Mbunge-wa-Jimbo-la-Mvomero-Amos-Makala-akifafanua-jambo-kwa-wananchi-hawapo-pichani.Wakati mauaji na uhasama kati ya wakulima na wafugaji yakishika kasi katika wilaya za Kilosa na Mvomero, Morogoro, wananchi wamewalalamikia wabunge wa mkoa huo kuwa wanahusika mgogoro huo, JAMHURI limeweza kuripoti.
 Taarifa ambazo gazeti hili imezipata zinasema kwamba wananchi hao sasa wamekatishwa tamaa na mapigano yasiyokoma baina yao huku, yakiwanufaisha watu wachache wanaotoka nje ya wilaya hizo.


 Wanasema baadhi ya viongozi wa Serikali waliogawana ardhi iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa wananchi wa waishio katika vijiji hivyo, wamekuwa na vitendo vya kuchochea migogoro ili kujenga chuki kati ya jamii za wafugaji na wakulima.
 Kwa nyakati tofauti wananchi waishio katika vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya wakulima na wafugaji katika wilaya hizo, wanawataja wabunge wanaodaiwa kuchochea migogoro na kupandikiza chuki baina ya jamii za wafugaji na wakulima kuwa ni Amos Makalla (Mvomero), Ahmed Shabiby (Gairo) na Abdul-Aziz Abood ambao wanatajwa kuhujumu vijiji kwa upande wa vijiji vya Hembeti, Dihombo na Kambala vilivyopo katika Wilaya ya Mvomero.


Wananchi hao wameieleza JAMHURI kuwa wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwaleta watu kutoka Morogoro Mjini na nje ya mkoa huo kwa mabasi na kuwapeleka kwenye maeneo ya vijiji hivyo na kuwapa maeneo ya kulima bila kufuata utaratibu uliowekwa na vijiji husika.
Kwa upande wake, Ibrahimu Rijua anasema miaka iliyopita kabla na baada ya Operesheni Vijiji vya Ujamaa ya mwaka 1972 waliishi katika kijiji hicho cha Kambala bila kuwa na mgogoro na mtu yeyote, wakiheshimiana na kuthaminiana kama wananchi wa Tanzania, tofauti na sasa ambapo viongozi wa kisiasa wamegeuka kuwa wachochezi na wavuruga amani nchini.


 “Nilizaliwa katika kijiji hiki cha Kambala mwaka 1957 na hii ilikuwa kabla ya Operesheni Vijiji na mwaka 1958 ambako kilifanyika kikao cha kwanza kilichowajumuisha wahusika na kumchagua Lekake Machanja kuwa mjumbe,” anasema Rijua.
Anasema kabla hata ya nchi kupata uhuru, kijiji cha Kambala kilikuwako, na mwaka 1968 Serikali ilianzisha miradi ya maji na kujenga majosho kwa ajili ya mifugo wakati huo Mvomero ikiwa tarafa na Hembeti ikiwa kata.


“Hapa tumechanganyikana na Wapare, Wasukuma, Wahaya, Wabena, Waluguru na Wakaguru wakijihusisha na ufugaji na kilimo, na kabila kuu ni Wamaasai ambao ni wafugaji kwa asilimia 75, lakini kwa miaka yote hatupigani wala hatuna sababu ya kufanya hivyo,” anasema.
Rijua anasema shule ya msingi ya Kambala na zahanati ya kijiji hicho zilijengwa mwaka 1977 sambamba na ujenzi wa masijala tofauti na vijiji vingine.


