Polisi yatamba kuwadhibiti ‘Wakorea Weusi’ Mbeya

Na Thompson Mpanji, Mbeya
Polisi mkoani Mbeya imetangaza kukidhibiti kikundi cha uhalifu cha vijana wanaojitambulisha kama ‘Wakorea
Weusi’, wakijihusisha na kujeruhi watu na uporaji mali za watu.
Kikundi hicho ni miongoni mwa makundi ya kihalifu yaliyoibuka hivi karibuni mjini hapa, na kutambuliwa kwa majina
tofauti, hali iliyozua sintofahamu na hofu kwa wakazi wa mjini humo.
Kufuatia hali hiyo, polisi mkoani Mbeya ilianzisha msako na kuwatia mbaroni vijana 42 waliokuwa wakituhumiwa
kwa uhalifu huo.
Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na kiongozi wa ‘Wakorea Weusi’, Kelven Raphael (22), mkazi wa
Mwakibete, Bombambili jijini humo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu
Kamishna Mohamed Mpinga, amesema udhibiti wa kundi hilo umefanikiwa kwa kushirikiana na wananchi.
Mpinga amesema polisi imewakamata vijana hao wa ‘Wakorea Weusi’ hivyo kupunguza hofu kwa wananchi.
Hata hivyo, Mpinga amekanusha uvumi ulioenea mjini hapa ukikihusisha kikundi hicho na masuala ya kisiasa, na
kwamba ni vijana wenye hulka ya ubakaji.
Inasadikiwa kwamba asili ya jina hilo ni mzozo wa muda mrefu wa kidiplomasia unaoongezeka kati ya Marekani na
Korea Kaskazini.
“Hawa vijana walianza kama timu za mpira katika maeneo yao na hawajatoka nje ya Mkoa wa Mbeya, ni vijana
wetu tunaoishi nao na nichukue nafasi hii kuwaomba viongozi wa mitaa na wananchi kuzidi kutoa ushirikiano
wanaposikia taarifa zinazohusiana na uhalifu,” amesema Mpinga.
Kwa mujibu wa Mpinga, kulikuwa na taarifa kwamba matukio ya uhalifu yalianza kutokea muda mrefu huku
wananchi wakishindwa kutoa taarifa kwa hofu ya kulipiziwa visasi pindi wanapofikishwa polisi au mahakamani”.
Mpinga ametoa wito kwa wamiliki wa biashara za vinywaji, kuheshimu sheria za taratibu za muda wa
kufunga unapowadia ili kuepuka kuwa vyanzo vya uhalifu.

1715 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons