Miaka 30, Rais Samia amefungua milango

Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Julai 1, 2022 Tanzania imetimiza miaka 30 tangu mfumo wa siasa za vyama vingi urejee hapa nchini. Wakati mfumo huu ukirejea mwaka 1992, ilikuwapo hofu kubwa katika sehemu mbalimbali za nchi hii. Wengi walivihusisha vyama vingi na vurugu. Hofu hii ilielekea kutimia kwa Zanzibar mwaka 2001 yalipotokea mauaji ya askari polisi na Watanzania kadhaa. Kwa mara ya kwanza Tanzania ilizalisha wakimbizi wakakimbilia eneo la Shimoni, Kenya.

Kwa Tanganyika (Tanzania Bara) mara zote kila baada ya uchaguzi zimekuwapo tuhuma za washindani kuibiwa kura. Kiuhalisia, ushindani kati ya vyama vya upinzani na chama tawala uliendelea kukua hadi mwaka 2015. Vyama viliifanya kazi ya kuisimamia serikali na kuwafanya wananchi kufahamu baadhi ya mambo ambayo awali yasingefahamika.

Wakati Tanganyika inapata Uhuru Desemba 9, 1961 na Zanzibar ilipofanya Mapinduzi Matufuku Januari 12, 1964, nchi hizi mbili zilikuwa na mfumo wa vyama vingi. Hata tarehe ya Muungano kati ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar uliofanyika Apili 26, 1964 kuzaa Tanzania, nchi ilikuwa na mfumo wa vyama vingi. Mfumo huu wa vyama vingi kwa hapa nchini ulisitishwa mwaka 1965 na ukarejeshwa mwaka 1992 baada ya wimbi kubwa na vuguvugu la kisiasa duniani.

Sitanii, kashfa ya Richmond, EPA, Kagoda, Green Miles na nyingine nyingi zilifahamika kupitia mfumo wa vyama vingi. Inawezekana kashfa hizi ziliwakera waliokuwa wanufaika, lakini kwa upande wa wananchi kulipuliwa kwa kashfa hizi kulisaidia wananchi kunusuru fedha zao wanazotoa kupitia kodi, ambazo zingeishia katika mifuko ya wajanja wachache. 

Ushindani uliendelea kukua hadi mwaka 2015. Nasema 2015 maana ghafla mwaka 2019 dunia ilibaini jambo jipya kwa Tanzania. Elimu ya wanasiasa wa upinzani ilishuka ghafla kwa kiwango kikubwa, wakashindwa kujaza fomu katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, fomu zao zikawa na makosa nchi nzima, ila kwa CCM zilijazwa vizuri. CCM zilijazwa vizuri na wagombea wao wengi wakapita bila kupingwa. 

Ikaja mwaka 2020 kwenye Uchaguzi Mkuu, mchezo ukaendelea kuwa uleule. Wapinzani ikawa hawajui kujaza fomu, japo katika vyuo na madarasa ya shule za msingi hadi sekondari walisoma pamoja na wagombea wenzao wa upande wa CCM. Hili ndilo limenifanya niseme demokrasia ilikua hadi mwaka 2015, baada ya hapo demokrasia ilipata utapiamlo, ikasinyaa kwa kiwango cha kutisha. Kila mtu alijua na dunia ilijua. 

Sitanii, mfumo wa vyama vingi ulijaribiwa rasmi mwaka 1995. Katika Uchaguzi Mkuu huu wa kwanza wa vyama vingi, washindani wakubwa na kura walizopata walikuwa ni Benjamin William Mkapa (4,026,422) na Agustino Lyatonga Mrema (1,808,616). 

Uchaguzi huu ulifanyika Oktoba 29, 1995. Nilikuwa msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Kahororo, Bukoba, huku nikiwa mwalimu Mugeza Sekondari, hivyo niliona vuguvugu la Mrema kituoni. Tulihesabu kura, tukabandika matokeo kwenye kuta za kituo na tukapeleka masanduku halmashauri ya mji kwa ajili ya jumla kuu. Utaratibu ulikuwa huo kwa nchi nzima. Mrema alikuwa kimbunga.

