Tujifunze kutunza muda

Faraja ya Raph W. Sockman inasema, “Msingi wetu wa matumaini ni kwamba, daima Mungu hamchoki mwanadamu.”
Katika makala ya leo nitazungumzia matumizi ya muda na vikwazo mwanadamu anavyokumbana navyo katika safari yake ya maisha. Ninaomba kukuuliza swali hili: Kama leo ndiyo ingekuwa siku yako ya mwisho ya kuishi hapa duniani ungefanya nini?
Jiulize. Martin Luther kwa upande wake alisema, “Hata kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho, bado ningefanya kazi ambayo ingezaa matunda kwa ajili yangu au kwa anayekuja nyuma yangu.”
Wakati wote muda ni rafiki wa ‘mafanikio’ na pia ni adui wa ‘mafanikio’. Jemedari Napoleon Bonaparte (1769-1821) aliyepata kuwa mfalme wa Ufaransa, alipata kusema, “Ipo aina moja ya jambazi ambaye sheria haipambani naye, lakini ndiye anayeiba kilicho cha thamani kubwa kwa mwanadamu – ‘muda’.
Tuutumie muda vizuri. Muda ni mjumbe wa Mungu, tuutumie muda vizuri. Jana iliyopita huwezi ukaifufua, wiki iliyopita huwezi kuifufua. Mwezi uliopita huwezi ukaufufua, mwaka uliopita huwezi ukaufufua.
Ukipoteza muda, muda utakupoteza zaidi. Napoleon alizoea kuwaambia wanafunzi wake kuwa kila saa unayopoteza ni fursa ya kuwa na balaa baadaye. Ukichagua kuchezea muda huwezi kukwepa matokeo yake ambayo siku zote ni mabaya tu. Muda ni mali.
Ni vizuri kuthamini muda. Ukitaka kujua umuhimu wa mwaka mmoja muulize mwanafunzi ambaye amerudia darasa, ukitaka kujua umuhimu wa mwezi mmoja muulize mwanamke aliyejifungua mtoto kabla ya mwezi mmoja na ukitaka kujua umuhimu wa juma moja muulize mhariri wa gazeti linalotoka kila wiki. Ukitaka kujua umuhimu wa siku moja muulize mtu mwenye kibarua cha kulipwa kwa siku wakati ana watoto kumi wa kulisha.
Shujaa wa Afrika, Nelson Mandela, aliwahi kutuasa kuwa inatupasa tutumie muda vizuri na siku zote tukumbuke muda huenda sahihi. Kila siku unayopata kuishi hapa duniani ina umuhimu wake.
Methali ya Kifaransa inaeleza kuwa ‘hazina zote za duniani haziwezi kurudisha fursa moja iliyopotea.’ Utajiri wote wa ulimwengu hauwezi kurudisha nyuma dakika moja iliyopotea. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.
Kesho yako haiwezi kuongelewa bila leo yako. Leo ni akiba ya kesho. Kesho ni mavuno ya leo. Unachopanda leo ndicho utakachovuna kesho. Izungumzie kesho yako kwa kuiangalia leo yako. Padri Dkt. Faustin Kamugisha anasema, “Tusiiogope kesho kwa vile matunda ya kesho yamo kwenye mbegu za leo, leo tuishi vizuri ili kesho iwe ya maana”.
Huwezi kukwepa kuwajibika kesho kwa kukwepa kuwajibika leo. Kesho hujaiona na hujui itakuaje lakini uamzi wako unaweza kuiharibu kesho yako au unaweza kuujenga wako.
Leo uko pale ambapo mawazo yako yamekuleta, kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yamekupeleka, jenga leo yako vizuri ili uifurahie kesho yako. Mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, anashauri kwamba, ‘Leo lazima iwe bora kuliko jana, na kesho kuliko leo, la sivyo kuna tatizo.’
Kila mara kuna watu wanaotaka kuishi kesho, lakini wanashindwa kuifurahia leo, maisha yetu yawe na mwelekeo, tusiishi kwa sababu tu tumepata fursa ya kuishi, tusiishi kwa dhana ya kuyajaribu maisha, maisha hayajaribiwi.
Kanuni ya maisha ni kwamba hakuna aliyewahi kufika na wala hakuna aliyechelewa kufika, bado milango iko wazi kwa yeyote, juhudi zako ndizo zitakazokufikisha pale ulipopakusudia kufika.
Katika maisha kuna mambo mengi, mengine ni magumu, na mengine huumiza sana moyo. Jifunze kuuambia moyo wako kuwa, nijapopita katika kipindi kigumu cha maisha sitayumba, sitarudi nyuma, sitakata tamaa, wala sitapoteza matumaini yangu nitasonga mbele kwa jitihada, kwa ujasiri, kwa matumaini, kwa malengo, na kwa imani.
Pale unaposema hapa nimefika mwisho, Mungu anasema huu ni mwanzo mpya, usikate tamaa kwa sababu ya mazingira, watu wabaya au kipato. Amini unaweza na utaweza daima. Mwandishi Frank Gaines anasema, “Tutakapojifunza tu kuona lisiloonekana, tutajifunza kutenda lisilowezekana.”
Badili namna yako ya kuyatafsiri maisha. Mwandishi Jim Clair anasema, “Yasiyowezekana ni mambo rahisi sana kwa Mungu kuyatatua.” Mshirikishe Mungu katika mipango yako ya maisha, mshirikishe Mungu katika mapito yako ya maisha.
Kila tatizo ni zawadi, bila matatizo tusingekuwa. Kumbe matatizo ni fursa! Ili uishi ni lazima uteseke, na ili uteseke ni lazima uwe unaishi. Tunapoishi mara moja hapa duniani ni lazima tutateseka.