  Hata hivyo anasema Mei 11, 1984 kilifanyika kikao cha pamoja cha viongozi wa vijiji vya Kambala, Hembeti, Dihombo na Mkindo kuhusu mipaka ya kijiji cha Kambala na vijiji vinavyopakana na kijiji hicho.
Anasema mwaka 1985 kilipimwa na kusajiliwa kisheria, ambako Desemba 10, 1986 Idara ya Upimaji na Ramani ilitoa hati ya kukubali mawe ya mipaka ya kijiji cha Kambala na Julai 30, 1990, Serikali ilitoa hati ya kumiliki ardhi ya eneo la kijiji. Pamoja na hayo anaeleza kwamba Agosti 27, 1993 kijiji cha Kambala kilikabidhiwa na Serikali hati ya kuandikishwa ikiwa na namba MG/KIJ/473


Naye Papayai Rijua, kiongozi wa kimila wa Wamaasai anasema mgogoro wa ardhi na mapigano yasiyokoma yalianza Novemba 23, 2012 baada ya baadhi ya wakulima kulalamika kuwa ng’ombe wameharibu mazao yao.  
 Anasema ng’ombe walikuwa kwenye eneo la kunyweshea mifugo yao katika Bonde la Mgongola ambako pia kuna eneo la kilimo na siku hiyo ndipo kundi la sungusungu maarufu kama ‘mwano’ lilivamia mifugo yetu na kufyeka kwa mapanga ng’ombe 12 na kupora 52.
  “Madai ya kundi hilo la kihalifu ambalo limeundwa na baadhi ya wavamizi wa ardhi ya kijiji cha Kambala wanaotoka katika vijiji vya jirani na Manispaa ya Morogoro, ni kuendesha jitihada za kuwaondoa wafugaji wa jamii ya Kimaasai katika eneo hilo ambalo wameishi kwa kipindi kirefu hata kabla ya uhuru,” anasema.


  Anasema kikundi hicho kimepewa nguvu na viongozi wa mkoa na wilaya waliokuwapo kabla ya mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni, kikipongezwa kwa kufanya mauaji na uporaji wa mifugo katika kijiji hicho na vijiji vingine vinavyokaliwa na wafugaji mkoani humo.
  Kiongozi huyo wa kimila wa Kimaasai ameieleza JAMHURI kuwa baada ya kukithiri kwa matukio ya uvunjifu wa amani unaosababishwa na wakulima kutoka nje ya kijiji hicho, Manispaa ya Morogoro na nje ya mkoa huo huku watu wakiuawa, kuporwa mifugo yao na uharibifu wa mali za wananchi, uongozi wa kijiji umeweka utaratibu wa kulima katika bonde hilo lakini haufuatwi.


  Anasema wavamizi wamekuwa wakiletwa na mabasi ya kampuni ya Abood na malori katika bonde hilo bila kuihusisha serikali ya kijiji na kwamba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Fatuma Mwasa, aliwahi kuongoza msafara wa wakulima kutoka Morogoro Mjini na kusababisha machafuko makubwa.
“Baada ya kuona amesababisha machafuko, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo kipindi hicho, Issa Machibya, aliwataka wakulima waliovamia bonde hilo kufuata utaratibu uliowekwa kwa kutambua kuwa hicho ni kijiji halali kama vingine,” anasema.
 Hata hivyo, anasema kukithiri kwa migogoro ya wakulima na wafugaji kunachangiwa na baadhi ya watawala kutozingatia misingi ya utawala bora huku wakijinufaisha na migogoro hiyo.


 Anasema uadui unaoenezwa na watawala dhidi ya wananchi wanaowaongoza umeanza kutowesha amani nchini na hivi sasa umeanza katika jamii za wakulima na wafugaji, na huu ni ubaguzi ambao ulipigwa vita tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza, lakini umeshika kasi kipindi hiki ambacho kila kiongozi anafanya lolote analolitaka.
 
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kambala
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kambala, Kashu Moreto, anasema mgogoro huo kati ya wakulima na wafugaji umesababishwa na wanasiasa ambao baadhi yao ni miongoni mwa watu walioingia katika bonde hilo na kulima bila utaratibu.
Anasema viongozi wa Serikali wameshindwa kabisa kutamka wazi kwamba Kambala ni kijiji halali kinachojiendesha kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazojulikana kitaifa na kueleza kwamba kimepimwa kama vilivyopimwa vijiji vingine nchini.


