Si siri kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini, mambo si shwari. Amani na utulivu wa nchi yetu vimetikisika. Nadiriki kusema hivi kwa sababu, tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliofanyika mwaka 1995, amani na utulivu vimekuwa vikiyumba kila kukicha.

Kuanzia uchaguzi wa mwaka 1995 tumeshuhudia wapinzani wakigomea matokeo na matukio ya fujo baada ya hapo. Mambo hayo yamefanya amani na utulivu wa Tanzania kuanza kuyumba. Viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vinavyoshindwa katika uchaguzi sasa hawana hofu tena kumwaga damu. Wanachochewa kufanya fujo, kutukana viongozi wa Serikali na hata kukaidi amri halali za mamlaka.


Tumeyashuhudia haya. Yalianzia Visiwani, pale viongozi wa Civic United Front (CUF), walipoyakataa matokeo na hatimaye kutomtambua Rais wa Zanzibar aliyeshinda wakati huo, Dk. Salmin Amour.


Yaliyotokea sote tunayafahamu. Shaka ikatanda hasa Pemba, ambako wananchi waligawanyika kiitikadi za kisiasa hata katika mambo ya kijamii.


Wakaacha kuzikana, wakasusiana sherehe za harusi na kadhalika. Hujuma za wazi wazi za huduma za jamii zikawa zinafanywa. Watu wasiojulikana wakadaiwa kuweka vinyesi vya binadamu kwenye visima, kwenye skuli na sehemu nyingine nyingi. Kwa ufupi amani na mshikamano vilitoweka.


Viongozi, wanachama na wafuasi wa CUF, wakajipachika jina la “ngangari”. Wakimaanisha wako imara na tayari kwa lolote. Zanzibar kukawa si mahali salama pa kuishi. Shughuli za kiuchumi zikayumba visiwani humo hali iliyosababisha Serikali kuchukua hatua.


Hatua iliyofikiwa ilikuwa ni ya kuanza mazungumzo kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CUF, maarufu kama “Mwafaka”. Mwafaka huu wa kwanza kutafuta suluhu kati ya CUF na CCM ulisimamiwa na Chifu Emeka Anyauko, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Hata hivyo, Mwafaka wa kwanza chini ya Anyauko, haukufanikiwa. “Ngangari” wakaendelea kupambana na Serikali wakati wote, hadi walipokuja kumtambua Dk. Salmin, kwa shingo upande.


Katika kipindi hicho, upande wa Tanzania Bara, chama kikubwa cha upinzani kilikuwa ni National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), chini ya Mwenyekiti wake Augustine Mrema, aliyekuwa Waziri katika Serikali ya CCM ya Awamu ya Pili chini ya Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, kabla ya kutimuliwa.


Aidha, yaliyokuwa yakitokea Zanzibar wakati huo kama nilivyoyaeleza, kwa upande wa Tanzania Bara, mambo yalikuwa shwari kiasi. Zilikuwapo ghasia ndogo ndogo zilizokuwa zikijifanywa na wafuasi wa CUF hasa kwenye mikutano yake ya Kidongo Chekundu, Temeke Mwisho na Zakhem Mbagala mkoani Dar es Salaam, Bagamoyo na Tanga.


Kwa upande wa chama kilichokuwa na wafuasi wengi jijini Dar es Salaam cha NCCR-Mageuzi, sina kumbukumbu ya wafuasi wake kufanya vurugu kwenye mikutano yao.


Baada ya Uchaguzi wa kwanza na yaliyotokea Zanzibar, “ngangari” wale wale, wakarejea yale yale ya mwaka 1995. Januari 2001, wakiwa hawaitambui Serikali ya Rais Abeid Aman Karume, wakafanya maandamano makubwa Pemba na Dar es Salaam.


Kwa kukaidi maelekezo ya vyombo vya dola, kutokana na vurugu zilizoambatana na maandamano hayo, polisi iliwabidi watumie nguvu ya ziada kuwadhibiti na kujilinda na hatimaye watu zaidi ya 20 walifariki dunia na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya. Vifo hivi vilitokea Pemba ambako ni ngome kuu ya CUF hadi sasa.


Kutokana na kutomtambua Rais Karume, na kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, wabunge 16 walifukuzwa. Kwa busara ile ile ya mwaka 1995, safari hii bila kumtumia msuluhishi kutoka nje, yalianzishwa mazungumzo mengine kati ya CCM na CUF. Ukaanzishwa Mwafaka II, mazungumzo ambayo hatimaye yalifanikisha kutiwa saini Oktoba 2003.


Katika Mwafaka II yalikuwapo mambo ambayo CCM na CUF walikubaliana yafanyike. Mambo hayo ni pamoja na kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar, kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na kufanyika kwa uchunguzi wa mauaji yaliyokea Januari, 2001. Haya yote yakafanyika.


