Ana kwa ana ni tafsiri ya mahojiano baina ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere, na mwandishi wa gazeti, David Martin. Mahojiano haya yalichapishwa katika Gazeti la Kiingereza, New Internationalist, toleo la Mei, 1973. 

David Martin ni Mwingereza na ni mwandishi wa magazeti kwa muda mrefu. Aliwahi kufanya kazi Tanzania kama msaidizi wa mhariri wa magazeti ya Serikali – The Standard (Daily News hivi sasa) na Sunday News. Alishika madaraka hayo baina ya mwaka 1970 na 1971.

New Internationalist ni gazeti linalochapishwa Uingereza katika lugha ya Kiingereza, nalo hujishughulisha zaidi na masuala ya nchi zinazoendelea. Sasa Endelea na mfululizo wa mahojiano hayo…

Swali: Mwongozo umeeleza uhusiano baina ya viongozi wa wanaoongozwa. Mwongozo huo unaeelekea kuwa ni kiini cha migogoro ya kikazi kwa muda wa miaka hii miwili. Siku mbili zilizopita ulisikika ukisema kwamba mtu huru atafanya kazi bila kusimamiwa, bila ya kuhitaji bakora au vishawishi.  Wakati ambapo Tanzania inashughulika na ujenzi wa ujamaa fikra za watu wengi bado ni za kibepari. Je, unafikiri siasa ya watu kufanya kazi bila ya unyapara na hasa bila ya vishawishi inawezekana kweli wakati huu?

Jibu: Kwa mara nyingine tena nafikiri inafaa mtu atofautishe kati ya lengo na namna ya kulifikia lengo lile. Mimi sijui namna nyingine ya kueleza watu wetu aina ya jamii tunayokusudia kuijenga. Sina njia nyingine ya kuelezea. Jamii hiyo haipo lakini ni lazima nieleze, kwani ni lazima tukifahamu kile tunachojaribu kukifanya. Sisi tunajaribu kujikomboa.

Hii ni muhimu sana. Ukombozi kwetu ni jambo lenye maana sana. Tunatoka katika historia ya kutokuwa huru. Iwe historia ya kikabila, ya kikoloni au ya kitumwa. Ukweli ni kwamba tunatoka katika historia ya kutokuwa huru. Ukombozi kwetu ni suala la kufa na kupona. 

Kwa watu wetu, kwa kila mtu; kwangu mimi na kwa mkulima, mfanyakazi kiwandani, mwalimu wa shule na watawala – kwetu sisi sote ukombozi ni maisha. Sijui namna nyingine ya kuwaambia watu wetu – “mtu aliye huru anafanya kazi, atajenga nyumba yake, ataijenga, hahitaji kusukumwa ili ajenge nyumba yake, atajiendeleza mwenyewe.”

Lakini unaponiuliza je, mambo haya yanawezekana leo? Ninasema, hapana. Hatuna jamii ya aina hiyo, tunatoka katika historia ya kutokuwa huru. Sasa nifanyeje? Niikubali tu hii historia ya kutokuwa huru kana kwamba ni ya lazima ambayo hatuwezi kuibadili, historia isiyoepukika? Au niseme ikiwa ni fikra za kitumwa, basi na tuziendeleze fikra hizi hizi za kitumwa?

Ni kweli tunao hapa watu ambao wanataka kuwanyonya wenzao – tunafahamu hiyo. Ni kweli tunao watu wasiopenda usawa. Hakuna usawa Tanzania. Mshahara wangu ni mkubwa kuliko wa kima cha chini Tanzania, na hali ya kutokuwa sawa ni hali ya kutokuwa huru na kama hatuko sawa hatuko huru.

Hivi ni kueleza matatizo haya kifalsafa, lakini ni kweli. Lakini maadam baadhi ya watu Tanzania – na hawa ni wachache – wanaishi maisha ya juu zaidi na kumiliki nchi zaidi ya wenzao walio wengi lazima utakuwa na jamii isiyo huru.

Kwa hiyo mfanyakazi mpaka atakaposhuhudia usawa na kukua kwa demokrasia; atazidi kuwa huru na huru wakati akiona usawa huo zaidi. Hivi sasa haupo hapa na ilivyokuwa haupo hapa sasa, tutakuwa jamii inayokusudia kufika kwenye jamii ya watu huru lakini bado ina tatizo la kutokuwa sawa.

