Siku moja niliulizwa ninamkumbukaje Mama Joan Wicken? Haraka haraka jibu lililonijia kichwani lilikuwa: “Alikuwa mchapa kazi hodari sana, aliyeitumikia nchi yetu kwa moyo wake wote na kwa nguvu zake zote!”

Jina la “Mama Wicken” halitakuwa geni kwa Watanzania waanzilishi wa Chama TANU kabla ya Tanganyika kupata Uhuru na kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi uliotukuka wa Baba wa Taifa letu Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


Historia ya utendaji kazi wa Mama Joan Wicken nchini mwetu inaanza kabla nchi yetu haijapata Uhuru.  Mwaka 1958 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa kiongozi wa Chama cha Kupigania Uhuru wa Tanganyika – TANU, alifanya ziara nchini Uingereza kwa mwaliko wa Chama cha Leba (Labour Party).  Katika ziara hiyo, alivutiwa sana na mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwenye Chuo cha Ruskin kilichokuwa kinamilikiwa na Chama cha Leba.  Mafunzo hayo yalikuwa yakiwatayarisha ‘Makada’ wa Chama cha Leba ambao hatimaye walikwenda kueneza kwa wananchi, chachu ya itikadi ya Chama hicho.  Mwalimu aliuomba uongozi wa Chama cha Leba kukisaidia Chama cha TANU ili kiweze kuanzisha Chuo kama kile cha Ruskin.  Ombi lake lilikubaliwa.  Chama cha Leba kiliteua Maafisa wake wawili wanawake kuja Tanganyika kukisaidia Chama cha TANU kufanikisha azma ya kuanzisha Chuo hicho.  Mmoja wa Maafisa hao wawili alikuwa Mama Joan Evelyn Wicken aliyekuwa na cheo cha Ofisa Msaidizi katika Jumuiya ya Madola kutoka Chama cha Leba ambaye naye aliwahi kupata mafunzo kwenye Chuo hicho.


Wakati wa uhai wake, Mama Wicken alipenda kusimulia alivyowasili nchini Tanganyika kwa mara ya kwanza mwaka 1959  kufanya uchunguzi na baadaye kusaidia shughuli za kuanzisha Chuo cha Chama cha TANU cha Mafunzo ya Uongozi na Uhamasishaji cha Kivukoni.  Alieleza jinsi walivyopokewa vizuri na Chama cha TANU.  Mwalimu aliwapa gari alilokuwa akilitumia yeye kwa shughuli za Chama cha TANU, walitumie kwenye shughuli za kutafuta michango kwa ajili ya Chuo kilichodhamiriwa.  Mama Wicken alikuwa akikumbuka walivyosafiri nchini kote, wakati mwingine wakiongozana na msafara wa viongozi wa Chama cha TANU waliokuwa kwenye harakati za kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama.  Katika misafara hiyo, walitambulishwa kwa wananchi na walipata fursa ya kuwahamasisha wananchi kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha TANU.


Wakati mwingine walisafiri peke yao na dreva wao Said Kamtawa (Hayati) ambaye alitumika kama ‘mkalimani’ aliyewasaidia mabinti hao Waingereza kueleza kwa Kiswahili madhumuni ya Chuo cha Chama cha TANU na kuomba michango kwa wananchi.  Ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, mayai, mahindi, maharage na senti moja, tano na kumi ndiyo iliyokuwa michango kutoka kwa wananchi waliohamasika kuchangia.  Pia, walikuwepo Waasia wafanyabiashara waliojitolea kuuchangia mfuko huo wa kuanzisha Chuo cha Chama. Mwafrika mmoja mfanyabiashara aliyetoa mchango mkubwa sana katika shughuli za TANU alikuwa Hayati Mzee John  Rupia.


Wakati shughuli za kuchangisha zikiendelea Chama cha TANU kilifanikiwa kupata majengo ya hoteli moja iliyokuwa haifanyi kazi kwenye eneo la Kivukoni, Kigamboni. Mabinti Waingereza Mama Wicken na mwenziwe walishirikiana bega kwa bega na wananchi wanachama wa TANU kufyeka vichaka na majani marefu yaliyokuwa yameota kuzunguka majengo hayo, ukarabati mkubwa ulifanywa na hatimaye Chuo cha Kivukoni kiliweza kuanzishwa.


Baada ya kukamilisha kazi hiyo, Mama Wicken alitaka kurudi kwao Uingereza lakini wakati huo nchi ilikuwa imekwishapata Uhuru.  Mwalimu alimuomba awe Msaidizi wake Mahsusi (Personal Assistant), akakubali.


