Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kadhaa wamepiga marufuku matumizi ya nafaka kutengenezea pombe. Wengine wameenda mbali zaidi kwa kuwaamuru wakulima kutouza mahidi mabichi.

Mwishoni mwa mwaka juzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipiga marufuku matumizi ya chakula cha msaada kutumika kutengenezea pombe. 

Hapa kuna upigaji marufuku unaofanana, ingawa mmoja unaweza kuwa na mantiki. Huu wa Waziri Mkuu una mantiki kwa kuwa amezuia matumizi ya ‘chakula cha msaada’ kutumika kutengenezea pombe. Una mantiki kwa sababu si dhambi kwa anayetoa msaada kuuambatanisha na masharti! Inapotokea hali ya aina hiyo, ni wajibu wa mpokea msaada kuyakubali masharti ili asaidiwe, au kuyapinga masharti ili akose huo msaada.

Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa kumzuia mkulima kuyatumia mazao yao kadri ya utashi wake ni uonevu. Viongozi wasidhani wananchi, hasa wakulima; ni watu mbumbumbu wanaostahili kupewa maelekezo, hasa maelekezo hayo yanapokuwa yanakiuka haki za msingi za binadamu.

Kumzuia mkulima kuuza mahindi yake mabichi, hasa akitambua kuwa aina hiyo ya mahindi inampa faida nono kuliko ile ambayo angepata kwa kuuza mahindi makavu, ni kumwonea.

Pale Dumila, Morogoro, kuna vijana wengi wanaouza mahindi yaliyochomwa. Yanapatikana kwa kipindi chote cha mwaka. Yapo yanayotoka katika mashamba ya vijana wenyewe, mengine wanayapata kutoka kwa wakulima.

Mkulima anayeuza mahindi mabichi anapata faida kubwa yenye kumfaa katika maisha yake ya kila siku. Wapo waliojenga nyumba kwa kazi hiyo ya mahindi mabichi. Hindi moja linauzwa kwa wastani wa Sh 500. Debe moja la mahindi makavu kwa bei ya sasa ni wastani wa Sh 20,000. Unahitaji mahindi 40 mabichi (bila kujali ukubwa wake) kupata Sh 20,000. Lakini unahitaji idadi kubwa mno ya mahindi makavu kujaza debe moja. Hesabu za kawaida kabisa zinamshawishi mkulima kuuza mahindi mabichi ili apate faida kulingana na jasho lake halali shambani.

Hatuwezi kuepuka baa la njaa kwa kuwaonea wakulima kwa kuwawekea sheria ndogo ndogo zinazowaathiri kimapato. Mkulima si mjinga. Hahitaji taarifa ya Serikali kumpa hadhari ya chakula. Yeye mwenyewe kwa kuyatazama majira yalivyo ana uwezo wa kubaini uwepo wa baa la njaa. Hakuna mkulima mbumbumbu wa kuuza mazao yote mabichi akasahau, au akapuuza kubakiza akiba ya kumfaa kwa chakula.

Mwito wangu kwa viongozi wa Serikali ni kuwa wawaache wakulima wauze mazao yao kadri wanavyoona inafaa. Wakati wa kilimo wanahangika wenyewe. Wengi wao hawawajui na wala hawajawahi kuwaona maofisa ugani. Mbolea wanazitafuta wenyewe kwa gharama kubwa. Wao wenyewe wanaamia ndege na kufukuza wanyama waharibifu wa mazao. Suluba hizi zinawatosha. Hawahitaji nyingine kutoka kwa wakuu wa wilaya au wakuu wa mikoa ambao hawana msaada wowote kwenye kilimo chao.

Njia nzuri ya kukabiliana na baa la njaa ni kwa mamlaka zinazohusika kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha kisasa – chenye tija.

Wakulima wawezeshwe kuendesha kilimo cha umwagiliaji. Wakopeshwe zana na pembejeo kwa bei zinazohimilika. Wataalamu wa ugani wazuru mashamba yao na kuwapa mbinu za kilimo bora chenye tija.

Hizo ndizo mbinu zinazoweza kuwafanya wanufaike zaidi na kwa maana hiyo Serikali inaweza kuwa na sababu za msingi za kuwataka wasiuze ‘mahindi mabichi’. Kama kila kitu anahangaika mkulima mwenyewe, basi hata uamuzi wa auze mahindi ya aina gani aachiwe yeye mwenyewe.

Pili, hili la kupiga marufuku matumizi ya nafaka kutengeneza pombe za kienyeji nao ni ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Mkulima anayehangaika mashambani akipambana na wakati mgumu kwenye kilimo, anahitaji kujiliwaza. Wapo wakulima wanaojiliwaza kwa pombe au ngoma. Hawa ni wale wasiokuwa na uwezo wa kununua bia za viwandani au pombe nyingine zenye bei ghali.

Sherehe zetu vijijini mara nyingi zimekuwa zikinoga kwa uwepo wa vinywaji mbalimbali kama vile pombe zilizotengenezwa kwa nafaka. Utakuwa uonevu wa hali ya juu kuzuia matumizi ya nafaka kwa ajili ya pombe kwenye sherehe kwani wakulima wana haki ya kufaidi kile kisichopingana na imani zao.

