Na Alex kazenga.

Wiki iliyopita mitandao yakijamii ilitawaliwa na video fupi ikimuonyesha  mtoto mdogo mwenye umri kati ya miaka 5 akielezea jinsi alivyo toa taarifa kituo  cha polisi na kufanikiwa kumzuia baba yake kuuza shamba la familia.

Video hiyo  fupi iliyorekodiwa kwa kutumia  simu iliwavutia watu wengi, huku wengi wakistaajabu uwezo wa mtoto huyo kufanya maamuzi ya kiutu uzima ya kumshitaki baba yake mzazi na kumzuia asiuze shamba.

Tukio hilo ambalo limetokea wilayani Ngara  katika kijiji cha Kabanga, ni ushahidi wa kilio cha mashirika kama UNICEF na taasisi nyingine za kiraia na zile zisizo za kiraia ambazo zimekuwa zikipigania haki za watoto.

Hili ni tukio la aina yake hasa ikizingatiwa kuwa ni marachache sana kuweza kutokea hasa katika jamii nyingi za kiafrika ikizingatiwa kuwa ni mara chache kwa mtoto kama huyo kuwa na mawazo kama hayo.

Hii ni kwa sababu katika jamii  za kiafrika watoto wanakabiliwa na changamoto ya kutokusikilizwa na mara nyingi mawazo yao hujikuta yakidharauliwa kwa sababu ya umri wao.

Tabia hii  ya kutokuwa na utamaduni wa kutowasikiliza watoto, na kufanya maamuzi ambayo hawajahusishwa kwa njia moja ama nyingine huenda kikawa chanzo cha watoto wengi kuranda randa mitaani katika miji mingi nchini.

Kwa mfano kwa kutumia tukio la mtoto huyu aliyethubutu kumshitaki baba yake polisi  tunaweza kujiuliza, ni watoto wangapi wako mitaani kisa wamekosa pa kuishi baada ya wazazi wao kufanya maamuzi yenye athari kwa familia.

Mpaka kufikia hatua hii kuna uwezekano mtoto huyu amekomazwa pengine na changamoto ambazo amekuwa akizipitia kila siku katika maisha yake ya kila siku.

Alichokifanya mtoto huyu kingefanywa na mtoto kutoka nchi zilizoendelea kisinge shangaza watu wengi bali linge onekana ni tukio la kawaida lakini kwa kuwa limetokea katika jamii yetu linaonekana geni.

Umefika wakati kwa jamii kutambua kuwa umefika muda wa kupiga vita na  kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa ili waweze kuishi katika misingi iliyo bora.

Mfano mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wake, kudhulumiwa mali hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, utoaji mimba wa makusudi, kuonewa na vitu vingine vinavyoweza kumuathiri kiakili.

Aidha, lazima jamii ielewe kuwa watoto wanayo mahitaji ya msingi ambayo kote Duniani yanatengeneza ‘haki’ zao, kimsingi haki za mtoto huwa ni wajibu wa mtu mzima kutimiza mahitaji ya mtoto ili awe mwenye afya, apate elimu bora na ashiriki katika ujenzi wa nchi yake.

Pia ni lazima ifahamike kuwa mtu yeyote  hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, adhabu ya kikatili, kunyanyasika au afanyiwe matendo ya kumdumaza katika ukuaji wake.

 

By Jamhuri