“Februari 22, 2013 Serikali ilitoa cheti cha kijiji cha Kambala ambacho kinatumika badala ya hati ya zamani kama utambulisho wake kisheria, lakini pamoja na vielelezo vyote hivyo kimegeuka kuwa kambi ya mapigano yanayopoteza maisha ya watu na mali zao,” anasema mwenyekiti huyo.
Anasema hakukuwa na ulazima wowote wa kutokea kwa migogoro hii isiyokwisha kama kungekuwa na utaratibu wa kuheshimu sheria zilizowekwa kwa ajili ya kuendesha vijiji.
 
Mwenyekiti wa zamani
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Diwani wa Kata ya Kambala, Majuka Koira, ameieleza JAMHURI kuwa kundi lililopigwa marufuku la ‘mwano’ kutoka Gailo limeendeleza kufanya matukio ya uvunjifu wa amani katika kijiji hicho huku likiungwa mkono na baadhi ya viongozi akiwamo Mbunge Amos Makalla.


Koira anasema kundi hilo la sungusungu ama mwano limekuwa likipatiwa mafunzo ya kurusha mishale, kupakwa majivu usoni na ushirikina, na mkufunzi anayefahamika kwa jina la Pasha Pasha ambaye alikiri katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, limekuwa likihusika na uporaji wa mifugo, uchomaji wa nyumba na kuua watu, hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya kundi hilo.


 “Kinachotushangaza ni kupongezwa kwa kikundi hicho cha kihalifu na viongozi kwamba kinafanya kazi nzuri kuliko hata Jeshi la Polisi, kutokana na wizi wa mifugo ambayo huishia kugawana na wakati mwingine kuiuza katika minada na mapato kugawana, huu ni uhuni uliovuka mipaka,” anasema.
 “Katika tukio la mwisho, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Leonard Paul, alikuja usiku kutembelea eneo la mapigano na Mei 13, mwaka huu kulikuwa na taarifa za kundi hilo la mwano kuvamia kijiji huku wakipiga filimbi na kusababisha wakazi wa kijiji hicho kukimbia hovyo, na polisi walipojulishwa hawakumkamata mtu yeyote,” anaeleza.


 Anasema awali akiwa makamu mwenyekiti wa halmashauri alianzisha vikao vya ujirani mwema kwa vijiji vyote vinavyopakana na Kambala, na hakukuwa na matukio ya migogoro na vurugu kama zinazoendelea sasa huku watu wakipoteza maisha na mali zao.  
  “Ndugu mwandishi, kipindi chote tuliishi kwa amani na utulivu, na suala la amani ilikuwa ajenda ya kudumu. Haya yanayoendelea sasa yamesababishwa na wanasiasa wanaokusudia kuharibu amani hii,” anasema.
 
Askofu atoa ya moyoni
Askofu Jacob ole Mameo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, ambaye mzaliwa wa Kijiji cha Kambala akiwa miongoni mwa wafugaji walioathirika na  migogoro inayoendelea kati yao na wakulima, anasema wanasiasa wanaondekeza ukabila mkoani humo ndiyo chanzo cha matukio hayo yasiyokubalika.


  Askofu Mameo ambaye ametajwa na baadhi ya wananchi kwamba naye ni miongoni mwa wanaochochea mgogoro huo ambao umesababisha vifo vya watu, mifugo na uharibifu wa mali za wakazi wa kijiji hicho na uharibifu wa mazao katika Bonde la Mgongola amekanusha madai hayo na kusema hizo ni porojo za kisiasa.


  Anasema viongozi waliokosa utashi wa kisiasa na kusaidia kutatua matatizo ya wananchi, wameelekeza vitendo vyao viovu kulichafua kanisa hasa linapokaribia kufanya uchaguzi mwezi wa Juni mwaka huu.
“Mimi ni mzaliwa wa kijiji cha Kambala, elimu yangu ya msingi nimeipata katika Shule ya Msingi Kambala ambayo iko hadi leo hii na baba yangu mzazi aliuawa na wakulima mwaka 1991 eneo la Mkindo hapo hapo kijijini,” anasema.
Anasema kama kiongozi wa kiroho hawezi kufurahia watu wakiuana kwa sababu ya chuki zinazopandikizwa na baadhi ya watu kwa manufaa yao wenyewe, hivyo ameshirikiana na Serikali mara kwa mara kutatua migogoro hiyo ya wafugaji na wakulima.