Hao wakuu wa wilaya na mikoa wanaotoa amri za kuzuia pombe zinazotokana na nafaka, watajisikiaje nao wakiambiwa sherehe zao zisiwe na bia au vinywaji vingine?

Wanatambua kuwa wakulima hawawezi kununua soda. Wanatambua kuwa hata togwa linatengenezwa kwa nafaka! Wanapozuia matumizi ya nafaka wasidhani wanazuia pombe tu. Wanazuia hata togwa! Hii si haki hata kidogo.

Umaskini umewafanya watumie mahindi, ulezi, mtama na aina nyingine za nafaka wanazozalisha wenyewe kutengeneza kinywaji kinachowapa fursa ya kuyasahau machungu ya maisha.

Kwa mtazamo wa kawaida tu, wanywaji pombe za kienyeji ni wengi kuliko idadi ya wale wanaokunywa pombe za kisasa. 

Kuzuia utengenezaji na unywaji pombe za kienyeji, ukiacha kuwa ni kuwatesa makabwela wanaohitaji kujiliwaza baada ya kazi ngumu za kutwa nzima, ni kuua kipato cha maelfu kwa maelfu ya Watanzania.

Miongoni mwetu wamo waliosoma shule za msingi hadi vyuo vikuu kwa fedha zilizotoka kwa wazazi au walezi waliotengeneza na kuuza pombe za kienyeji.

Familia zetu nyingi zinapata mahitaji muhimu ya matibabu kutokana na fedha wanazopata kutoka kwenye pombe zilizotengenezwa kwa nafaka. Kuna maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanaopata uwezo wa kununua ‘panadol’ kutokana na biashara ya pombe za kienyeji. Ilimradi Tanzania ni nchi yenye kutoa uhuru kwa mtu kuishi kulingana na imani yake, hawa wanaotengeneza au kuuza pombe zinazotokana na nafaka waachwe wafanye shughuli zao.

Endapo viongozi wa Serikali sasa wanatambua umuhimu wa wakulima hata kuamua kuwawekea masharti ya kutunza nafaka, basi ufanyike utaratibu wa kuwawezesha kuachana na pombe za kienyeji zinazotokana na nafaka. Wawezeshwe ili wamudu kununua bia na pombe nyingine. Lakini kama bia zinapangwa bei kwa kuzingatia kipato cha matajiri na kuwaweka kando makabwela, viongozi wa umma hawana mamlaka ya kuwazuia kupata wanachokitaka.

Kadhalika, huu utaratibu za kuwazuia wananchi kuuza mazao nje ya nchi nadhani hauna tija kwa wananchi na nchi kwa jumla. Endapo mkulima au mfanyabiashara anaona kuuza mahindi Zambia, Kenya au Uganda kuna faida kubwa kuliko kuuza hapa nchini, kumzuia kufanya hivyo si jambo la kiungwana. 

Nchi yetu ina ardhi nzuri na maji ya kutosha. Tuna maeneo yanayoweza kutumiwa kulima mazao ya kulisha mataifa mengi ya ndani na hata nje ya Afrika. 

Mataifa kama Sudan Kusini yana shida ya vyakula. Tunachopaswa kukifanya ni kuhakikisha wakulima wetu wanalima zaidi na kuuza nje ziada. Upigaji marufuku huu wenye mwelekeo wa kisiasa hauna faida kwa mkulima na mfanyabiashara Mtanzania.

Nihitimishe kwa kuwaomba wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kutotumia baa la njaa kuwaonea wananchi maskini. Rais John Magufuli amesema huu ndiyo wakati mzuri kwa wakulima kutajirika! Utajiri huo utawezekana endapo wakulima wataachiwa uhuru wa kuamua mambo yao kwa mazao wanayohangaika kuyalima wao wenyewe. Wajibu wa viongozi ubaki kuwakumbusha wakulima wajibu wa kutunza vyakula badala ya kuwazuia.

Kama kuuza mahindi mabichi kuna tija, mkulima aachwe auze hayo mahindi. Kama uuzaji pombe zinazotokana na nafaka umekuwa chanzo murua cha kuboresha maisha ya baadhi ya Watanzania, waachwe waendelee na shughuli zao.

Utaratibu huu wa kuwafanya wakulima kama watu malofa wasiokuwa na uwezo wa kufikiri na kuamua maisha yao, hauna budi kufika tamati.

Nayasema haya kwa kuzingatia kuwa wazazi wangu ni wakulima. Mimi nimelima. Kwa kuyajua madhila yanayotokana na kazi ya kilimo, nashawishika kutetea mpango wowote wa kuwafanya wawe huru kuamua wauze mahindi mabichi au makavu. Nashawishika kuwatetea waachwe waendelee kutengeneza vinywaji baridi na vinywaji vikali kutokana na nafaka. Huu ndiyo muda wa vyama vya wakulima kusimama kutetea haki za wakulima makabwela katika Taifa letu.

By Jamhuri