Kama si mfuatiliaji wa mambo unaweza kuamini kuwa Wakenya wamekurupuka kuyazuia magari ya Watanzania kubeba abiria kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya.

Hawakukurupuka. Walichofanya ni kujaribu kumwamsha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Wanamwamsha ili atekeleze ahadi aliyowapa ya kuufungua mpaka wa Bologonja!

Tunachopambana nacho sasa ni matokeo ya ahadi za Nyalandu za kukurupuka na kutafuta sifa zenye mwelekeo wa kumjenga kisiasa na kiuchumi.

Ndio, ni Nyalandu huyu huyu ambaye Februari 20, mwaka jana alitoa ahadi ya ‘kufungua Bologonja’ kwenye kikao cha mawaziri wa utalii na wanyamapori kutoka mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda, kilichoitishwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.

Kwenye kikao hicho kulikuwa na hoja kadhaa, lakini ni hoja moja iliyotawala mjadala wote. Nayo ilikuwa ni ya kufunguliwa kwa Bologonja; ambayo ilifungwa na Rais Julius Kambarage Nyerere. Mjadala ukawa wa Tanzania na Kenya. Hoja za Wakenya zikawa kwamba, kama kuna ushirikiano wa kijumuiya, iweje Tanzania iendelee kuufunga mpaka huo? Hapa ikumbukwe kwamba ‘mpaka’ ulifungwa ili kuwawezesha Watanzania kufaidika na rasilimali kubwa ya vivutio vyao vya utalii.

Ni kwa sababu hiyo, tangu mwaka 1985 Tanzania na Kenya ziliweza kuainisha maeneo ya watalii kuingia na kutoka kwa kutumia usafiri wa nchi kavu. Ikakubalika sehemu hizo ziwe za Sirari/Isibania, Namanga/Namanga, Holili/Taveta na Horohoro/Lungalunga.

Hakuna ‘crossing border’ mahali panapoitwa Bologonja. Huo ni upenyo au ‘njia ya panya’. Haitambuliki kitaifa na hata kimataifa. Bologonja haijawahi kuwa ‘entry point’ kwa watalii wanaotoka au kuingia Tanzania. Haipo kwenye makubaliano hayo ya mwaka 1985.

Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku ‘njia hiyo ya panya’ kwa sababu ya kuzingatia maslahi ya kiuchumi ya Watanzania. Sababu za kiuchumi ni kwamba watalii kutoka Masai Mara nchini Kenya wakiruhusiwa kuingia nchini mwetu kupitia Bologonja, hiyo ina maana kwamba hoteli zetu zitabaki kuwa maeneo ya watalii kuja kujisaidia tu! Itakuwa hivyo kwa sababu upande huo wa Kenya kuna hoteli nyingi, na kwa sababu hiyo mtalii asingeona busara ya kutolala Kenya ilhali akitambua kuwa ana uwezo wa kuingia Tanzania na kufaidi vivutio vyote; kisha akarejea Kenya kulala. Ndugu zetu Wakenya hata wao wasingekuwa tayari kuona watalii, badala ya kuacha fedha Kenya, wanazileta Tanzania. Wanataka watalii watumie muda mrefu zaidi kwao kwa maana hiyo waache fedha nyingi zaidi huko.

Kilichofanywa na viongozi wazalendo wa wakati huo wa Tanzania, ni kuifunga kabisa Bologonja ili watalii wanaotaka kuingia kwetu wapitie Namanga, Sirari, Holili au Horohoro. Hiyo ina maana kwamba umbali wa safari usingewaruhusu kuingia na kutoka nchini mara moja. Kwa maneno mengine, ilionekana watalii wabanwe kwa utaratibu huo ili wapate muda mrefu wa kuwapo nchini mwetu na kwa sababu hiyo tuweze kufaidi zaidi fedha zao. Zipo sababu nyingine za kufungwa kwa Bologonja, lakini kwa kweli sidhani kama kuna sababu muhimu, kubwa na ya maana kimaslahi kwa Tanzania kuliko hii niliyoitaja.

Kikao cha mawaziri wa utalii wa Kenya, Uganda na Tanzania cha Februari 20, mwaka jana kilitoa miezi sita kwa Tanzania na Kenya kuafikiana masuala yao ya kiutalii; kubwa likiwa la kufunguliwa kwa Bologonja. Kama ilivyotarajiwa, miezi sita ikapita bila jibu.

Hapa ni vema wasomaji wakatambua kuwa ni Gazeti hili hili la JAMHURI ambalo liliandika juu ya mpango huo hatari wa kufunguliwa kwa Bologonja, hata ukaweza ‘kuahirishwa’. Nyalandu alikuwa na kasi ya ajabu kuhakikisha anawafurahisha Wakenya. Wahifadhi wengi, akiwamo Mama Zakia Meghji, aliyepata kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, walimkanya. Mama Meghji aliyeoongoza wizara hiyo kwa miaka mingi kuliko waziri yeyote, wakati akijadili hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, akamuonya Nyalandu juu ya mpango huo.

