Ndugu Rais, Bashiru Ally ni wa fungu lipi?

Ndugu Rais, fikra za walio timamu hazijadili watu. Hujadili fikra pevu za watu walio timamu. Kwa walio wengi mpaka leo hawajaelewa ilikuwaje mpaka ndugu Bashiru Ally akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Namfahamu tu kwa mawazo yake ya kufikirisha hasa tulipokuwa tukichangia pamoja hoja mbalimbali katika vyombo vya habari vya kimataifa kama DW, BBC, VOA, Radio France International na vingine. Ni mtu makini.

Mzee wangu mstaafu akaniuliza: “Bashiru anaonekana kijana, lakini mbona fikra zake ni kubwa mno?’’ Nikamwambia wingi wa busara hautegemei ukubwa wa kichwa. Ni zamani ambapo kuwa na mvi kichwani ilikuwa ni ishara ya busara.

Ndugu Rais, uteuzi wa ndugu Bashiru haukuwa wa bahati mbaya. CCM ilikata mti ikapanda mti. Katika kitabu cha ‘The Peoples’ Schoolmaster’ imeandikwa: ‘Tausi mzuri hahitaji mapambo.’ Bashiru hana vikundi. Hahitaji wapambe. Kifikra anajitosheleza. Katika baadhi ya nchi nyingine za Afrika watawala walipojiridhisha kuwa wamewatenda wananchi wao uovu mwingi, nao hawatakiwi tena, walijiundia vikundi vya ‘mavuvuzela’ ambavyo kazi yake ilikuwa ni kupandikiza chuki katika jamii na kuwatukuza kifalme. Uchaguzi mkuu ulipofika maandiko yaliyoandikwa katika Biblia yalitimia. Kwa kuwatuma wapumbavu walijikuta wamejikata miguu nao sasa wanakunywa hasara.

Ukora wa awamu ya nne ulikifuta kabisa Chama Cha Mapinduzi katika vifua vya baadhi ya wananchi. Kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu aliyepita Komredi Abdulrahman Kinana, kukirudishia chama uhai katika mawazo ya Watanzania, ilikuwa ngumu, kubwa, sawa kabisa na kazi iliyofanywa na muasisi wa CCM, Julius  Nyerere ya kuyaotesha mawazo katika vichwa vya Watanzania makini yaliyofanikisha na hatimaye kupatikana wanachama.

Tunaweza kwa upofu wetu leo tukampuuza Abdulrahman Kinana kwa sababu wahenga walisema ‘ivushayo mbovu’. Wengine bila Kinana hata tusingezijua ofisi tunazozishikilia na kujidai nazo leo. Kinana, aliacha viyoyozi na mwanga wa stima katika nyumba za waliobarikiwa, akaenda kulala katika nyumba za mbavu za mbwa ili ainyoshe njia ya ushindi wa CCM yake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alitembea kijiji baada ya kijiji nchi nzima, akila matembele na kunywa maji ya visima, akihubiri amani, undugu na umoja katika nchi. Alikuwa msikivu mtu yule mfano wake sijapata kuona. Kinana aliikosoa serikali hadharani. Akawaita mawaziri wabovu mizigo. Wajumbe waliokuwa wakipitisha jina la mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015 walilipuka kumshangilia Kinana kwa kazi kubwa aliyokifanyia chama huku wengine wakimwita jembe.

Bashiru umesema, yapo mambo mengi sana tena makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ambayo mnataka wabunge wa CCM wakawaeleze wananchi ili wajue faida zake kwao na jinsi gani inaweza kusaidia kuinua uchumi wao; wajue muunganiko kati yao na miradi hiyo mikubwa ili wajue faida zake.