Nakubaliana pia na John W. Gardner aliyesema, ‘Kutokuwapo kwa matatizo kabisa kungekuwa chanzo cha kutoweka kwa jamii au mtu binafsi.’ Hatukuumbwa kuishi kwenye dunia ya namna hiyo. Kimaumbile sisi ni watatuzi wa matatizo na watafutaji wa matatizo.
Mateso katika maisha siyo laana, ni changamoto, mateso katika maisha ni mwalimu asiyeonekana lakini bora zaidi kuliko wale wanaoonekana. Wakati unapokuwa unakabiliwa na mateso usiulize, kwa nini mimi, badala yake uliza, Mungu unataka nijifunze nini?
Mateso katika maisha ni baraka usiyoweza kuipokea ukiwa unacheka. Ukweli wa maisha ni kwamba binadamu hapendi kuteseka, lakini mateso ni bahati inayojitokeza kwanza katika sura ya balaa, kwa hakika mateso katika maisha ni changamoto, tena ni changamoto inayoyumbisha akili, roho na upendo.
Wakati wa mateso tunabaki na labda nyingi. Tunabaki na hoja nyingi akilini, tunajiuliza, kwa nini mimi? Nimemkosea nini Mungu? Kuna haja gani ya kuishi kwa kumtumainia Mungu. Katika maisha unahitaji watu watakaokuzomea ili umkimbilie Mungu, unahitaji watu watakaojaribu  kukutakia hofu ili uwe na ujasiri, unahitaji watu watakaosema hapana ili ujifunze mbinu mpya ya mafanikio.
Unahitaji watu watakaokukatisha tamaa ili uweke matumaini yako kwa Mungu. Unahitaji watu watakaokufanya upoteze kazi yako ili uanzishe biashara yako. Hayo yanaitwa mapito ya kuelekea njia ya mafanikio.
Padre Dkt. Faustine Kamugisha anasema, ‘tukubali tunapoteseka hatuwezi kufahamu na kung’amua barabara mipango ya Mungu juu yetu.’ Kibinadamu wakati wa mateso ni wakati wa ukiwa, sononeko, huzuni, giza, lawama, lakini wakati wa mateso kwa binadamu ndiyo wakati wa kujiandaa kupokea yale aliyoyatumainia na kuomba kwa muda mrefu.
Tusinung’unike wakati wa mateso, tusiogope, tusonge mbele. Wakati wa mateso tunaalikwa kuzungumza na Mungu, kuwa naye karibu, kumuuliza kulikoni Baba? Mara nyingi watu wanaoishi maisha ya uadilifu wanateseka sana na kusakamwa na jamii ya watu. Hii ni ishara njema kwao hata kama wanateseka na kusakamwa na jamii ya watu.
Mateso siyo mwisho wa safari yako ya kiroho, kiuchumi na kisiasa. Wakati wa mateso tusiwe kama kuku. Kwenye kura ya maoni kuhusu ama sherehe za Krismasi zifanyike au zisifanyike, kuku wanaweza kupiga kura ya zisifanyike. Tusipige kura ya kuyakataa mateso katika maisha yetu.
Nidhamu inafunzwa katika shule ya mateso. Katika hali ambayo inathibitisha kwamba mateso ni mtaji katika maisha, Jawaharlal Nehru ameandika; “Mtu asiye na furaha ni yule ambaye hajawahi kupata taabu, taabu kubwa sana katika maisha ni kutokuwa na taabu kamwe.” lakini Titus Livy 61 AD anaandika; ‘Mateso huwafanya watu wamkumbuke Mungu.’
Maisha ni shule ambamo kila majonzi, kila maumivu, kila jambo la kuvunja moyo huleta fundisho kubwa. Mungu angeweza kuzuia Yusufu asitupwe gerezani [Mw 39:20-22]. Angezuia Danieli asitupwe kwenye shimo la simba [Dan 6:16-23]. Angezuia Yeremia asitupwe katika shimo la matope [Yer 38:6]. Angezuia Paulo asivunjikiwe na jahazi mara tatu [2Kor 11:25]. Angewazuia vijana watatu wa Kiebrania wasitupwe katika tanuri la moto [Dan 3:26].
Hakufanya hivyo, aliruhusu mateso yawapate. Mateso katika maisha ni baraka usiyoweza kuipokea ukiwa unacheka. Maisha yana maana pale tunajitambua na sisi kwamba tuna umaana. Yape maisha yako tafsiri sahihi, usiishi kama kwamba umelazimishwa kuishi.
Neno ‘haliwezekani’ tulitumie kwa uangalifu mkubwa katika maisha yetu. Jambo baya kuliko yote siyo kifo, lakini ni kuishi maisha yasiyo na malengo. Bilionea wa Afrika, Aliko Dangote, anasema; ‘Mtu asiye na malengo hana sababu ya kuishi’.
Mtu asiye na lengo ni kama meli bila usukani. Mtu aliyepotea, mtu kabwela, mtu bure. Neno ‘haiwezekani’ limewafanya binadamu wengi kuishi maisha yasiyo na malengo. Haiwezekani ni neno linalokutwa katika kamusi ya wapumbavu.
Mafanikio yanahitaji maandalizi, mtu anayeweza kukuokoa wewe ni wewe. Ni wewe unayeweza kujiandikia historia nzuri au mbaya, ni wewe unayeweza kuwa chachu ya mabadiliko au mhanga wa mabadiliko, unaishi maisha yako, huishi maisha ya mtu mwingine. Maisha ni kuanguka na kuinuka, ukianguka inuka. Ukianguka amini unaweza bado kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi.

0789 090828/0719 700446