 

Mei 14, 2014 Mama Meghji alisema haya kuhusu Bologonja…

 

Mheshimiwa Spika, upande wa Kenya hata ukisimama upande huu wa Tanzania unaweza kuona kule, wamejenga hoteli nyingi sana, tented camps nyingi sana, tented camps hoteli karibu 50 na bado wanaendelea kujenga hizi tented camps pamoja na hoteli. Pia tunajua kwamba nauli ya kutoka Europe ambapo ndio watalii wengi wanatokea kwenda Kenya ni ndogo ukifananisha na nauli kutoka Europe kuja Tanzania. Kwa sababu za kiuchumi pia, wana ndege zao Kenya Airways na kadhalika, kwa hivyo, wanalipa fedha kidogo kwa nauli kutoka Europe kuja Kenya ukifananisha na kutoka Europe kuja Tanzania. Sasa tujiulize, kwa nini watalii waje huku kama pamoja na nauli ndogo watatembelea Mbuga ya Serengeti kupitia Maasai Mara upande wa Kenya? Waje kufanya nini? Kama wanataka kutembelea Serengeti watalipa fedha kidogo, wataingia Serengeti na kuona wanyama mbalimbali hakuna haja kwa wao kuja Tanzania kwa maana hiyo.

Sera hii ya kutofungua mpaka huu kama nilivyosema ni ya miaka mingi. Mimi nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa muda wa miaka tisa, Waziri anayeshughulikia Afrika Mashariki pamoja na Mawaziri mbalimbali alijaribu sana kunishawishi tukubali tufungue mpaka huu ya Bologonja. Huyu Waziri nimtaje ndani ya Bunge alikuwa ni Mheshimiwa Biwott, nafikiri watu wengine wanamuelewa. Alikuwa Waziri, alikuwa na uwezo mkubwa sana, alikuwa na ndege na kadhalika, kwa hiyo, alijaribu kushawishi sana ili mpaka huu ufunguliwe lakini upande wa Tanzania tulikataa. Napenda kusema kwamba tuliungwa mkono kwanza na Waziri aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye hivi sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tuliungwa mkono na Rais wa wakati ule ambaye ni Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kabisa ningemuomba Mheshimiwa Waziri jambo hili aliache kama vile Kamati ilivyosema. Hivi sasa upande wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, langu lilikuwa la Bologonja. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyosema kwamba hatutafungua Bologonja na status quo haijabadilika. Lakini ningependa kusema kwamba, alivyosema juu ya suala la independent study, huu ni ujanja. Hii Independent Study imekuwa inazungumzwa miaka yote hiyo, huu ni ujanja wa upande wa Kenya. Kwa hiyo, tunasema kwamba kwa kweli ni kama vile kusema kitu hiki ni cheupe au kitu hiki ni cheusi, halafu ukasema nataka kufanya study kujua kama ni cheupe au ni cheusi. Tulishasema suala la uchumi, kwa hiyo, tunaomba msimamo wa Serikali uwe hapo hapo wa kutofungua Bologonja.

Mwisho.

Kunahitajika maelezo gani ya maana kuyazidi haya ya Mama Meghji? Vikwazo vyote hivi vilipoonekana kukwamisha mpango wa Nyalandu, Oktoba, mwaka jana akakutana tena na wenzake. Hapo akabanwa na kuhojiwa kwanini hajatelekeza ahadi yake.

Kwa kutaka kumaliza udhia, na pengine kwa maslahi binafsi aliyonayo, akarejea ahadi ya kuwafungulia Wakenya Bologonja.

Alitumia maneno dhaifu, lakini yenye tija kwa Wakenya kama njia ya kuwapoza. Nakumbuka alitumia maneno kama “ninyi ni ndugu zetu, suala la Bologonja tutaliangalia namna ya kulitekeleza, msiwe na wasiwasi”. Kwa Wakenya, kauli hiyo ikawa ndiyo ngao yao. Hadi leo wanaendelea kumuuliza, vipi mbona hutekelezi ahadi?

Wakenya walipoona hakuna kinachoendelea, nao wakaamua kutikisa kiberiti. Wameona pa kuanzia ni kwenye magari ya Tanzania yanayoingia Kenya kuchukua watalii.

Kuna ujanja ujanja mwingi unaendelea kwenye hiki kinachoitwa mgogoro. Ukweli hausemwi. Wala Watanzania wasidhani Wakenya wamekurupuka tu kuzuia magari yao kufanya kazi nchini Kenya. Mgogoro huu umejikita juu ya kufunguliwa kwa mpaka wa Bologonja, basi! Huo ndio ukweli. Bologonja ikifunguliwa, Wakenya wataruhusu, si magari tu, bali hata bodaboda na bajaji za Tanzania kuingia Kenya kuchukua watalii. Watakunywa champagne.