Mwaka 2000 Rais Mkapa aliongeza ushindi wake ukafikia kura 5,863,201, wakati huo Prof. Ibrahim Haruna Lipumba wa CUF, ambaye wafuasi wake walikuwa wakiimba mitaani Lipu, Lipu, Lipumba… alishika nafasi ya pili kwa kura 1,329,077. Mrema alianza kupata anguko la kisiasa akapata kura 637,077. Kilichofuata baada ya hapo kwa Mrema ni historia.

Mwaka 2005 Jakaya Mrisho Kikwete wa CCM alipata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28. Prof. Lipumba umaarufu wake ulibaki palepale akapata kura 1,327,125, huku Freeman Aikaeli Mbowe akisimama kama mgombea urais wa kwanza wa CHADEMA akapata kura 668,756 sawa na asilimia 5.88. Mwaka 2010 umaarufu wa Kikwete ulishuka akapata kura 5,276,827 sawa na asilimia 62.83, huku Dk. Wilbrod Slaa wa CHADEMA akipata kura 2,271,941 sawa na asilimia 27.05.  Prof. Lipumba upepo ulianza kukata akaambulia nusu ya kura alizokuwa anapata awali, yaani 695,667 za urais.

Mwaka 2015 ndio mwaka unaotajwa kuwa na historia ya kipekee katika siasa za vyama vingi kwa nchini Tanzania. Miaka yote wapinzani walikuwa wakilalamika kuibiwa kura, ila kwa mwaka 2015 waliongeza malalamiko ya ziada. Aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli alipata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46. Wakasema baada ya mawakala wa mgombea wa CHADEMA Edward Lowassa kuondolewa katika vituo vyote vya kupigia kura nchini, kura za Lowassa zilijisimamia bila wakala akapata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97. Hapa wakawa wanasema: “Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.”

Mwaka 2020 kila mtu anafahamu matokeo yalivyokuwa na utangulizi wangu unajieleza. Rais Magufuli alipata kura 12,516,252 ambazo ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa. Tundu Lissu wa CHADEMA akapata kura 1,933,271. Mtakumbuka hiki ndicho kipindi ambacho Tanzania imeshuhudia kesi nyingi za kisiasa mahakamani kuliko wakati wowote tangu nchi ipate Uhuru.

Kati ya mwaka 2015 na 2021 kwa Tanzania mtu kufahamika kuwa ni mfuasi wa chama cha upinzani, ghafla iligeuka laana. Baadhi ya Watanzania wakakimbilia nje ya nchi, na mtakumbuka wakuu wa wilaya na mikoa waliacha kujiita vyeo vyao hivyo, wakawa wanajiita wenyeviti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama!

Nchi ikazalisha wakuu wa mikoa vijana, waliokuwa wanadharau kila awaye, isipokuwa aliyewateua bila kujali umri wala nafasi yake katika jamii. Tanzania ikageuzwa kilinge cha kamatakamata. Hata makala kama hii kuiandika enzi hizo, ilikuwa tayari unajiandalia kesi bila kujua kosa lako kuwa ni kutoa mawazo au kusema ukweli hadharani.

Sitanii, Watanzania wakabaini kuwa Tanzania si salama tena. Baadhi wakakimbia nchi, waliokuwa na madaraka wakafanya kila walilotaka. Mikutano ya hadhara ikapigwa marufuku, watu wakawa wanapotea kama kuku aliyeliwa na vicheche; rejea Ben Saanane na Azory Gwanda wasiofahamika waliyeyukia wapi hadi sasa. Tundu Lissu akamiminiwa risasi. Leopold Kwemba Lwajabe aliyekuwa Mkurugenzi wa Miradi Wizara ya Fedha na wengine wakafa katika mazingira ya kutatanisha. Fedha zikawa zinachukuliwa kwenye akaunti za wafanyabiashara. Wee acha tu.

