Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, alitoa ahadi nyingi mno.

Ahadi hizo zilikuwa mbali na zile zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho. Akiwa anaelekea kumaliza miaka miwili ya kipindi chake cha pili cha uongozi, utekelezaji ahadi hizo unaonekana kuwa kuwa kitendawili.


Utekelezaji ahadi hizo ulishatiliwa shaka tangu mwaka 2010. Baadhi ya wananchi, na hata wagombea wa vyama vingine walitilia shaka utekelezaji wa ahadi hizo kwa maelezo kwamba kukamilika kwake kulihitaji matrilioni ya shilingi.


JAMHURI imeona ni vema kumkumbusha Rais Kikwete na Chama Cha Mapinduzi juu ya ahadi hizo.


Ifuatayo ni orodha ya ahadi. Mbele ya kila ahadi kuna jina la mahali alipoitolea. Ikumbukwe kuwa ahadi hizi ni nje kabisa ya Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015.

1. Kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa – Nzega, Tabora.

2. Mkoa wa Tanga kuwa Jiji la Viwanda – Tanga mjini.

3. Tabora kutumia maji ya Ziwa Victoria – Igunga.

4. Kulipa madeni ya chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) – Shinyanga.

5. Kumaliza migogoro ya ardhi nchini – Dodoma.

6. Wakulima kuacha kutumia jembe la mkono – Dodoma mjini.

7. Kuwapatia trekta wakulima – Kata ya Mrijo, Dodoma.

8. Wananchi kutoondolewa kwenye Ranchi ya Misenyi – Kagera.

9. Kujenga Uwanja wa Ndege Misenyi – Kagera.

10. Kupanua Uwanja wa Ndege Bukoba – Bukoba Mjini.

11. Kujenga uwanja wa ndege mkubwa Kigoma – Kigoma Mjini.

12. Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda – Kagera.

13. Mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme – Kagera.

14. Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu – Kagera.

15. Hukumu kwa waliopatikana na hatia ya kuua albino – Mbeya.

16. Kununua meli kubwa kuliko mv Bukoba – Kagera.

17. Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali.

18. Serikali kuvisaidia vyama vya ushirika – Mwanza.

19. Kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalumu chenye vifaa kupambana na wahalifu – Mwanza.

20. Wilaya ya Geita kuwa hadhi ya mkoa Januari mwakani – Geita.

21. Kulinda Muungano kwa nguvu zote – Pemba.

22. Kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko Kilosa – Morogoro.

23. Kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa – Mbeya mjini.

24. Kujenga bandari Kasanga – Rukwa

25. Kumaliza tatizo la walimu miaka mitano ijayo – Songea.

26. Kufufua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira – Mbeya.

27. Kuzuia hatari ya Kisiwa cha Pangani kuzama – Tanga.

28. Kununua bajaji 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini – Iringa.

29. Kujenga barabara yenye kiwango cha lami kutoka Same hadi Kisiwani – Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam-Same mkoani Kilimanjaro.

30. Kumaliza tatizo la maji katika Wilaya ya Same – Same mjini.

31. Kuboresha barabara za Igunga-Tabora.

32. Kusambaza walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu – Kisesa Magu.

33. Kununua vyandarua viwili kwa kila kaya – Mbeya mjini.

34. Kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) – Hydom Manyara.

35. Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa – Musoma.

36. Kulinda haki za walemavu – Makete.

37. Kujenga baabara ya Njombe – Makete kwa kiwango cha lami, urefu wa kilomita 109 – Iringa mjini.

38. Kujenga barabara Musoma-Mto wa Mbu Arusha – Arusha.

39. Kuanzisha Jimbo la Ulyankulu- Shinyanga mjini.

40. Kujenga barabara ya lami Manyoni-Kigoma-Kaliua, Tabora

41. Kukarabati barabara ya Arusha-Moshi – Arusha mjini.

42. Kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa hadi Singida – Dodoma.

43. Kuwafidia wanakijiji ng’ombe waliopotea wakati wa ukame mwaka 2009 – Longido.

44. Vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria – Shinyanga-Kahama kuunganishiwa maji – Shinyanga.

45. Tatizo la umeme kufikia kikomo Novemba mwaka huu mkoani Arusha – Arusha mjini.

46. Kukopesha wavuvi zana za kilimo – Busekera, Wilaya ya Musoma.

47. Kuwapatia maji wakazi wa Wilaya ya Longido – Longido.

48. Kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Seregenti – Ngorongoro.

49. Utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo kuwasaidia wafugaji kuweza kupata na kutunza mifugo yao vizuri – Mbulu mkoani Manyara.

50. Kusambaza maji nchi nzima – Babati vijijini.

51. Kusambaza umeme, utoaji wa huduma za afya, na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji na utoaji ruzuku kwa wakulima mwaka 2010-2015 – Babati vijijini.

52. Kuongeza mara tatu idadi ya wananchi wanaonufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha – Iringa.

53. Kuhakikisha Isimani inapata maji ya uhakika – Iringa.

54. Kuiwekea lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania – Iringa.

55. Kulinda usalama wa wananchi kwa ujumla ili kudumisha amani na sifa ya nchi –Ifunda.

56. Kutokomeza malaria 2015 – Bunda, Mkoa wa Mara.

57. Kuwapa wanawake nafasi zaidi – Kilolo, Iringa.

58. Ahadi kuisaidia Zanzibar kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii – Kibandamaiti, Mjini Zanzibar.

59.Kuipandisha hadhi hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar kuwa ya rufaa – Kibandamaiti mjini Zanzibar

60. Kuisaidia Zanzibar kila panapohitajika msaada – Kibandamaiti.

61. Serikali kujenga upya Bandari ya Mbamba Bay – Ruvuma.

62. Ununuzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400 – Mbamba Bay, Ruvuma.

63. Kufufua chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Mbinga (MBICU) – Ruvuma.

64. Ahadi Rais wa Marekani Barack Obama kuimwagia misaada Tanzania – Ruvuma.

65. Ahadi hakutakuwa na umwagaji wa damu baada ya uchaguzi – Dar es Salaam.

66. Mtwara kuwa mji wa viwanda – Mtwara.

67.Ahadi ujenzi wa kwanda cha dawa ya kuua viluilui vya mbu – Kibaha.

68.Hospitali ya Tumbi kuwa ya mkoa – Kibaha.

69. Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kutenga eneo maalumu la viwanda – Kibaha.


By Jamhuri