Hasara wanayopata Watanzania sasa kwa tukio la kuzuiwa magari ya Tanzania, chanzo chake ni ahadi ya Nyalandu ambayo kama angekuwa makini, alipaswa kujiuliza ni kwanini Mwalimu Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, hadi Mzee Benjamin Mkapa waligoma kuifungua Bologonja. Alipaswa ajiulize ni kwanini Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ndio ione umuhimu wa kufunguliwa kwa mpaka huo.

Nyalandu ni kiongozi anayesaka sifa. Mara zote anataka aonekane yuko tofauti na wengine. Kwake yeye, wengine wote si weledi, isipokuwa yeye. Ndio maana tunaona sasa amesaini kubadili sheria ya uwindaji wanyama kutoka miezi sita na kuwa miezi tisa! Anamburuza Katibu Mkuu wa sasa. Hajihangaishi kujua kwanini ilikuwa miezi tisa, ikarejeshwa sita; na sasa kwanini iende miezi tisa. Aangalie. Nyalandu ni mwanasiasa. Atamharibia. Nyalandu ameonywa na wahifadhi na wadau wengine, lakini kagoma. Amegoma kwa sababu yeye anajua kila kitu. Anahaha kupitisha dhambi hiyo. Kwa kweli nitamshangaa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na hata Rais Kikwete, ambaye ni mhifadhi mzuri sana, endapo watabariki dhambi hii.

Ndio maana tunaona anataka umiliki vitalu vya uwindaji uwe miaka 15 hadi 20 badala ya miaka mitano ya sasa. Ndio maana anataka kupunguza ada za kuwinda wanyama na ndege akisema ziko juu mno kana kwamba wawindaji wanalalamika. Hii ni sawa na kushusha bei ya tanzanite ilhali ukijua hakuna nchi nyingine tunayoshindana nayo kuchimba tanzanite!

Ndio maana anaona waliojenga ukumbi wa kisasa pale Mpingo House ni wapuuzi, na kwa maana hiyo ameamua mikutano yake mingi aifanyie katika hoteli za kitalii kwa gharama kubwa zinazolipwa na TANAPA, Ngorongoro na mashirika mengine.

Nini kifanyike? Wakenya watambue kuwa ahadi ya Nyalandu ya kufungua Bologonja ni ahadi yake binafsi. Kama yapo makubaliano waliyoingia, ieleweke kuwa hayo ni yao wenyewe. Siyo ya Watanzania.

Rekodi ya Nyalandu kwenye uhifadhi si nzuri.

Ametangaza kuwania urais. Kwanini tusiamini kuwa ni Nyalandu aliyeandaa mgogoro huu wa Tanzania na Kenya kwa maslahi yake ya kutaka ‘kuzikusanya’ ili aweze kuingia Ikulu?

Kwanini tusiamini kuwa anafanya hivi ili aungwe mkono na wafanyabiashara Wakenya na hata Serikali ya nchi hiyo, ili pamoja na Wamarekani (kama alivyokwishathibitisha mwenyewe), mwaka huu mwishoni ulimwengu ushuhudie akiapishwa?

Ni Nyalandu huyu huyu aliyetunga hadaa akidai kwamba wabunge walikuwa wamejipanga kukwamisha bajeti yake ya mwaka 2014/2015 endapo wakurugenzi aliokuwa hawataki, wasingeondoka. Alisambaza uongo kiasi kwamba ikaonekana wabunge kweli wana mpango wa kukwamisha bajeti. Ilipobainika kwamba ule ulikuwa uongo, tayari bajeti yake ilishapita!

Kwa hili la kufunguliwa kwa Bologonja, kwanini Watanzania wasiamini kuwa ni Nyalandu mwenyewe aliyelipika, na sasa anajitahidi kulisawazisha kwa lengo la kujipatia sifa? Kwanini miaka yote lilipoibuka, lilizimwa kwa hoja likaisha, lakini sasa limepamba moto?

Ule mkataba wa mwaka 1985 (ambao ninao), ulisainiwa na Wizara ya Mambo ya Nje. Yeye si Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Ana mamlaka gani kurekebisha au kupindua jambo lililosainiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa? Kuna siri gani inayomfanya asiihusishe wizara hiyo?

Hatuhitaji nguvu kubwa ya kufikiri juu ya jambo hili. Hiki kinachoitwa mgogoro, si mgogoro. Ni mpango ulioundwa na Nyalandu kwa maslahi yake ya kiuchumi na kisiasa. Lakini kama kuna malipo kayapata kutoka kwa Wakenya kwa ahadi ya kufungua Bologonja, atambue mpango huo utamgharimu. Sioni kwenye hili atawapa Wakenya maneno gani ya kuwaridhisha na wakati huo huo akawaridhisha pia wafanyabiashara ya utalii wa Tanzania.

Sinema hii imeanzishwa na Nyalandu kwa maslahi yake anayoyajua yeye. Kama ni suala la watalii wetu kuingia nchini, nakubali Wakenya watuzuie kutumia uwanja wao. Hiyo itatusaidia kupata akili na kasi ya kuhakikisha nasi tunakuwa na ndege kama zao. Bologonja isifunguliwe.

 

1327 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!