Katika hatua nyingine, iliyoashiria mambo kuwa shwari Zanzibar, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akamteua Hamad Rashid Mohamed kuwa Mbunge, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hamad Rashid Mohamed alitokea CUF.


Ukaja Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambao ulikuwa ni wa kumchagua Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano na wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, Rais Mkapa alikuwa amemaliza muda wake hivyo, Jakaya Kikwete aliyekuwa mgombea wa CCM, akachaguliwa kuwa Rais akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.


Hali ya kugomea matokeo ikawa kama ilivyokuwa mwaka 1995 na mwaka 2000 kwa upande wa Zanzibar. Hata hivyo, safari hii hakukuwa na vurugu kama zile za katika uchaguzi ulizopita.


Kama nilivyosema hapo juu, miongoni mwa mambo mengine yaliyokubaliwa ni pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo sasa na pia kwa kuzingatia historia.

 

Katika suala hili, ilibidi vikao vya juu vya CCM na CUF vijadili na kutoa uamuzi wa kukubali utaratibu huo ambao Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilikutana Butiama, Mara, na Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilikutana Dar es Salaam. Vyama vyote vilikubaliana na suala hili na kulitangaza.


Hata hivyo, ili kuhalalisha uamuzi huo, vyama vyote vilikubaliana kura ya maoni (referendum) ipigwe Zanzibar, ili kuwauliza wananchi kama wanaukubali utaratibu huo. Kwa bahati nzuri, wananchi wa Zanzibar walikubaliana nao.

 

Ukaja Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Tofauti na uchaguzi ulipita, huu ulikuja ukiwa tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) “magwanda” wakiwa wamejiandaa kwa kufanya operesheni inayojulikana kama “Operesheni Sangara”, iliyolenga zaidi mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Chadema walikuwa wamepania, wakijiaminisha kuwa Uchaguzi wa 2010 wanaingia Ikulu. Wakawaaminisha hivyo wafuasi wake, nao wakawa nalo hilo kwenye vichwa na mioyo yao. Katika namna ya matumaini hayo, Mwenyekiti wa Chadema aliyegombea urais mwaka 2005, hakugombea. Katika uchaguzi wa 2005 aliambulia kura 668,756 na wabunge watano, hakugombea.


Safari hii, wakiamini kuwa Katibu Mkuu wao, Dk. Wilbrod Slaa ana nguvu na mvuto kutokana na mafanikio ya Operesheni Sangara, wakamtwisha zigo la kupambana na Rais Kikwete. Lakini, Dk. Slaa akijua kuwa hawezi kushinda, na kwamba baada ya hapo atabakia tu kuwa Katibu Mkuu, bila ya kuwa Mbunge wa Karatu, akatoa masharti ya yeye kukubali kuwa mgombea urais. Masharti ambayo ni kwa ajili ya maslahi yake ya miaka mitano atakayokaa bila kuwa mbunge.


Katika masharti hayo, Dk. Slaa akakitaka chama chake kimlipe mshahara na marupurupu kama anayolipwa mbunge! Na masharti hayo yawekwe kwenye mkataba wa maandishi na usainiwe mbele ya wanasheria. Hivyo, Dk. Slaa alijua anazunguka kuomba kura ambazo hazitatosha, lakini kila mwisho wa mwezi ataweka mfukoni zaidi ya shilingi milioni saba.

 

Vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi vikiwa vinaonesha wazi vimechoka katika uchaguzi wa mwaka 2010, viliingia kwa matumaini kidogo sana hasa baada ya wagombea wake wa urais mwaka 2005, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Dk. Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi) kufanya vibaya.


Chadema, wakitumia chopa kuzunguka kuomba kura, vijana walioandaliwa katika maeneo waliyokuwa na matumaini nayo, hawakuonesha ustaarabu wa kisiasa wakati wote wa kampeni. Wagombea wake wa ubunge nao, badala ya kunadi sera, wakageuka watu wa mipasho, udhalilishaji, matusi na kejeli. Kazi kubwa ikawa ni kuwashambulia watu binafsi hasa wapinzani wao na hasa, wagombea wa CCM.


Katika Jimbo la Arusha Mjini, mgombea wa Chadema, Godbless Lema, akatumia muda mrefu kumshambulia kwa matusi, kejeli na kumdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, badala ya kunadi sera. Kwa sababu nilizozieleza hapo juu, vijana wengi na wafuasi wa Chadema wakaona hiyo ndiyo siasa!

ITAENDELEA

Mwandishi wa makala haya, Gabriel Athuman, ni kada na mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayekitumikia chama hicho Makao Makuu Dodoma. Anapatikana kwa simu na.

0657861666

1245 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!