  Akitoa mfano jinsi anavyoshirikiana na Serikali kuhakikisha watu wanaishi katika maeneo hayo kwa amani na utulivu, anasema Septemba 13, 2013 alimpigia simu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, na pia kukutana naye ana kwa ana na kumweleza kwamba wenzao wameunda kundi hatari la mwano lakini hakumsikiliza.
  Hata hivyo, pamoja na kutosikilizwa na Mtaka, alionana na Joel Bendera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo ofisini kwake akamweleza uwepo wa kikundi hicho kilichoundwa kwa ajili ya kuteketeza jamii ya kifugaji mchana kweupe, wakisaidiwa na viongozi wa tarafa na diwani, pia hakusikilizwa.
  “Baada ya viongozi hao wote niliowaeleza suala hilo kwa nyakati tofauti na wote wakanipuuza, Septemba 15, 2013 yakatokea mapigano na watu wakauana bila sababu akiwamo kiongozi wa kundi hilo aliyeuawa ndani ya ardhi ya kijiji chetu na kama wangenisikiliza jambo hili lingedhibitiwa mapema,” anasema.


 “Novemba 6 na 7, 2013 yakatokea mapigano mengine makubwa sana ambako wananchi kutoka Gailo waliungana na kikundi cha mwano na kufanya mapigano na jamii ya Wamaasai kwa kuwasaka kila eneo hadi walipokuja polisi kutoka makao makuu. Hii ni hatari mno,” anaongeza Askofu Mameo.
  Anasema tatizo ni baadhi ya wakulima kutoka Morogoro Mjini wanaoendesha shughuli za kilimo katika bonde hilo bila kuzingatia utaratibu uliowekwa na uongozi wa kijiji.


 Pamoja hayo, anasema tatizo kubwa sasa ni chuki za ukabila zinazoanza kuenezwa kwa kasi katika maeneo hapa nchini na viongozi wa kisiasa waliofilisika kwa hoja na kuwaeleza ukweli wa mambo wananchi.
 
Wananchi wa Dihombo
Nao wananchi wa kijiji cha Dihombo kinachopakana na Kambala wameieleza JAMHURI kwamba wanasikitishwa na kuendelea kwa matukio ya uvunjifu wa amani kunakoendelea katika vijiji hivyo na hayo ndiyo matokeo ya siasa chafu na uongozi mbovu wa nchi.
  Wanasema Serikali nzima inafahamu migogoro yote inayoendelea katika eneo hili akiwamo Rais Jakaya Kikwete, lakini kama hawasikii wala hawaoni na hili ni jambo la hatari sana katika nchi.


  Thobias Leonce (25), mkazi wa kijiji cha Dihombo, anasema kwa utaratibu uliokuwako awali hakukuwa machafuko yoyote kutokana na kutoruhusiwa kwa wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye bonde hilo kabla ya mazao kuvunwa.
  “Bonde hili limekuwa likitumika kwa kilimo cha mpunga toka mwaka 1962 kwa kuanzishwa na Mzindakaya likiwa na ukubwa wa zaidi ya hekta 40,000 likitegemewa na kata zote tatu,” anasema Leonce.


 Anasema viongozi wa kisiasa ndiyo wachochezi wakubwa mgogoro huo na hivi sasa imewekwa amri ya kusimamisha shughuli zote za kilimo katika bonde hilo kwa kushinikiza utaratibu uliowekwa na kijiji cha Kambala ufuatwe, nasi hatuna chakula wala hatuwezi kulipa mikopo tuliyokopa katika taasisi za fedha.
Naye Mwanaidi Rashidi (42), mkazi wa kijiji hicho, anasema kuvunjika kwa amani kati ya jamii za wafugaji na wakulima kumesababisha sasa kuishi kwa hofu na uadui huku mkazi wa kijiji kimoja hawezi kuingia kijiji kingine.
 “Hii Tanzania ya leo haieleweki kabisa na viongozi wote hakuna anayethubutu hata kuhoji suala hili, kwani mtu akienda Kambala tunajua ni lazima atauawa tu na wa huko akija kwetu hawezi kutoka salama, haya ni maisha gani tena!” anaeleza.


