Mkoa wa Geita, ambao umetawaliwa na shughuli za uchimbaji madini, sasa unakabiliwa na changamoto za usalama kazini katika machimbo yanayowahusisha wachimbaji wadogo.

Moja ya matukio hayo ni pamoja na lile lililotokea usiku wa kuamkia Januari 26, mwaka huu ambapo watu 15 – mmoja akiwa raia wa China – walinusurika kufa kwa kufukiwa na kifusi katika mgodi wa RZ Union, unaomilikiwa na Ahmed Mbarack kwa kushirikiana na raia wa China.

Mgodi huo ni mmoja kati ya migodi 850 yenye leseni ya uchimbaji mdogo mkoani humo. Mgodi huo upo katika Kijiji cha Mawe Meru, Kata ya Nyarugusu, Geita. 

Mmoja wa watu waliokuwa wamefukiwa na kifusi ndani ya mgodi huo, na kukaa ardhini kwa zaidi ya siku tatu, huku wakiishi ardhini huko kwa kula biskuti na uji, alizungumza na JAMHURI.

Akizungumza na JAMHURI, Magalula Kayanda amesema hali yao ilikuwa mbaya na mwenzao mmoja alishakata kauli lakini maji yaliwafanya wawe na nguvu.

Amesema waliingia mgodini saa nne usiku, na kuanza shughuli za uchimbaji na saa nane usiku walisikia kishindo kikubwa huku wakisikia sauti kwa mbali, sauti hizo zilitoka kwa wenzao waliokuwa nje ya mgodi, wakiwaita watoke nje.

“Tukiwa ndani ya mgodi zaidi ya mita 100 ardhini, tulisikia tukiitwa na waliokuwa nje wakitueleza tusogee kunatitia, baada ya kusikia wote tukakaa sehemu moja na ghafla umeme ukakata, kukawa giza hakuna mawasiliano na hewa ikawa haiingii,’’ amesema Kayanda.

Huku wakiwa hawajui cha kufanya kutokana na hali halisi ya kutitia kwa mgodi huo, changamoto kubwa ilikuwa namna ya kupata hewa kutokana na mifumo kuharibiwa, ghafla mpira mmoja wa kupitisha hewa ulianza kufanya kazi na kuwapa tumaini jipya la kuishi.

Mchimbaji mwingine, Jackson Lucas, amesema walikuwa umbali wa mita 100 ardhini.  Lucas anasimulia kwamba hali mbaya ya hewa ikichangiwa na harufu ya kinyesi ilikuwa moja ya changamoto ya kukaa katika shimo hilo kwa siku tatu.

“Tulikojipenyeza kusimama ilitulazimu kusogea pembeni kidogo tu na kujisaidia haja kubwa, huku harufu yote ikiturudia, wakati maji ya kunywa yalikuwa hapohapo pembeni, niliona ndiyo mwisho wa maisha yangu, nilichofanya ni kumuomba Mungu tu anisaidie,’’ amesema Lucas.

Lucas amesema baada ya kupata karatasi yenye ujumbe unaouliza kama wako salama na kupata maji, waliona tumaini jipya na kuamini kuwa watatoka salama hata kama wangekaa kwa siku nyingi zaidi.

Tukio jingine la kihistoria lililotokea wilayani Geita mwaka 2015, baada ya wachimbaji watatu kukaa ardhini kwa zaidi ya siku tano kabla ya kuokolewa wakiwa hai eneo la Kukuruma linalomilikiwa na Mgodi wa Geita (GGM), tukio jingine kama hilo lilitokea wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, ambako wachimbaji walikaa ardhini kwa zaidi ya siku arobaini kabla ya kuokolewa wakiwa hai.

Kwa mujibu wa taarifa za mgodi huo, waliofukiwa wametambuliwa kwa majina ya Ezekiel Bujiku (20), Yohana Shigangama (34) na Aniset Masanja (32).