Hakika, kila mtu akakumbuka dhana ya kuwa Katiba ya Tanzania inatoa madaraka makubwa kwa Rais yasiyo na ukomo, jambo ambalo ni la hatari mno. Hata waliokuwa hawaoni umuhimu wa siasa, wakaanza kutamani ujio wa Katiba Mpya itakayoainisha mipaka na madaraka ya Rais na taasisi zake.

Sitanii, kumbe katika maumivu juu ya mambo yalivyokuwa yanakwenda tulikuwa wengi. Machi 19, 2021 nchi yetu ikapata Rais mpya, Samia Suluhu Hassan. Kwa hakika baada ya muda mfupi akaanza kufanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali. Akarejesha Uhuru wa vyombo vya habari, akiwa Marekani akatoa kauli kuwa atafanya mageuzi makubwa hata yakimgharimu urais wakati akigombea.

Desemba, mwaka 2021 ukafanyika mkutano wa wadau wa siasa, katika kuhakikisha waliyokubaliana yanatelekezwa akaunda Kikosi Kazi cha wajumbe 24 kikiongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala kutafuta majibu sahihi kuhusu mfumo wa siasa nchini, ikiwamo Katiba Mpya Tanzania tumekwama wapi. Rais Samia katika kuthibitisha nia yake ya dhati, Julai 1, 2022 ameandika makala na kuisambaza kwenye vyombo vya habari, ikiweka wazi nia yake ya kufanya mageuzi makubwa katika nchi hii.

Sitanii, nimeguswa na nukuu kadhaa za makala hii, hasa pale aliposema: “Si wakati wote ni wa kupongezana na si wakati wote ni wa kupingana. Kwenye kujenga Tanzania Bora ninatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Ninatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote.

“Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote. Ninaamini maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.”

Nukuu hii ina ujumbe mzito ndani yake. Dhana ya maridhiano anayoisema, tayari ameonyesha njia. Mara kadhaa amekuwa akisema ameunda Kikosi Kazi kisaidie kutoa mapendekezo yatakayoweka njia ya kurekebisha sheria, kusawazisha penye milima na mabonde. Naamini fursa hii Watanzania tukiitumia vema, tukatoa mawazo yetu yenye kushauri tunataka nchi yetu iongozwe vipi, tutokeje katika mkwamo wa Katiba na maeneo 9 yaliyoainishwa kwa ujumla wake, tutakuwa tumeitendea haki jamii yetu.

Uzoefu unanionyesha kuwa nchi zote ambazo zimekuwa na migogoro ya ndani kisiasa, migogoro hiyo humalizwa na wananchi wenyewe wanapoamua kukaa na kuzungumza. Tumeliona hili Zanzibar, tumelishuhudia kwa majirani zetu Burundi na hata Afrika Kusini, mzee Nelson Mandela alimpa jukumu la kusimamia mazungumzo Askofu Desmond Tutu, suala lililomaliza uhasama kati ya wazawa na makaburu nchini humo. 

Nafahamu kuna vyama vimeweka msimamo kuwa havitashiriki kutoa mawazo yao mbele ya Kikosi Kazi, lakini ukiniuliza nashawishika kushauri kuwa ni bora wahusika washiriki mazungumzo hayo waeleze yanayowakera kuliko kukaa nayo kifuani. Sina uhakika iwapo kiwango cha faida ya kukataa mazungumzo mbele ya Kikosi Kazi, inalingana na hasara ya kushiriki mazungumzo hayo (kama ipo).

Miaka 30 ya mfumo wa siasa za vyama vingi ni mingi. Kupitia Kikosi Kazi cha Rais, Watanzania sasa tunayo nafasi ya kupitia mfumo wetu wa kuendesha siasa baada ya miaka 30, tukasema iwapo unatufaa tuendelee nao na ikiwa hautufai, basi tueleze upi utatufaa. Rais Samia amefungua milango, tuitumie fursa hii kuandaa mazingira bora ya miaka 50 hadi 100 ijayo. Mungu ibariki Tanzania.