Wafanyakazi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania wametangaza mgogoro na mwajiri wao, wakidai haki ya kuachishwa kazi. Wafanyakazi wanaohusika katika mgogoro huo ni 179 kutoka katika Idara ya Huduma kwa Wateja walioajiriwa kati ya mwaka 2001 na mwaka 2011.

Wakizungumza  kwa nyakati tofauti kwa kwa sharti la kutojwa majina, wafanyakazi hao wamesema baadhi waliajiriwa na Kampuni za Celtel na wengine Zain na Airtel kwa masharti ya kudumu. Mmoja wa wafanyakazi hao ameiambia JAMHURI kwamba Kampuni ya Celtel iliiuzia Zain ambayo nayo iliiuza kwa Airtel, ambapo wafanyakazi hao walichukuliwa bila kubadilishiwa mikataba yao kwa mwajiri mpya.

 

“Katika makubaliano ya Airtel na waajiriwa ilikubaliwa kwamba mfanyakazi atabaki na haki zake zote, na iwapo kutakuwa na kutoridhika katika utekelezaji wa mkataba, mwajiriwa atakuwa huru kurudi kampuni yake (Airtel) muda wowote,” amesema mfanyakazi mmoja.


Amesema mgogoro huo ulianza baada ya wafanyakazi kukaa na mwajiri wa sasa (Spanco) na kuuliza haki za malipo ya kuachishwa kazi Airtel. Amesema baada ya mwajiri huyo kuwakana wenzao walioachishwa kazi, kwamba hawana haki ya kudai fidia ya kuachishwa kazi kwa kuwa haki za nyuma zote hazitambui, hivyo wanatakiwa kumdai mwajiri wa zamani ambaye ni Airtel.

 

Amesema mgogoro huo umepewa namba CMA/DSM/KIN/800/11 na mwingine CMA/DSM/KIN/737/11/788.

Amesema mwajiri aliwaambia kwamba haki zote za nyuma zilifutwa kwa mujibu wa mwajiri wa sasa. Hata hivyo, wafanyakazi waliamua kwenda kwa mwajiri wa zamani (Airtel) kuhusu haki hiyo lakini hakuonesha ushirikiano.


Baada ya kuona wanadharaulika, waliamua kumwandikia mwajiri huyo barua kukumbushia madai yao, ambapo aliwajibu lakini hakuridhika. Amesema waliomba kukutana na mwajiri wa zamani, ambapo walikwenda wawakilishi wa wafanyakazi hadi makao makuu ya Airtel kwa majadiliano. Lakini makubaliano yaliyofikiwa siku hiyo ni kwamba mwajiri atoe cheti cha huduma, hata hivyo mwajiri alikataa kulipa gharama nyingine.

 

Baada ya kuona hatua ya majadiliano haina mafanikio, wafanyakazi waliamua kufungua mgogoro katika Baraza la Usuluhishi namba CMA/DSM/KIN/R.61/13. Amesema mwajiri alikiri kudaiwa fedha hizo na kuomba muda akapige hesabu kisha atoe msimamo, lakini alidai kuwa hawezi kuwalipa wafanyakazi haki ya kuachishwa kazi kwa kuwa amehamishia kwa mwajiri wa sasa, Airtel.  Baada ya uamuzi huo, ilionekana kwamba hakuna njia nyingine zaidi ya kurudi katika mkataba, na kipengele cha 3 cha makubaliano ya mwajiri na mwajiriwa. Kifungu hicho kinatoa uhuru kwa mwajiriwa kurudi katika ajira yake, iwapo hataridhika na hali ya utekelezaje wa mikataba.

 

Akizungumza kwa njia ya simu, Meneja Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, amesema kuwa hana taarifa ya mgogoro huo. Lakini baada ya kuelezwa na JAMHURI, Mmbando alikiri kufahamu mgogoro huo na kumtaka mwandishi aende ofisi za Airtel, kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu.

 

“Kaka nakuomba uje Jumatatu ofisini tuzungumze, hili suala la kuzungumzia kwenye simu naomba uje ofisini…nakuomba tafadhari sana kaka,” amesema na kukata simu.

Hata hivyo, JAMHURI ilimtumia ujumbe mfupi wa maneno katika simu yake ya kiganjani kuwa Jumatatu haitawezekana kwani gazeti lilikuwa liko mbioni kwenda mtamboni lakini hakujibu ujumbe huo.


By Jamhuri