Waliowahi kumfahamu Mama Wicken wataelewa kuwa sababu kubwa iliyofanya Mwalimu amuombe kuwa Msaidizi wake ni ukweli kwamba mama huyo alikuwa mchapakazi hodari sana.  Hakujali kufuata saa zilizopangwa na Serikali.  Ombi lake kwa Mwalimu lilikuwa kumruhusu aingie kazini saa 3.00 asubuhi badala ya saa 1.30 na baada ya hapo hakuwa na saa ya kutoka kazini aliweza kufanya kazi hadi usiku!


Halikadhalika, waliofanya naye kazi Ikulu enzi hizo, watakumbuka kwamba alikuwa hana makuu kabisa.  Alianza kutumia usafiri wa ‘scooter’ na baadaye akawa  na kigari  kidogo ‘Morris minor’ ambacho alikitumia kwa shughuli zake za kazi na za binafsi, hakutaka gari la Serikali.  Asubuhi kwenda kazini Ikulu aliendesha gari lake kutoka kwenye hosteli aliyokuwa akiishi ya ‘Salvation Army’ iliyoko Kilwa Road hakutaka nyumba ya Serikali.  Jioni majira ya saa 1.00 aliondoka Ikulu kuelekea Msasani ambako aliketi kubadilishana mawazo, kupata muongozo na kupewa kazi na Mwalimu.  Saa mbili usiku aliingia kwenye ‘Morris Minor’ yake na kurudi nyumbani kwake Kilwa Road.

Wapo watakaojiuliza, huyu Mama aliyekuwa akishinda ofisini tangu saa 3.00 asubuhi hadi saa mbili usiku alikuwa anakula?  Miss Wicken alikuwa anabeba mkate wake unaoitwa “sandwich” kwa kimombo na nyanya yake moja au tunda lolote.  Alikuwa kamwe hanywi maji, chai ndiyo ilikuwa kinywaji chake wakati wote aliposikia kiu.  Hata pale Mwalimu Nyerere alipotoa agizo kwamba wapishi wa Ikulu wawe wanampa Mama Wicken chakula cha mchana, Mama huyo aliona hana haki ya kupata chakula cha Ikulu wakati yeye si familia ya Rais!


Uadilifu wa Mama Wicken kazini ulikuwa ni wa hali ya juu. Kazi yake ilikuwa ikimpa fursa ya kusafiri na Rais ndani na nje ya nchi akiwa Msaidizi wake aliyekuwa akishughulikia hotuba zote alizokuwa akizitoa Mwalimu Nyerere kwa lugha ya Kiingereza.  Kila baada ya safari Mama Wicken alikuwa akirejesha hesabu ya masurufu aliyopewa bila kuchelewa.  Endapo kwenye safari wenyeji walitoa huduma zote zilizohitajika kwa wajumbe wa msafara, Mama Wicken alikuwa akirejesha fedha zote alizopewa za masurufu ya safari kwa kwa Mhasibu Ikulu.  Aliamini kwamba wananchi walikuwa na shida nyingi zilizohitaji pesa – walihitaji dawa, elimu na kadhalika, fedha hizo ilipasa zitumike kwa kusaidia wananchi badala ya kuchukuliwa na wafanyakazi ambao walikuwa wakilipwa mishahara na kulipiwa gharama zote safarini.


Mwalimu alipostaafu Urais mwaka 1985 na hatimaye uenyekiti wa Chama mwaka 1987, Mama huyu aliamua kurudi kwao Uingereza.  Wazazi wake na dada yake walikwishafariki kwa hiyo aliakwenda kuishi na rafiki zake kwenye kijiji cha Keighley, eneo la Leeds, Yorkshire kaskazini magharibi ya Uingereza. Serikali ya Tanzania iliamua kumlipa ‘Kiinua Mgongo’ kwa kazi aliyofanya kwa Taifa na kwa utumishi wake uliotukuka.  Alipopelekewa hundi ya mafao yake, hakuipokea, aliirudisha hundi hiyo Serikalini kwa madai kwamba wananchi wa Tanzania walizihitaji zaidi fedha hizo kuliko yeye alivyozihitaji!


Mwalimu Nyerere alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini mwaka 1989, alimuomba Mama Wicken arudi Tanzania ili aendelee kuwa Msaidizi wake katika shughuli za Tume hiyo.  Aliporejea Mwalimu alimwambia “Sasa nataka uwe Msaidizi wangu hadi siku ya mwisho!”  Akiwa na maana ya hadi siku ya mwisho wa maisha yao. Mama Wicken alipenda kusimulia hayo kwa tabasamu na kueleza kwamba alikuwa anamheshimu sana Mwalimu na alikuwa amemzoea sana kikazi, asingeliweza kukataa ombi hilo maana alikuwa bado na nguvu za kuweza kuendelea kufanya kazi na Mwalimu.


