16.

Je, unafahamu ikiwa biashara yako ina mzunguko wa zaidi ya Sh milioni 20 utaratibu wa kulipa kodi ukoje? Usikose toleo lijalo la JAMHURI, utaratibu utaelezwa kwa usafaha. Tukutane Jumanne ijayo.

By Jamhuri