Katika kipindi cha wiki moja, tasnia ya habari imepata pigo kubwa kwa kuwapoteza wapiganaji wake wawilikatika tasnia hii.
Kwanza alikuwa ni Samwel Chamulomo, aliyekuwa Mtangazaji wa TBC Kanda ya Kati, mauti yalipomkuta akiwa mkoani Dodoma. Pili ni Sophia Yamola, mwandishi wa habari za siasa na uchunguzi, aliyefariki Mei 21, mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo, Dar es Salaam.


  Katika makala hii, nitamzungumzia zaidi Sophia Yamola, niliyemfahamu zaidi kutokana na ukaribu wetu kikazi na kibinafsi. Nilimfahamu Sophia kabla ya kujiunga na tasnia hii ya habari. Alikuwa mcheshi na mtukutu hasa kupenda kupekenyua na kufahamu undani wa jambo husika.
Katika kipindi kifupi alichokuwa katika tasnia ya habari nchini, niliweza kufanya kazi naye katika Gazeti la Dira ya Mtanzania, ambapo nilijifunza mambo mengi kutoka kwake.  


Mpekenyuzi kama alivyopenda kujiita, alikuwa mtu mwenye msimamo, asiyependa kuona mtu yeyote akionewa na kunyimwa haki yake. Alikuwa mtetezi wa haki za watu ingawa nasikitika alishindwa kutetea haki yake ya kumwezesha kuishi kila mwezi. Anaondoka duniani akiacha wadeni wake wengi.
Naumia zaidi pale nilipokuwa naye akilalamikia haki yake na kuuliza nini afanye ili apate haki yake hiyo! Alilalamika kwa kuishi kwa kujinyima huku jasho lake likishindwa kulipwa tangu mwaka jana.
Alipokuwa hospitalini amelazwa, mara kwa mara alikuwa akiulizia malipo yake ambayo, hata hivyo, hukuweza kuyapata mpaka mauti yanakukuta.


314733_596041430411663_2080180472_nSophy aliyekuwa na ndoto ya kuwa mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Chato, aliweza kujikita katika siasa kwa madhumuni ya kuendelea kuwatetea wanyonge kupitia fursa nyingine ya ubunge. Kutokana na dhamira yake hiyo, alifanikiwa kuwa na kushika nafasi kubwa katika Chama cha Wazalendo (ACT) akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Na matarajio yake ilikuwa Juni, mwaka huu, kwenda Chato kuhakikisha anasambaza uzalendo kwa ndugu zake.


Rafiki yangu, ndugu yangu na mwanataaluma mwenzangu ndoto zake zimezimika ghafla na sasa amerudi Chato akiwa amelala, amelala Sofia, amelala mpekenyuzi usingizi usio na kikomo.
Sophia, mwandishi wa habari, mpambanaji aliyeonja machungu ya baadhi ya waajiri wasiothamini jasho la wafanyakazi wao, waajiri wanaojiona miungu-watu, walio tayari kuona wanawatumikisha watu bila kuwalipa ujira wao japo kuwa ni kidogo.


Sophia amekufa huku akililia mshahara wake wa miezi mitatu aliotakiwa kuwa amelipwa tangu Januari mwaka huu. Tunamlilia mpekenyuzi aliyeniuliza ni lini haki zetu zitapatikana wakati huo akiwa Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo, alilalamika kwa kutolipwa fedha hiyo ambayo ingemsaidia kununua japo machungwa. Sophy, kama nilivyokuwa nimemzoea kumwita, alikuwa mpambanaji, aliyekuwa tayari kuchimbua mambo mengi na kuhakikisha anahabarisha umma wa Watanzania kuhusiana na mambo husika.


Wanahabari wanamlilia, wanajiuliza maswali yasiyo na majibu. Mama yake analia kwa kupoteza nguzo yake na rafiki yake. Wadogo zake wamepatwa na mshangao kama wanaoamini kuwa kunyamaza kwake ni kwa muda tu.
Watoto wake – Marry na Suzy – hawaelewi nini kimempata mama yao, wamepigwa na butwaa kuona ugeni mkubwa nyumbani kwao.


Katika harakati zake za kusaka ubunge, Sophia alikuwa akinitania mara kwa mara kuwa nitakuwa katibu wake baada ya kuukwaa ubunge, na atahakikisha anaboresha maisha ya wana-Chato kwa kutumia rasilimali zilizopo katika Mkoa mpya wa Geita.
 Tunamlilia Sophia wetu, tunamlilia rafiki na kipenzi cha wote, tunamlilia mpambanaji mwenzetu. Ni vigumu kuamini kuwa amenyamaza, amenyamaza milele katika masikio yetu.  


 Pamoja na kulala kwake, kunyamaza kwake ataendelea kuwa mpekenyuzi katika mioyo yetu. Nitaendelea kuyaenzi yale yote aliyoyafanya hasa katika suala la kupigania na kutetea haki za wanyonge. Ila daima namuahidi kuhakikisha nitadai jasho langu kwa nguvu zote. Nitadai haki yangu daima, maana haki haiombwi bali hudaiwa hata kama mdaiwa hafurahishwi na jambo hilo.
  Sophia alikuwa mpambanaji aliyeweza kuhakikisha anapeleka umeme kijijini kwao Kigamboni, ambapo alihakikisha umeme huo unafika na si kuishia kwenye nyumba ya kigogo mmoja tu huku wakazi wengine wakiishia kuwasha vibatari.


Alipambana, akamtafuta Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Profesa Sospeter Muhongo, ambapo alifanikisha mapambano hayo na umeme kuweza kufika nyumbani kwake pamoja na nyumba jirani ambako walikuwa tayari wamelipia huduma hiyo. Majirani zake wanamlilia, wanamlilia mshauri wao, mpambanaji na rafiki yao mpenda maendeleo aliyeondoka. Ameondoka Sophia bila kumalizia malengo waliyojiwekea.


Amenyamaza Sophia, amenyamza milele. Hatutoweza tena kusikia sauti yake, ucheshi wake na hata utani wake usiokwisha huku akichombeza na mbwembwe.
Nimezoea kukutana naye na kuzungumza mambo mengi, siwezi tena kumwona na kuzungumza naye. Ameondoka Sophia mpambanaji asiyekatishwa tamaa.
 Ninayo mengi ya kumwelezea ila mikono inatetema, mwili unaishiwa na nguvu, akili inakataa kukubali kunyamaza kwake. Nenda Sophy, tangulia kamanda, mbele yetu, nyuma yako.
Mwenyezi Mungu amlaze mahala Pema Peponi Sophy.

By Jamhuri