Bahati mbaya, ilipofika mwaka 1994, hali ya Mama Wicken kiafya ilianza kuzorota.  Aliamua kurudi kwao moja kwa moja kwa makubaliano kwamba angeendelea kumsaidia Mwalimu Geneva Uswiss kwa shughuli za kazi za Kituo cha Kusini (South Centre) – kilichoanzishwa baada ya Tume ya Kusini kumaliza kazi yake na kutoa ripoti.


Mama Wicken aliendelea kuwa Msaidizi wa Mwalimu Nyerere hadi Mwalimu alipoaga dunia. Akaja nchini kuungana na Watanzania katika mazishi ya Baba wa Taifa. Baada ya msiba, ofisi ya South Centre Geneva ilifanya kikao cha dharura kutathmini hali ya baadaye ya ofisi hiyo baada ya kifo cha Mwalimu. Mama Wicken kabla ya kikao kuanza, alinyanyuka na kumwambia aliyekuwa Mwenyekiti wa muda: “Aliyeniteua kumsaidia hayupo tena.  Kwa hiyo, wakati wangu wa kurudi nyumbani kupumzika umefika!”  Akibubujikwa machozi alitoka kwenye chumba cha mkutano na kusababisha wote waliokuwa kwenye kikao wapatwe na simanzi sana.


Hata hivyo, busara zake zilihitajika sana katika kipindi cha mpito baada ya Mwalimu kufariki.  Naye, wakati wote alikuwa yuko tayari kusaidia alipoombwa kutoa ushauri. Pamoja na hayo, kila aliyewasiliana naye alikuwa akielezwa jinsi ambavyo alikuwa ‘bize’ akitafsiri maandishi yake (‘notes) ya hatimkato (shorthand) aliyokuwa akiandika kila alipokuwa akienda Msasani kuongea na Mwalimu, na kila alichofanya kila siku tangu Tanganyika ipate Uhuru.  Mwalimu alipofariki mwaka 1999, Mama Wicken alisema ndio kwanza alianza kutasfiri ‘notes’ za mwaka 1972!


Mama huyu alikuwa mzalendo wa nchi yetu kuwashinda baadhi ya ‘wazalendo’ wenyewe.  Baada ya kurudi kwao wakati wote alikuwa akikumbuka michango na juhudi zilizofanywa na wananchi katika miaka ile kabla ya Uhuru ili kuanzisha Chuo cha Kivukoni bila kuomba wala kutumia hata senti moja kutoka nje ya nchi yetu.  Lakini, alinung’unika kwamba madhumuni mazima ya kuanzishwa kwa Chuo cha Kivukoni yalibadilishwa kwa sababu ya Tanzania kutaka “kwenda na wakati!”  Halikadhalika, alilalamikia sana kufutwa kwa ‘Azimio la Arusha’ katika siasa za Chama cha Mapinduzi!  Aliamini kwamba Azimio la Arusha lilikuwa ndiyo dira ya taifa, nguzo kuu ya uadilifu na ‘mdhibiti’ muhimu wa kuzuia kukua kwa tabaka la ‘walionacho’ na ‘wasionacho’ miongoni mwa Watanzania.


Mama Wicken, raia wa Uingereza atakumbukwa kwa kuishi maisha ya ujana wake hadi kuzeeka  akilitumikia Taifa la Tanzania na kutufundisha ‘uchapakazi’.  Alikuja Tanganyika akiwa msichana wa miaka 34 – alizaliwa tarehe 12 Julai 1925.  Hakuwahi kuolewa ingawa aliwahi kupata mchumba Mwafrika mwanasiasa nchini Kenya ambaye kwa bahati mbaya kabla hawajafunga ndoa aliuwawa kwa kupigwa risasi. Pamoja na mapenzi kwa Tanzania, Joan Wicken hakuisahau nchi yake ya asili.  Wakati wote yeye alikuwa ni “Mwingereza” aliyeipenda Uingereza kama alivyoipenda Tanzania – kwa moyo wake wote na kwa nguvu zake zote.  Maisha yake yalifikia kikomo Jumapili mchana tarehe 5 Desemba 2004 alipoaga dunia kwa amani, alipofumba macho akiwa ameketi kwenye kiti cha hospitali ya Serikali kijijini kwake Keighley Leeds, Uingereza ambako alikuwa amelazwa kwa muda wa wiki sita akisumbuliwa na kifua kilichomletea matatizo ya kupumua.

Mwenyezi  Mungu ailaze Roho ya Mama Joan Evelyn Wicken, mahali pema Peponi.

Mwandishi wa makala hii, Anna Mwansasu, ni msomaji wa Gazeti la Jamhuri. Alipata kufanya kazi ofisi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pia na Mama Joan Evelyn Wicken.

1818 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!