Wengine ni Dikson Moris (25) Mussa Cosmas (28), Raphael Nzubi (26), Amani Sylvester, Sheku Butogwa (22), Hassan Idd (31), Augustino Robert (27), Magalula Kayanda (23), Sabato Philimon (30), Meng Juping (36) raia wa China na wengine wawili ambao majina yao hayakupatikana.

 

Utaratibu wa kuingia mgodini

Akizungumza kuhusu utaratibu wa kuingia mgodini kila siku, Lucas ameliambia JAMHURI kuwa huwa wanapeana zamu kila baada ya saa nane kwa malipo ya Sh 10,000.

“Huwa tunapeana zamu kila baada ya saa nane na tunapoingia na kutoka hulipwa Sh 10,000…huwa tunaingia kwa ngazi maalumu zilizopo mgodini, kilichosababisha tufukiwe ni uchakavu wa miti maalumu inayozuia usianguke (matimba) maana ilikuwa imeoza kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kubadilishwa,’’ amesema Lucas.

Chanzo cha kufukiwa na mgodi

Pamoja na kuwapo kwa Sheria ya Madini namba 14 ya mwaka 2010, uchunguzi wa JAMHURI umebaini chanzo kikubwa ni uzembe pamoja na kutozingatia kanuni za usalama migodini.

Uzembe huo ni pamoja na kutofunga miti mikubwa ya kuzuia kuporomoka kwa mgodi, kutumia vyuma (angle line) vyenye kuhimili uzito na kuzuia kuporomoka kwa mgodi huo.

Kutokana na ajali hiyo, inaonesha miti iliyotumika kuimarisha kuta (matimba) ilikuwa imeoza na hivyo kushindwa kuhimili kuta za shimo na kusababisha kuanguka.

Wakati kazi ya uokoaji ikiendelea, umbali wa zaidi ya mita 100, ambapo wananchi walikuwa wamekusanyika kushuhudia tukio la uokozi, walisikika wakilipuka kwa shangwe baada ya raia wa China, Meng Juping, ambaye pia ni msimamizi wa mgodi hii wakiimba kuokolewa akiwa hai.

 

Sera ya uanzishwaji vyama vya wachimbaji 

Mwaka 1983 Serikali ilitoa sera ya kuanzishwa kwa vyama vya wachimbaji madini wadogo katika mikoa yote inayojishughulisha na uchimbaji madini (Region Miners Assosiations)

Lengo la uundaji na uanzishwaji wa vyama hivyo lilikuwa kuwaunganisha wachimbaji wadogo mikoani, kujenga umoja na kuwa na sauti ya pamoja, kuwa kiungo kikuu kati ya wachimbaji na Serikali, kuishauri Serikali katika mambo muhimu yanayohusiana na uchimbaji madini nchini kwa faida ya Taifa.

Kutokana na uamuzi huo wa Serikali, Mkoa wa Geita ambao ulikuwa miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Mwanza, chama cha MWAREMA kiliundwa rasmi mwaka 1886, kabla ya Mkoa wa Geita kuwa mkoa mwaka 2011.

Baada ya Geita kuwa mkoa, wachimbaji wa mkoa huo waliunda chama cha GEREMA, Novemba 28, 2011, kutokana na agizo la Wizara ya Nishati na Madini kama sera inayoelekeza.

Mkoa wa Geita unazo leseni 850 kwa wachimbaji wadogo huku kati ya hizo, zinazomilikiwa na Watanzania ni 600, leseni hizo zinamilikiwa kwa utaratibu wa mmoja mmoja, ubia ama kwa vikundi (Saccos) za uchimbaji.

Taarifa ambazo JAMHURI limezipata zinasema wachimbaji wadogo wanachangia wastani wa uzalishaji wa kilogramu 10-15 ya dhahabu kwa mwezi, na vile vile hutegemea na uchimbaji, usagaji na uchenjuaji wa miamba yenye madini hayo.

