Inawezekana leo ninaelekea kujadili mada inayochanganya kidogo. Ili kuijadili vizuri mada hii nitamtumia mwanafalsafa Plato, aliyeona kwa mara ya kwanza ukweli juu ya vivuli na vitu halisi. Na ili kupambana na ulemavu wa fikra, ni muhimu kubungua bongo mara kwa mara.

Plato ndiye mwanafalsafa aliyeanzisha Astria ya Pango. Astria hii ndiyo iliyoendelea hadi kuonyesha ukweli kwamba kuna vitu vinavyodumu na vile vinavyopita. Kwamba vingine ni vivuli na vingine ni vitu halisi, ukweli na vitu visivyobadilika milele yote.

Mfano, upendo ni kitu kinachodumu milele yote. Watu wanaopendana wanakuja na kupita, lakini upendo upo pale pale. Au ubaya. Watu wanatenda ubaya na kushiriki ubaya. Watu hawa wanakufa na kupita, lakini ubaya unabaki palepale. Hata kama tungefanikiwa kuwamaliza wabaya wote, ubaya utabaki katika wazo la ubaya, na endapo atachipuka tena mtu mbaya, atashiriki  ubaya katika wazo la ubaya!

Dokezo hapa ni kwamba, muhimu ni vitu vinavyodumu. Vitu visivyopita. Ni lazima tuwekeze nguvu zetu zote na akili zetu zote kwa kushughulikia na kuvielewa kwa kiasi kikubwa vitu visivyopita, vitu halisi na si vivuli. Tuwekeze kwenye upendo wenyewe zaidi ya kuwekeza kwenye watu wapendanao. Tuwekeze kwenye kuelewa na kufahamu kwa undani ubaya, zaidi ya kushughulikia watu wabaya au watu wenye kutenda ubaya. Watu wanapendana na kuachana, lakini upendo uko pale pale.

Plato katika nadharia ya Astria ya Pango, anajaribu kutengeneza picha ya watu ambao walizaliwa pangoni au shimoni na wanaishi huko kuanzia utoto wao hadi ukubwa wao. Huko pangoni wapo peke yao. Na maisha yao yote ni ya pangoni. Nje ya pango kuna watu wakiwa na mishumaa ikiwaka wanapita huku na huko. Mwanga wa mishumaa huakisi sura za hao watu wapitao na kutoa vivuli vyao. Vivuli hivyo hutokea katika ukuta wa shimo au pango ambamo wamo watu waishio humo maisha yao yote. Ingawa hivi vivuli huashiria uwepo wa watu nje ya hilo pango, wao huona hivyo vivuli kama ndio watu wenyewe. Hii inatokana na ukweli kuwa katika maisha yao, hawajawahi kuona tofauti kati ya watu na vivuli vyao.

Kwa maoni ya Plato, watu hawa waishio kwenye pango, wataamini daima kwamba vivuli ndivyo vitu halisi. Hii astaria ya pango ilimfikisha Plato katika hatua ya  nadharia ya mawazo. Hii inajulikana kama Nadharia ya Plato ya Mawazo. Kwa ujumla nadharia ya mawazo ni ule ukweli ambao haubadiliki au una hali ya umilele na haina hali ya umaada ambapo vitu vyote vijavyo kwetu katika hali ya umaada huja kama vivuli vyake. Katika nadharia ya mawazo Plato anasema kuwa wazo ni kitu ambacho hakibadiliki, kipo milele na wala hakuna sura ya mwili. Na kutokana na hili wazo, vitu vyote tuvionavyo ni vivuli vya hilo wazo au hayo mawazo.

Astria ya pango au hadithi ya mfano wa watu walioishi maisha yao yote pangoni, inatoa picha halisi inayoonyesha mfumo wa maisha ya watu wengi. Kadiri ya Plato, idadi kubwa ya watu wanaishi katika maisha ya giza shimoni. Mfumo wa kufikiri wa hawa watu ni wa fikra vivuli, kwani mtandao mzima wa muundo na mjengeko wa mawazo yao hauendi zaidi ya kile kinachoonekana machoni pao. Namna yao ya kufikiri haivuki mipaka ya maonekano na mapokeo. Hivyo kulingana na Plato, ni elimu peke yake ambayo inaweza kuwatoa hawa watu kutoka kwenye maisha ya kivuli kwenda kwenye  ulimwengu wa mwanga.

Elimu kadiri ya Plato si tu jambo la kusoma vitabu mbalimbali na kupata shahada, bali ni hali ile inayomfanya mtu awe na uwezo wa kujua ukweli kama ulivyo na kuishi kadiri ya misingi ya hiyo elimu. Kwa kadiri ya Plato, elimu ni lazima imfanye mtu abadilike kutoka kwenye ulimwengu wa kivuli na kwenda kwenye ulimwengu wa mwanga.

