Jumatano iliyopita timu za Simba na Yanga zilishindwa kuoneshana ubabe, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kabla ya mchuano huo, Simba ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushinda hasa kwa vile iliingia uwanjani ikiwa imeshinda michezo yote minne ya awali, huku Yanga ikiwa imeshinda miwili na kufungwa mbili pia.

Mwamuzi Mathew Akrama, ambaye hata hivyo, ameshasimamishwa kwa tuhuma za kuchezesha mtanange huo chini ya kiwango, anashutumiwa kuwa aliibeba Simba, jambo lililosababisha kuzuka kwa mvutano mkubwa wa ubora wa timu hiyo kwa mahasimu wao, Yanga. Wadadisi wa masuala ya soka wanatoa mfano wa jinsi alivyomtoa uwanjani kwa kadi nyekundu mshambuliaji Simon Msuva wa Yanga.


Akrama alitoa adhabu hiyo katika dakika ya 79 kwa kile alichodai kuwa Msuva alijiangusha makusudi ili kupoteza muda. Hata hivyo, Akrama hakufanya hivyo kwa kipa Juma Kaseja wa Simba aliyeonekana kuchelewesha muda mara kadhaa. Anatuhumiwa pia kwa kutochukua hatua kali kwa kumtoa nje kiungo Haruna Moshi “Boban” wa Simba, aliyemvunja mfupa wa mguu beki Kelvin Yondan wa Yanga, dakika mbili kabla hajamtoa nje Msuva.


Pamoja na rafu ile kuonekana waziwazi kuwa ni mbaya, mwamuzi huyo alishindwa kutoa kadi nyekundu kwa kiungo huyo. Hatua hiyo ilikuja huku akiwa ameshakataa bao safi la Yanga lililofungwa na mshambuliaji wa kulipwa kutoka Burundi, Didier Kavumbagu, katika dakika ya 53.


Mwamuzi huyo alilikataa bao hilo akidai kipa Kaseja alisukumwa wakati akiudaka mpira huo na kumtoka mikononi, hivyo ukamkuta Kavumbagu na kuutumbukiza wavuni. Hata hivyo, marudio ya picha za televisheni yalithibitisha kwamba hapakuwa na tukio hilo la utetezi unaotolewa na Akrama.


Wakati Akrama akidai kuwa Kaseja alisukumwa, kipa huyo alijifanya kuwa ameumizwa mdomoni na kuanza kuonesha kama anatoka damu kinywani, lakini picha hiyo ilionesha kuwa hakuguswa na mtu yeyote wala sehemu yoyote na mpira huo hakuugusa hata kwa ncha ya kidole. Kweli Akrama hawezi kukwepa lawama za ‘kuchemka’ katika mchezo huo.


By Jamhuri