Na Thompson Mpanji, Mbeya

Kutokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya Afya, miundo mbinu mibovu ya barabara na madaraja katika vijiji vingi vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani hapa baadhi ya wagonjwa wanaoishi mpakani wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kutibiwa Mkoa wa Njombe na Iringa.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti baadhi ya madiwani wa Kata za Mawindi, Ipwani na Igava wamewapongeza wananchi kwa kuwa na mwitikio wa kujitolea kujenga majengo ya zahanati kwa nguvu zao, lakini wameelezea changamoto ya kutotekelezwa kwa sera ya Serikali ya kumalizia hatua ya upauaji na kuwapelekea wahudumu wa afya.

Diwani wa Kata ya Mawindi, Mtaila Mhando amevitaja vijiji viwili kati ya vitano ambavyo havina zahanati kuwa ni Manienga na Mkandami, ambapo amedai kuwa mwaka 2010 wananchi wamechangishana fedha na kupauwa bati, lakini hawajawahi kupata fedha kutoka halmashauri.

Amezungumzia changamoto iliyopo katika vijiji hivyo kuwa vimezungukwa na mito miwili hali inayoweka ugumu kuvuka mvua inaponyesha na kujaza mito kutokana na kuhofia kupoteza maisha.

“Ndugu Mwandishi Kijiji cha Mkandami kimezungukwa na mito miwili ambayo ni Mto Alali unaotoka Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe na Mto Kiyoga kutoka ukanda wa Mafinga, mkoani Iringa na kipindi cha mvua unajaa hadi mwezi Aprili ambapo madereva wa boda boda wanageuka kuwa wakunga wakikuta maji yamejaa na kushindwa kuvuka na akina mama wajawazito wanapopata uchungu kwa kweli inasikitisha,” amesema kwa masikitiko Diwani huyo.

“Zahanati ya Kijiji cha Mkandami ujenzi umekamilika, kuanzia kiti, kuta, milango, lipu ndani na nje, choo na bafu na nyumba ya mkunga ipo na tungeomba kupatiwa Mkunga walau wa dharula kunusuru maisha ya akina mama wajawazito na watoto wasio na hatia wanaozaliwa kando ya mito. Zahanati ya Kijiji cha Manienga licha ya kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua mwaka 2014, wananchi walijotolea kuezeka bati na kazi iliyobakia ni kupiga lipu, tunaomba Halmashauri itusaidie kumalizia hatua iliyobakia.”

Diwani wa Kata ya Igava, Udes Seleman amesema Kata yake ina vijiji vitano ikiwemo cha Iwalanje ambapo wananchi wamejenga zahanati hadi hatua ya rinta, Kijiji cha Ikanutwa wanamalizia ujenzi kufikia hatua ya rinta, Kijiji cha Vikae bado hawajaanza ujenzi. Kijiji cha Igunda wameshaanza ujenzi ambapo Kijiji cha Igava wameshakamilisha ujenzi na kuanza kupata huduma ya afya.

Akizungumza na JAMHURI, Diwani wa Kata ya Ipwani, Marcus Kalinga amewapongeza wananchi kwa mwamko wa kujitolea na kuiomba Serikali kukamilisha majengo ya zahanati kama sera ya Afya inavyotaka wananchi wasipate usumbufu na hata kuwanusuru kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya afya.

“Zahanati ya luango imefikia rinta na serikali imalizie. Kijiji cha Elimseni na Kibelege wamepewa mifuko ya saruji 75. Ninaomba waanze ujenzi, kwa sasa wananchi wa Ipwani wanaenda kutibiwa Ilembula na Makambaku katika Mkoa wa Njombe, na Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kutokana na changamoto ya barabara mbovu na wengine wanakwenda kutibiwa Mbeya. Serikali itusaidie kukamilisha kituo cha afya,” amesisitiza Diwani Kalinga ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa Diwani amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Matemela na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbalizi katika Kata hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi amekanusha wananchi wa Kata ya Mawindi kuzalishwa na waendesha Bodaboda na kwamba Kata hiyo inacho Kituo cha afya.

“Tunayo Ambulance ya kuweza kuwafikisha wajawazito katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Rujewa endapo wanashindwa kuzalishwa kutokana na shida mbalimbali za uzazi na katika kituo hicho kuna waganga wa kutosha na wanazo zahanati mbili na wahudumu wapo. Ni kweli kuna zahanati mbili wamezijenga kwa nguvu za wananchi, kama ni choo wamejenga basi ni hivi karibuni, tutaangalia umbali kutoka kituo cha afya ili tuweze kuwapelekea wahudumu,” amesema Mkurugenzi Msangi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla katika mikutano yake ya kazi na watendaji wa Halmashauri za Wilaya mkoani humo amekuwa akiwaagiza watendaji wa Halmashauri kujenga na kukamilisha zahanati katika vijiji na vituo vya Afya katika kila Kata hadi kufikia mwaka 2020 suala lililokubaliwa na wananchi.

Please follow and like us:
Pin Share