Moyo wangu ulinidunda kwa nguvu. Mbunge wa Morogoro, wilayani Kilosa katika Shule ya Msingi Msowelo, atamwambia nini Mwalimu Elizabeth Mbilinyi ilichofanya Serikali ya Awamu ya Tano wakati anafundisha watoto 342 katika darasa moja, na wote wakiwa wamekaa chini kwa kukosa madawati? Kama mmejenga hospitali za kisasa kila kona, Mbunge wa Mbagala Zakhem atasema nini, kwa sababu kweli TV ndani ya hospitali zipo, lakini hakuna dawa wala vifaa tiba vya kutosha.

Nilisimama katika shule moja ya msingi (ukweli ni katika magofu) nikitokea Ifakara. Wazee wenye hasira walinizingira wakidhani mimi ni sehemu ya uongozi wa nchi hii. Hasira waliyokuwa nayo, ole wake mbunge atakayediriki kuwaambia kuna faida wanayoipata kutokana na miradi yenu mikubwa ambayo baadhi yao wanaiona ndiyo sababu ya maisha yao kuwa magumu.

Watakaorudi salama watakuwa wachache. Wazee wamepigika mpaka wanatisha. Tangu wazaliwe mpaka wanazeeka hawajawahi kuiona ndege imesimama ardhini, leo uwaambie umewanunulia ndege kwa pesa yao wenyewe ambayo ingewalegezea ugumu wa maisha, wewe, hujitaki?

Barabara zao kuna msimu hazipitiki, wewe uwaambie unawajengea treni kwa pesa zao ambazo zingewasaidia kupata huduma za afya ambazo leo hawazipati. Watu hawawezi kununua hata kijiko kimoja cha mafuta ya taa kwa ajili ya vibatari vyao, uwaambie fedha yao karibu yote inatumika kuchimba umeme sijui Mtwara, wakati wanajua nyumbani kwako umeacha umeme mpaka wa ziada. Kaka Bashiru hapo kitaeleweka kitu?

Kaka Bashiru ulipoagiza kuwa: “Kama yuko mwananchi au wananchi wenye shida au kero ambazo wamepita nazo kila mahali, na hawakusikilizwa waniletee mimi. Na huko hakutakuwako kuvuka mstari. Simu yangu iko wazi saa zote.’’ Watu wako tumekusikia na kufarijika sana. Kumbe yuko mtu katika CCM hii hii anayejali wananchi? Laiti ningeijua simu yako kaka Bashiru, ningekuletea shida ya watoto wetu walioko katika shule mbalimbali. Wazazi, wadau wa elimu na Watanzania wenye upendo kwa taifa la kesho, wamekwenda kila mahali walipoweza, kupeleka kilio chao watoto kukosa vitabu shuleni, lakini hakuna walikosikilizwa.

Kaka Bashiru watoto wa taifa hili hivi sasa hawana vitabu shuleni. Imefikia watoto zaidi ya 100 kutumia vitabu vitatu tu. Kinachouma zaidi kaka Bashiru si kwamba vitabu havipo nchini. Wachapishaji wana vitabu vingi vimejaa kwenye maghala yao hawana pa kuvipeleka. Vitabu hivi vimethibitishwa kuwa vinafaa kutumika shuleni na Wizara ya Elimu. Wachapishaji wako tayari hata kuvisambaza mpaka shuleni. Kwa kusema kero ambazo hazijasikilizwa popote ziletwe kwako umekuwa kama mkombozi uliyetumwa na Mungu. Kaka Bashiru kilio cha wazazi wa taifa hili kuhusu ukosefu wa vitabu kwa watoto wao walioko shuleni, kikufikie.

Sikiliza kilio cha watoto wa taifa hili ambao sasa wamekosa vyote, sauti na mtu wa kumlilia. Kaka Bashiru kilio cha wadau mbalimbali wa elimu katika nchi hii kikufikie. Elimu sasa ni sawa na msiba. Ni matumaini ya wengi kuwa kilio hiki kimekufikia, nawe hautawaacha yatima watoto hawa bali utawapangusa machozi yao. Baba, wamelia mpaka macho yamewavimba!