Leo naitafuta wiki ya pili tangu nifike hapa Accra, Ghana. Naendelea na mafunzo juu ya mafuta, gesi na madini. Mafunzo haya yanalenga kuwapa utaalam watu mbalimbali; waandishi, makarani wa bunge, maafisa wa serikali, vyama vya kijamii, viongozi wa jadi na wengine wengi. Mafunzo haya yamelenga katika kutufundisha nchi zetu zinavyoweza kufaidika na wawekezaji wakafaidika.

Wanatupatia ujuzi jinsi ya kusoma na kuandika mikataba ya madini, mifumo ya kukokotoa mapato, iwapo taifa linapaswa kutumia mfumo wa kulipwa kodi au kugawana mapato na ni mfumo upi una faida. Kimsingi, baada ya kupata mafunzo haya, ambayo nitaandika kwa kina katika sekta ya gesi na madini hapo kwetu, naona tayari tumepigwa mchanga wa macho.

Sitanii, naamini Serikali iliyopo madarakani ipo kwa ajili ya watu na kutumikia watu, hivyo sina hata chembe ya shaka kuwa ushauri nitakaoutoa utachukuliwa na kufanyiwa kazi katika eneo hili kwa faida ya taifa letu sasa na vizazi vijavyo. Tusipokuwa na hizi mbinu, tutabaki na mashimo. Ghana wameanza, na jamii inaanza kuona matunda ya mfumo huu mpya wa kufuatilia mapato yatokana na madini na gesi. Hapa wana na mafuta pia.

Hata hivyo, leo sikusudii kuandika makala juu ya mafuta, gesi na madini. Makala hii nitaiandika siku nyingine. Kilichonisukuma kuandika makala ya leo, ni wimbi la sifa tunazopata Watanzania tulipo katika kozi hii kutokana na utendaji wa Rais John Pombe Magufuli. Tupo Watanzania sita. Hapo nyumbani kuna msemo kuwa “Baniani mbaya, ila kiatu chake dawa.”

Sitanii, mafunzo haya yanayoendelea wapo washiriki kutoka Uganda, Kenya, Rwanda, Zimbabwe, Zambia, Angola, Sierra Leon, Mauritania, Ghana, Nigeria na Tanzania. Hizi ni nchi 11. Tukienda mapumziko, washiriki wanatufuata Watanzania na kutuzunguka. Wanahoji Rais Magufuli amewezaje kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma?

Wageni hawa wapo mbali na Tanzania, lakini wanasema kupitia vyombo vya habari wanafuatilia na kuona Tanzania imempata Rais aliyestahili kuongoza bara lote la Afrika. Nimejaribu kuwauliza waniambie nini kimewafanya wampende Rais Magufuli na wametaja yafuatayo:-

Kubaini wafanyakazi hewa 16,000. Kutumbua hadharani watumishi wa umma wanaokula rushwa au kutumia vibaya madaraka. Kununua ndege mpya mbili. Ujenzi wa Barabara za Mwendo Kasi. Uunganishaji wa wizara na kupunguza idadi ya mawaziri. Kusimamia usafi miji ikawa safi. Kupunguza matumizi ya serikali. Kuzuia safari za nje kwa watumishi wa Serikali.

Orodha haiishii hapo tu. Wanataja pia ukusanyaji wa mapato. Matumizi ya risiti za elektroniki na kampeni yake ya “Ukinunua Dai Risiti.” Ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufanikisha upatikanaji wa vitanda na magodoro. Kufuta sherehe ya Bunge akasema fedha hizo zipelekwe kununua vitanda vya hospitali.

Madawati kwa wanafunzi. Elimu bure hadi kidato cha nne. Kutia saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard na kupata fedha za ujenzi huo kutoka China. Uongozi wa kutaka kuona matokeo ya kazi aliyofanya na si kusubiri ripoti. Udhibiti wa uvuvi haramu. Tena kuna taarifa hapa kuwa Magufuli amezuia michango ya harusi, suala wanalopongeza kuwa inasumbua katika nchi zao.

Sitanii, wengi wanaona ndoto ya Rais Magufuli kujenga viwanda nchini Tanzania kuwa itatimia, maana wanasema marais wa nchi zao maisha yao ni vikao visivyo na tija kwa mataifa yao. Kimsingi wanafikia hatua wanatuuliza iwapo kuna uwezekano wa kuwaazima Rais Magufuli akaendesha nchi zao kwa angalau mwezi mmoja, kisha akawarudishia.

Kubwa kuliko yote, wanampongeza kwa kusimamia sheria bila kujali anayeguswa ni mkubwa au raia wa kawaida. Wanapongeza hatua ya askari wa usalama barabarani kuwa na EFD risiti, na wanasifu kuwa Rais Magufuli amebana trafiki wa Tanzania hawali rushwa kama wa nchini kwao. Kimsingi safu hii ni fupi, ila Rais Magufuli amerejesha heshima ya Tanzania kimataifa.

Nchi za Afrika zinafuatilia vyombo vya habari vya Tanzania kuliko wakati wowote. Habari za Tanzania sasa wanasema nchini kwao zinachapishwa kwa nia ya kuwashawishi marais wa nchi zao waone jinsi Rais mwenzao (Magufuli) anavyofanya kazi. Kuna mmoja kutoka nchi jirani, ameniambia baada ya ujio wa Rais Magufuli madarakani, angalau na Rais wao sasa anajitutumua na kutoa amri kuthibitisha kuwa na yeye ni Rais. Waghana hapa, wanasema Serikali yao ilinunua mabasi kabla ya kuyajengea barabara maalum kama Tanzania ilivyofanya, sasa yanaishia kwenye foleni na hayana msaada wowote kwao!

Sitanii, kila waliponiuliza kasi ya maendeleo ikoje, mimi nimekuwa nikiwapa jibu moja tu. “Tuombee tuendelee na kasi iliyopo si muda mrefu tutaanza kuwapa misaada kama inavyowasaidia Marekani. Tanzania itawasaidia bila masimango, ila kwa sharti moja tu, kwamba muwe tayari kununua bidhaa za viwanda vyetu tunavyojenga.” Wengi wanasema watakuwa mabalozi wa kujitolea kwa nchi zao kununua bidhaa za Tanzania.

Naomba kuhitimisha makala hii kwa kusema kwamba, inawezekana Rais Magufuli kwetu hapo ndani baadhi ya watu hawafurahishwi na uamuzi wake katika baadhi ya masuala ya kisiasa, ila kiuhalisia ukirejea aliyofanya tangu ameingia madarakani na ukaangalia mataifa ya nje yanavyofuatilia utendaji wake, hakika unaona nchi yetu inaelekea katika kuuaga umaskini. Hongera Rais Magufuli, endelea kusimamia sheria. Nimeona nikufikishie sifa zako nilizokutana nazo hapa Accra.

2809 Total Views 3 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!