Anasema shule ya msingi iko Kambala na shule ya sekondari ya kata iko Dihombo kwa sababu ya kutokuaminiana na kuishi kwa mashaka wananchi wanakosa fursa ya kupata elimu.
  Hata hivyo, anasema wanaopaswa kulaumiwa ni viongozi wa Serikali na wanasiasa waliochochea migogoro hiyo kwa maslahi yao binafsi ikiwa ni pamoja na kujinufaisha na shughuli za kilimo na uporaji wa mifugo.
 
Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajab Rutengwe, ameieleza JAMHURI kwamba analishughulikia suala hilo kwa kuchunguza kiina cha mgogoro, kwani bado hajakaa kipindi kirefu tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.
  “Nilichojifunza kutokana na mgogoro huu uliodumu kwa kipindi cha miaka 30 sasa ni uanzishwaji wa maeneo ya utawala bila kuwashirikisha watawala na kanuni zipo za uanzishaji wa maeneo hayo zikisimamiwa na serikali za mitaa,” anasema mkuu wa mkoa.


  Anasema uanzishwaji wa maeneo ya utawala ni lazima ushirikishe vikao vya Baraza la Madiwani, sasa kama taratibu hizo hazikufuatwa na hati zimetolewa, hapo kuna tatizo.
 “Haiwezekani kijiji kikaanzishwa ndani ya kijiji mama na kutangulia kupewa hati wakati huku kijiji cha kilichotambulika awali hakina hati hiyo, haya ni mambo ya kushangaza na ndiyo chanzo cha migogoro hii,” anasema.
 
Kijiji cha Mabwegere
Kijiji cha Mabwegere wilayani Kilosa ambacho kiliandikishwa Januari 4, 1990 na kupewa hati ya kumiliki ardhi namba 36042, nacho kwa muda mrefu kinakabiliwa na mgogoro wa wakulima na wafugaji.
  Hata hivyo, Juni 16, 1999 Serikali ilitoa hati ya kuandikishwa kwa kijiji hicho yenye namba MG/KIJ.522 iliyotolewa na H. Gonde, aliyekuwa Msajili wa Vijiji, kwa mujibu wa kifungu namba 22 cha Sheria za Serikali za Mitaa chini ya sheria namba 7 ya 1982.


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mika Kashu,  wamekuwa na mgogoro na wakulima waliovamia eneo la kijiji na kuendesha shughuli za kilimo huku mawe ya mipaka ya eneo la kijiji yaking’olewa.  
 Katika kesi ya ardhi namba 23 ya 2006 iliyofunguliwa na Halmashauri ya Kijiji cha Mabwegere dhidi ya Hamisi Shabani Msambaa na wenzake 32, na kutolewa hukumu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kwamba mawe ya mipaka ya kijiji hicho yaliyong’olewa na wavamizi wa hao yarudishwe.
  Licha ya kutolewa kwa uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imekaidi kutekeleza amri hiyo halali ya Mahakama na kutafuta msuluhishi mwingine wa mgogoro huo, ambaye naye ameshindwa kufanya hivyo.
“Tunashindwa kuelewa kabisa kwa nini viongozi wanapingana na mhimili wa Mahakama na kuchochea zaidi migogoro ambayo imepatiwa ufumbuzi kisheria,” anasema Kashu.


