Wiki jana, nimetembelea ofisi moja ya kiongozi ambaye anasemekana anaingilia kazi za watu. Lengo langu lilikuwa ni kuonana naye tena nikiwa na hasira sana kuwasilisha malalamiko yangu ya uzembe wa viongozi wengine katika maeneo yao. Kilichonikuta kule ni huruma ya watu wengine ambao wamefika hapo kwa sababu ya kushindwa kusaidiwa na viongozi wengine.

 

Imeniudhi sana kwa kuwa najua wajibu wa watendaji na viongozi mbalimbali kama waajiriwa wetu katika kutatua na kumaliza matatizo yanayotukabili badala ya kwenda kuomba msaada kwa viongozi wengine. Huu ni waraka ambao nimeamua kuandika mara ya pili baada ya kuona kama ninawapigia mbuzi gitaa.

 

Mimi ni mwananchi wa kawaida. Wapo watumishi wengi ambao wanalipwa mishahara yao kutokana na kodi zangu ninazolipa kwa kila jambo ambalo linaniingizia kipato au ninalitumia. Ninalipia jengo na shamba na fedha hizo zinakusanywa kuwalipa hao waitwao watumishi wa umma.

 

Ninapogundua na kwa uelewa wangu kwamba huduma ninayopaswa kuipata kutokana na kulipa kodi zangu sitahiki, siipati ninakerwa sana. Lakini ninakerwa zaidi ninapogundua kwamba wapo viongozi wachache wanaoliona hilo kama ni uhalifu na kuamua kuchukua hatua na wakaonekana wanajipendekeza kwa kufanya kazi za watu wengine.

 

Awali nilikuwa naaminishwa hivyo kama binadamu, lakini nilipobaini kwa jicho langu kuwa si kweli ilinikera sana. Wapo tuliowapa dhamana ya kutupimia maeneo ya ujenzi na serikali kwa kupitia kodi zetu. Serikali ilinunua vifaa vya kazi hiyo, lakini wao wakaamua kukaa ofisini na kupiga soga. Matokeo yake ni kuongeza migogoro ya ardhi kiasi cha kushindwa kujua hata mahali pa kuanzia. Wanasubili kusukumwa kutoka ofisini na kwenda katika makazi ya wananchi kuwapimia maeneo yao tena wakijua kuwa tunalipa.

 

Wapo madakatari ambao walisomeshwa kwa kodi zetu, lakini nao kwa uamuzi wao wa kuamua kufanya kazi watakavyo imefikia mahali unamwona mtu akipoteza maisha kwa sababu tu ya kukosa huduma ya matibabu au ushauri. Tumegeuza fedha ni utu na siyo kuwa muungwana na mzalendo.

 

Nakubaliana na mishahara midogo ambayo wanalipwa hao watumishi wa umma. Nakubaliana na mazingira magumu ya kazi ambayo wanakabiliwa nayo hao watumishi wa umma, lakini nilidhani jitihada za kuomba waongezewe mishahara zingetoka kwa wananchi ambao wanaona jinsi ambavyo wanateseka na kujituma kwao kwa jamii wanayoitumikia.

 

Leo nimeandika barua hii nikithibitisha wazi kwamba kuna ombwe kubwa la utumishi katika Serikali yetu. Wapo watu hawajui wajibu wao, wanasubili kuambiwa wafanye nini, hivi ni kweli hata suala la usalama wa shule ni lazima aambiwe waziri au mkuu wa mkoa?

 

Mdhibiti Elimu wajibu wake ni upi au hana mamlaka ya kufanyia kazi jambo lililo ndani ya mamlaka yake? Au lazima awe naye sehemu ya walalamikaji?

 

Najaribu kujiuliza tu ni kweli kwamba dhuluma za mishahara ni lazima zishughulikiwe na waziri au mkuu wa mkoa kama siyo watu wa ajira na Mahakama?

 

Kwanini wananchi wakate tamaa na viongozi wa ngazi za kati na kuamua kwenda mbele ambako majukumu ni mengi na ya kitaifa zaidi? Nadhani kuna mahali tunakosea katika uongozi lazima tufanyie kazi.

 

Kuna wajibu wa kila mtu kama kiongozi au mtendaji mahali pake na kama hawezi kutatua migogoro na kero za wahusika ni bora akajiuzulu na kuachia ngazi. Haiwezekani awepo kiongozi ambaye naye ni sehemu ya kulalamika. Tufike mahali tuseme inatosha na tupunguze siasa tufanye kazi. Yale mambo ya kubebana kijinga yaishe.

 

Mimi napambana sana na hali yangu. Ninawaona baadhi ya viongozi kama wananidhulumu kodi yangu kwa kutotatua kero zinazonikabili. Nakubaliana na baadhi ya viongozi ambao wanaona ni bora kuyafanya yale ambayo wenzao wameamua kuyaacha au kufanya siasa katika kuyatatua. Fanyeni kazi hata kama mtapata maneno ya kijinga kwamba mnajipendekeza.

 

Wote wanaosema hivyo ni wale ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao, na ni wale wanaopenda vyeo kwa unafiki bila kufanya kazi. Kwangu mimi Mheshimiwa Rais, hili ni ombwe zaidi ya ombwe. Kama kuna mtu ananisikia, ajue kuwa tunatakiwa kulifanyia kazi.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo

 

By Jamhuri