 

Naibu Waziri anena

Tukio hilo la uokoaji lilishuhudiwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, aliyeipongeza kazi kubwa iliyofanywa na wachimbaji wadogo kwa siku mbili, baada ya mitambo kushindwa kufika kwenye eneo la mwamba mgumu.

Amewaambia wachimbaji wadogo kwamba Serikali itahakikisha hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kutokana na shughuli za uchimbaji mdogo, lakini akawataka kufuata sheria na taratibu za uchimbaji.

Dk Kalemani alitumia fursa hiyo kuufunga mgodi huo kwa siku tano huku akimtaka Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, kufanya tathmini na kuchunguza usalama wa mgodi huo ili wachimbaji waendelee kufanya kazi kwenye mazingira salama zaidi.

“Eneo hili limefukuliwa sana, kamishna pitia eneo hili chunguza kila upande kujua usalama wake, hatuko tayari kuona Watanzania wakipoteza maisha,’’ amesema Dk. Kalemani.

Mbali na kutoa siku tano za uchunguzi pia aliagiza Kamishna wa Madini kumchukulia hatua mkaguzi wa madini aliyekuwa akikaguia mgodi huo kutokana na kasoro zilizoonesha kuwa eneo hilo halikukaguliwa.

Mhandisi Samaje amesema sheria ya madini inataka migodi ya dhahabu kukaguliwa kila baada ya miezi mitatu, na kwamba kutokana na maafa yaliyotaka kujitokeza atafanya ukaguzi ili kubaini uzembe umesababishwa na wakaguzi au wenye mgodi.

 Wakati huo huo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita kupitia Chadema, Upendo Peneza, ameshauri Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepsha ajali zisizokuwa za lazima.

Ameomba Serikali kuona namna ya kuwa na vifaa vya uokoaji katika Mkoa wa Geita, kutokana na kuwa na wachimbaji wadogo wadogo wengi ambao hawana uwezo wa kuwa na vifaa hivyo.

 

Kamati ya wokozi

Akizungumza na JAMHURI, Meneja wa mgodi wa dhahabu wa Busolwa ambaye alikuwa kwenye kamati ya uokoaji, Felix Adolf, amesema changamoto kubwa ni wakaguzi kutokagua ndani ya migodi na kuona mazingira ya wachimbaji wanayofanyia kazi.

“Ukaguzi wa kina unahitajika kwenye migodi, ni vema zikaundwa timu kwa kushirikiana na wachimbaji; wawatembelee wachimbaji wadogo waone kazi zao, hawa wanafanya kazi kwenye maeneo hatarishi na hawajui kama ni hatari kwao,’’ amesema Adolf.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga, amesema jitihada za kuwaokoa wachimbaji waliokuwa ardhini zilitokana na umoja uliokuwapo baina ya wachimbaji wa makampuni na wadogo bila kujali gharama, na kuwataka kuendelea kuwa na ushirikiano huo.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoani humo (GEREMA), Golden Hainga, wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita wanazo changamoto zinazowakabili, ambazo ni pamoja na uhaba wa mitaji ya uchimbaji madini.

Changamoto nyingine ni teknolojia duni ya uchimbaji madini, zana duni za uchimbaji na uchenjuaji Wachimbaji wameendelea kutumia zana na teknolojia duni, elimu duni ya uchimbaji madini, uhaba wa maeneo ya uchimbaji mdogo kwa wahitaji wapya.

Pamoja na changamoto hizo, wachimbaji wadogo mkoani Geita wamekuwa na utamaduni wa mahusiano mazuri na jamii wanaozunguka maeneo yao ya uchimbaji kwa muda mrefu.

Utamaduni huo umeufanya Mgodi wa Geita (GGM) na Bulyanhulu (Acacia) kutoa msaada wa hali na mali panapotokea matatizo yanayohitaji msaada wa haraka.  