Na kwamba mtu akishapata mwanga, atakuwa hajapata elimu ya kweli kama hatachukua jukumu la kuwafundisha wengine. Kwa maneno mengine, mtu mwenye elimu ya kweli ni yule anayeipata elimu akatoa elimu. Mtu anayeipata elimu akabaki nayo anakuwa bado yuko gizani, pangoni!

Hapo ndipo tunapojadili kwa kina maana nzima ya ulemavu wa fikra. Mtu mwenye elimu ya kitu chochote kile, asipoisambaza kwa wengine, huyo anakuwa mlemavu wa fikra. Kwa mawazo ya marehemu mzee Mengi, ni mara mia kuwa na walemavu wa viungo, kuliko kuwa na walemavu wa fikra.

Tumewaona walemavu wengi wa viungo ambao wameweza kuisambaza elimu waliyonayo kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii husika. Elimu, inaleta mabadiliko kwa mhusika na jamii inayomzunguka. Hiyo ni elimu halisi na wala zi kivuli cha elimu.

Mfano mwingine ni kwamba mtu aliyeelimika ni yule anayetambua kwamba wapendanao ni kivuli cha upendo. Kwamba upendo ndiyo kitu halisi, upendo ndio  ukweli, na upendo ndio kitu kisichobadilika. Wapendanao wanaweza kuachana, wanaweza kufa, lakini upendo upo palepale. Upendo hauwezi kupungua au kuongezeka kwa vile watu wengi au watu wachache wamependana. Sisi tutapendana na vizazi vijavyo watapendana. Ni kitu cha kudumu milele yote.

Mtu, aliyeelimika ni yule anayeshughulika na vitu visivyopita. Ni mtu yule anayeshughulikia heshima, kuliko kushughulikia watu wanaoheshimiana, ni mtu anayeshughulikia upendo kuliko wapendanao, na ni yule anayeshughulikia Utanzania kuliko kuwashughulikia Watanzania. Si kwamba anawapuuza Watanzania, hapana, ila kwake kitu cha msingi ni Utanzania. Mtu anayetanguliza Utanzania, atawahudumia Watanzania wote bila kuangalia kabila, sura, cheo au hali ya mtu.

Mtu, anayetanguliza Utanzania, atatenda haki wakati wote, atawapenda Watanzania wote na atawahudumia Watanzania wote. Sote tukishughulika na Utanzania, Tanzania yenye neema inawezekana leo, kesho na keshokutwa.  Tanzania yenye neema kwa vizazi vijavyo inawezekana pia. Hivyo ni muhimu kwetu sote kukazana kuisaka elimu, elimu ya kweli ya kutuletea mwanga na kututoa gizani.

Hoja kubwa hapa ni kwamba, tuna kazi kubwa ya kupambana na ulemavu wa fikra. Mzee Mengi, ametuachia katikati. Yeye alikuwa akilielezea jambo hili kila mwaka wakati wa tukio la kupata mlo wa mchana na watu wenye ulemavu wa viungo. Ilikuwa ni njia ya pekee ya kuwakumbusha Watanzania kwamba ulemavu mbaya ni ule wa fikra.

Tunahitaji mtu mwingine wa kutukumbusha jambo hili. Tunamhitaji mzee Mengi mwingine. Ili tutoke kwenye kuishi na kutukuza vivuli na kuishi vitu halisi. Nguo ya kijani kwa mwanachama wa CCM, si muhimu zaidi ya chama chenyewe, zaidi ya itikadi na ilani ya chama hicho.

Na kwa mapana chama cha siasa si muhimu zaidi ya Taifa letu la Tanzania. Rangi ya nguo za vyama itakuja na kupita, vyama vyenyewe vitakuja na kupita, lakini taifa letu la Tanzania litabaki na kudumu. La kushangaza, sisi tunashabikia sana vivuli, tunashabikia rangi za nguo za vyama, tunashabikia vyama vya siasa kwa nguvu zote zaidi ya ushabiki wetu kwa taifa letu la Tanzania.

Mungu ametuumba tumtambue yeye na kumsikiliza na kuyaishi maisha halisi na wala si kuishi vivuli vya maisha. Mungu, ametupatia utashi na akili ili tuweze kupamba na ulemavu wa fikra na kuikumbatia fikra pevu. Na kwa jambo hili, hatuihitaji polisi wala mwanajeshi, hatuhitaji bunduki, mabomu wala mizinga. Ni kila mtu kujitambua na kupambana kujikomboa kutoka maisha ya vivuli, kujikomboa kutokana na ulemavu wa fikra. Elimu nzuri, elimu ya ukombozi wa kifikra inaweza kuwa mkombozi wetu.

By Jamhuri