Anasema haja ya kuwa na msuluhishi huku hakuna taarifa yoyote ya Serikali namna ilivyotekeleza hukumu ya Mahakama halafu ikashindwa, ni kutafuta namna ya kupindisha uamuzi huo.
 Pamoja na uongozi wa mkoa huo kushinikiza kumpendekeza Paul Kimitti kuwa msuluhishi wa mgogoro huo wa ardhi ya Kijiji cha Mabwegere na kukataa kutambua uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, hakuna kilichofanyika kwani alijitoa hata kabla ya kuanza jukumu hilo.
Anasema hawana nia ya kugombana na wananchi wenzao kutoka vijiji vya jirani, ambao ni jamii za wakulima na kinachoonekana wazi ni viongozi wa Serikali kutafuta namna ya kuanzisha machafuko yanayoendelea kuhatarisha amani ya nchi kwa maslahi yao.


Pia amekituhumu kikosi cha uhalifu cha mwano kinachoungwa mkono na viongozi mkoani humo wakiwamo baadhi ya wabunge, kwa kushambulia wakazi wa kijiji hicho, kupora mifugo na kuteketeza nyumba zao kwa moto huku Serikali ikishindwa kulidhibiti kundi hilo.
 
Kijiji cha Mfuru
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mfuru, Musa Maganga, ameieleza JAMHURI kwamba mgogoro huo ulianza mwaka 1990 baada ya Kijiji cha Mabwegere kupewa hatimiliki ya ardhi huku kikiwa ni miongoni mwa vitongoji vinne vya Mfuru.
  Maganga anasema Kijiji cha Mfuru kilianza mwaka 1975 na mwaka huo huo walipeleka maombi ya hati chini ya mpango wa vijiji vya ujamaa na serikali kukipatia hati namba MG 110 ya mwaka 1976, ikiwa na vitongoji vya Kambini, Galani, Kibidu na Mabwegere.


Anasema kipindi chote hicho kulikuwa na amani hadi mwaka 1990 Mabwegere walipojitenga kwa kupata hati ambayo hakukuwa na ushirikishwaji wowote wa kijiji mama.
 Anasema kwa asilimia 75, Mabwegere ilikuwa ni kitongoji cha wafugaji wa jamii ya Kimaasai na kwamba baada ya kujitangaza kuwa ni kijiji halali cha wafugaji, walimega ardhi ya vijiji vya Mfuru, Mbigiri, Msowero na Dumila na kutangaza hati yao Januari 4, 1990.
“Kwa kitendo hicho cha kutangaza hati yao wakati kijiji mama hakikujulishwa utaratibu wowote uliokuwa ukiendelea, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kipindi hicho, Kapteni Kasapila, aliamuru mawe hayo ya mipaka yang’olewe kwani walifanya jambo hilo bila utaratibu,” anasema.
  Anasema Hati ya Kijiji cha Mabwegere namba MG/522 iliyoibua mgogoro tunayo hadi sasa nakala yake halisi na wao kusalia na nakala kivuli tu, na mwaka 2006 walikwenda mahakamani kushtaki.


“Mwaka 2014 serikali kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa iliamuru mipaka hiyo ipimwe upya ili kumaliza mgogoro huo na kumtangaza Kimiti kuwa msuluhishi wa tatizo hili kati ya Aprili na Mei mwaka huu, lakini hakuna kilichofanyika hadi sasa,” anasema.
 Katika mapigano hayo, anasema wanavijiji 22 wamefariki, wengine ni walemavu, huku wengi wao wakikabiliwa na njaa, uharibifu wa mazingira na kuporomoka kwa shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa vijiji hivyo.
  Anasema tatizo hilo limechangiwa na Serikali kwa kiwango kikubwa, kwa kuamua mambo bila kuzingatia taratibu na sheria za nchi kama zinavyoagiza.
 
Wabunge
Wabunge Amos Makalla wa Jimbo la Mvomero, Ahmed Mabkhut Shabiby wa Jimbo la Gairo, na Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdul-Aziz Mohamed Abood, ambao wanatajwa kuwa ni vinara wa kueneza chuki zilizosababisha mapigano miongoni mwa jamii za wafugaji na wakulima mkoani humo, walipotafutwa na JAMHURI hawakuweza kupatikana.

4364 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!