*JAMHURI lilianika ukweli wote likatishwa * CAG amaliza kazi, Mpina apongezwa

DAR ES SALAAM

NA CLEMENT MAGEMBE

Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau amesema amefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kumsimamisha kazi Meneja wa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dk. Milali Machumu na bodi ya wadhamini wa taasisi hiyo.

Dau amesema hatua hiyo ni ya ujasiri mkubwa kwa kuwa walifikisha malalamiko yao sehemu mbalimbali kwamba MPRU iliikuwa ikiwaibia mapato yatokanayo na ada ya tozo la kiingilio kwenye maeneo yaliyochukuliwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.

Amesema wananchi wa Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani, walinyanyaswa na taasisi hiyo kwa kuporwa zana zao za uvuvi na kubambikikwa kesi ambazo hazina msingi wowote na baadhi yao wamefungwa.

Mbunge huyo amesema MPRU imekuwa na madudu mengi na hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kuchukua hatua dhidi ya mtendaji huyo na bodi yake ya wadhamini, lakini kwa hatua alizozichukua Waziri Mpina baada ya ripoti ya ukaguzi ya CAG kubaini kasoro za uendeshaji wa taasisi hiyo zinapaswa kuungwa mkono.

Pamoja na maelezo ya mbunge huyo, baadhi ya watumishi wa MPRU wamelieleza JAMHURI kuwa wamefurahishwa na hatua hiyo, kwani taasisi hiyo ya umma ilikuwa inaendeshwa kienyeji mno na Meneja huyo bila kuzingatia sheria na taratibu za kazi.

Watumishi hao ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini wamesema pamoja na Waziri kumsimamisha kazi Dk. Machumu na kutaka uchunguzi ufanyike ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake, anapaswa kuchunguza kitendo cha kuwafukuza kazi wafanyakazi wanne bila sababu za msingi.

Wamesema malalamiko ya watumishi wa taasisi hiyo yako wizarani kwa kipindi kirefu na aliyefikishiwa taarifa zinazohusu utendaji mbovu wa meneja huyo ambao uliendelea kuingizia hasara serikali ni aliyepewa jukumu la kuunda timu ya uchunguzi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba.

Wamesema taasisi hiyo ilikuwa inaongozwa bila timu ya menejimenti baada ya kuwaondoa wajumbe wote na wengine kuwafukuza kazi bila sababu za msingi huku shughuli za uhasibu zikiendeshwa na meneja akisaidiana na dereva wake.

“Dk. Budeba anazo taarifa zote za taasisi hii lakini alishindwa kuchukua hatua mapema hadi CAG alivyogundua kasoro nyingi. Sasa hatuelewi amepewa kuchunguza tuhuma anazozifahamu kwa muda mrefu atakuja na majibu gani?

“Watumishi wa taasisi hii tulikuwa tunaelewa kuwa MPRU  kwa uongozi wa Dk. Machumu haikujikita katika biashara ya utalii wa bahari kwa kuiingizia Serikali mapato na badala yake ikageuzwa taasisi ya kugawana fedha kwa baadhi ya watu,” ameeleza mmoja wa watumishi hao.

JAMHURI limemtafuta Dk. Budeba ambaye ameagizwa na Waziri Mpina kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Dk. Machumu bila mafanikio.

Wiki iliyopita Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alimsimamisha kazi Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk. Machumu kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ipasavyo kitengo chake.

Uamuzi huo ulikwenda sambamba na kuivunja Bodi ya Wadhamini ya taasisi hiyo baada ya Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuainisha mapungufiu 24 ambayo yanahusu kitengo hicho.

Waziri Mpina alieleza kuwa taarifa ya ukaguzi wa ufanisi katika Usimamizi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu imebaini udhaifu katika usimamizi wa hifadhi za bahari na maeneo tengefu.

Alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuunda kamati ya uchunguzi juu ya utendaji wa meneja aliyesimamishwa.

Mpina ameeleza kuwa udhibiti duni wa matumizi ya rasilimali za bahari katika maeneo tengefu ya bahari hususan Tanga na Mtwara haukuzingatia kanuni za utoaji wa vibali vya matumizi ya Serikali.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kulinda rasilimali za nchi na kusisitiza idara yoyote chini ya wizara yake kuhakikisha inafanya kazi kwa weledi.

By Jamhuri