 

Ramani yakwamisha uokoaji

Mhandisi wa Mgodi wa Busolwa, Ibrahimu Nayompa, amesema walichelewa kuwapata na kuwaokoa waliofukiwa kutokana na ramani za awali zilizotolewa na wamiliki wa mgodi huo kutokubainisha kwa usahihi eneo walilokuwa wachimbaji hao wakati wakifukiwa na kifusi.

Amesema uokoaji ulikuwa mgumu kutokana na kubahatisha eneo husika, hali iliyowalazimu wachimbaji wanaofanya kazi kwenye mgodi huo kuwasaidia kwa kuwachorea picha za ramani mpya kuwapa mwanga eneo gani wanapaswa kuwatafuta.

“Wamiliki wa mgodi walishindwa kutupatia ramani ya uhakika, tulikuwa tunabahatisha, lakini nanyi ni mashuhuda namna mashine ilivyokuwa inashindwa kulenga na kutoboa kwenye eneo la shimo walipokuwa ndugu zetu,’’ amesema Nayompa.

Msemaji wa Mgodi wa RZ Union, Francis Kiganga, amesema shimo lililofunikwa na udongo lina urefu wa mita 38 kwenda chini na pembeni kuna njia yenye urefu wa mita nyingine 38.

 

Hofu yatanda

Kwa upande wa ndugu wakiwamo wazazi wa vijana waliofukiwa na kifusi, mbali na kuishukuru Serikali kwa juhudi zilizokuwa zimefanywa tangu tukio lilipotokea, walimshukuru Mungu kwa kunusuru maisha ya wahanga hao.

“Mimi ni mzazi wa Amani Sylivester Oscar (25), nimekuja kushuhudia iwapo mwanangu yuko hai au amekufa baada ya kupewa taarifa hiyo, ni tukio lililoniumiza,’’ amesema Oscar Daud.

Naye John Costantine ambaye alipata taarifa za kufukiwa kwa mtoto wa kaka yake mkubwa, Tanga Cosmas, ilimlazimu kufika eneo la tukio ili kujua kinachoendelea.

 

Daktari azungumza 

Akizungumza na JAMHURI, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk. Joseph Kisala, amesema wachimbaji hao waliookolewa wanaweza kupata madhara ya kisaikolojia.

“Wanaweza kupata madhara ya kisaikolojia kwa sababu tukio hilo kwanza siyo la kawaida kumpata mwanadamu, unajua binadamu tunaishi kwa kutegemea hewa ya oksijeni,” amesema Kisala.

Akizungumza hali zao kiafya, Dk Kisala amesema walipopelekwa hospitalini hapo hawakuwa na hali mbaya isipokuwa njaa na ukosefu wa maji mwilini, hicho ndicho kilichosababisha kukosa nguvu.

 

Usalama kazini 

Meneja wa Wakala wa Afya na Usalama Kazini (OSHA) Kanda ya Ziwa, Mohamed Mjawa, amesema Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi ya mwaka 2003 inamtaka mwajiri kutoa mazingira yenye afya, usalama na ustawi kwa wafanyakazi wake.

“Hii sheria ipo wazi kabisa kwani ni lazima mmiliki kutoa na kuendeleza kifaa na mifumo na utaratibu wa kazi ambao ni salama na bila hatari kwa afya ya wafanyakazi. Mwajiri lazima ahakikishe usalama na kutokuwapo na hatari ya kiafya katika utumizi, shughuli, uwekaji na usafirishaji wa kikorokoro na mali. 

“Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi mwaka 2003 inahitaji waajiri kutoa kifaa cha kulinda (PPE) kwa wafanyakazi wanaohusika katika kazi hatari, lakini hata wewe ni shahidi pamoja na eneo lile kuwa na mawe hatarishi lakini wengi wao walikuwa wamevaa ndala ‘yeboyebo’, hali ambayo ni hatari kwa shughuli za migodi,’’ amesema Mjawa.

By Jamhuri