Dar es Salaam

Na Andrew Peter

Kama kuna jina lililopunguza furaha ya Wanayanga katika siku ya mwisho wa msimu huu, ni George Mpole.

Mpole, mshambuliaji wa Geita Gold. Aliwakatili mashabiki wa Yanga waliokuwa na imani ya kuona nyota wao Fiston Mayele akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Mpole katika mchezo wa mwisho wa ligi alifunga bao na kufikisha mabao 17 na kumpiku Mayele aliyemaliza msimu na mabao 16, huku Mkongo huyo akipata bahati mbaya baada ya bao lake dhidi ya Mtibwa Sugar kukataliwa na mwamuzi.

Kitendo cha Mayele kukosa tuzo ya ufungaji bora ilikuwa shangwe kwa mashabiki wa Simba ambao walianza kuwatania Yanga kwa kumsifu Mpole, jambo lililowanyima furaha kwa kiasi fulani mashabiki wa Jangwani pamoja na kutwaa ubingwa bila ya kufungwa msimu huu.

Simba walipata cha kuwatania Yanga kwa sababu wao katika misimu minne waliyotwaa ubingwa walifanikiwa na kutoa mfungaji bora, rekodi iliyoshindwa kufikiwa na watani wao msimu huu.

Kinara wa mabao, Mpole, tayari ameonyesha nia ya kutaka kujiunga na Simba. Sasa kazi imebaki kwa viongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi kumwita na kukaa mezani ili kuyajenga.

Sina tatizo na ndoto ya Mpole kutaka kujiunga na Simba kwa sababu atakuwa na uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa pia uhakika wa mshahara pamoja na posho nyingi kutoka kwa mashabiki.

Ila kwangu naamini ni mapema mno kwa Mpole kuitaka Simba, kwa sababu anahitaji kuthibisha tena akiwa na Geita kwamba hakubahatisha kufunga mabao 17 msimu huu.

Ufalme alioutengeneza Geita Gold ni tofauti kabisa akienda Simba, kwa sababu ya aina ya nyota wanaowasajili sasa. Itampa wakati mgumu kupata uhakika wa namba ya kucheza, jambo litakalohatarisha kipaji chake.

Naamini Mpole ana watu sahihi wa kumsimamia, wanachotakiwa kufanya ni kuona jinsi anavyoweza kuongezewa dau la mshahara pamoja na usajili ndani ya Geita ili kuendelea kuipigania timu hiyo.

Mpole bado hawezi kuhimili maisha na presha ndani ya Simba kwa sababu tumeona wachezaji wengi waliotoka katika klabu ndogo wakishindwa kutamba ndani ya kikosi cha miamba hao.

Miongoni mwa nyota waliokuwa tishio katika klabu zao lakini wameshindwa kutamba Simba ni pamoja na Elius Maguli, Martin Kaheza na Adam Salamba. Hawa si kwamba hawana vipaji, ila ushindani na ile sera ya kuaminiwa wageni zaidi ndiyo iliyowapoteza.

Ila hatuwezi kumzuia kwenda kutimiza ndoto yake Msimbazi, lakini anapaswa kujifunza vingi kutoka kwa wenzake kabla ya kukimbilia huko. Utapata fedha, haina ubishi, ila kipaji chako kinabaki njia panda.