Kwa hiyo basi, leo, kesho na keshokutwa tunaweza kujikuta wakati mwingine tukitoa vishawishi na wakati mwingine tukivilaani vishawishi hivyo, lakini, tukivitoa. Tutajiona tukiwapa adhabu wafanyakazi….Ni juzi tu ilipobidi wafanyakazi fulani wafukuzwe.

Kazi ilikuwa ikitendeka vibaya kwa hiyo ilibidi wafanyakazi kadhaa wafukuzwe na baadaye kazi ikaendelea vizuri. Sisi hujikuta tukitenda mambo kama haya. Lakini kumfanya mfanyakazi afukuzwe kazi ili kazi hiyo iende vizuri ni jambo baya sana. 

Tutakilaani kitendo hicho, tutasema ni kibaya lakini mradi hii ndiyo jamii tuliyonayo sasa na siyo ile tunayojaribu kuijenga; tutaona kuwa wakati mwingine itatubidi kutenda vitendo hivi.

Jambo ninalosema ni kuwa hatuna hiari ila tu kueleza jamii tunayotaka kuijenga na kukubali kuwa jamii hiyo haipo sasa kwa hiyo hatuwezi kuishi kana kwamba ipo hivi sasa, walakini tuweke nadhiri kwenda mbele bila kusita kuelekea jamii hiyo, tukiridhisha kidogo iwezekanavyo.

Tuchukue mfano wa migomo. Inasemekana Mwongozo unawafanya wafanyakazi wagome. Ukweli ni kwamba tunaishi katika jamii isiyo na usawa, vipi basi tutategemea wafanyakazi wasigome? Lazima watagoma.

Wafanyakazi watakaa chini na sisi tutawauliza: “Mnaelewa maana ya kugoma?” Wafanyakazi nao watatujibu: “Na ninyi mnaelewa nini maana ya kutokuwa sawa?” 

Ni lazima tuwe na jamii ambayo haya yanakubaliwa ambamo tunahisi kwa lugha nyingine uchungu wa kuzaliwa kwa ujamaa. Hii nitaikubali. Hii tunaikubali, kwa vile hatujidai kwamba tuna jamii ya ujamaa, hatujidai kwamba tuna jamii ya watu sawa. 

Sisi tunasema tu kwamba tumeeleza lengo letu. Hatuna njia mahususi ya kufikia lengo hilo. Lakini tunaporidhisha lazima tufahamu kwamba tumeridhisha.

Swali: Ukweli kwamba nchi nyingi za Kiafrika zimedhamiria kufuata maendeleo ya kibepari unathibitisha kwamba umaskini na mila za Kiafrika pekee havitoshi kuhakikisha ufuatiaji wa siasa ya ujamaa. Vipi basi Tanzania imeweza kukubali na kuanza kuitekeleza misingi ya ujamaa? Unafikiri kama uongozi wa nchi nyingine zote za Kiafrika ungekuwa na nia, nchi zingeweza kufanya hivyo?

Jibu: Ndiyo nafikiri hivyo, na kusema kweli naamini hivyo. Uongozi Afrika ni muhimu. Nafikiri uongozi ni muhimu kila mahali. Sidhani kama tunafanya ujinga wakati TANU inaposisitiza juu ya uongozi. 

Ni jambo muhimu sana. Mambo yanayotokea Afrika yanategemea sana uongozi. Hata tukisemaje, umma bado hauna nguvu. Hata nchini Tanzania umma hauna nguvu. Mapambano ya kidemokrasia yapo ili umma upate nguvu, nguvu kamili, ili umma upate kuzitumia na kuamini kwamba ni halisi.

Hili ni pambano halisi la kidemokrasia. Kwa hiyo uongozi Afrika ni muhimu sana. Nafikiri itakuwa halali kusema kwamba licha ya matatizo ya kweli yaliyopo, jamii ya kijamaa kwa tafsiri halisi ni jamii iliyoendelea.

Ni jambo moja kusema tunataka kujenga jamii ya kijamaa, lakini kwa nchi iliyo maskini kusema kuwa sisi ni jamii ya kijamaa ni kuvuka mipaka. Jamii maskini ina kitu kimoja sawa na jamii ya kibepari,  nacho ni kuwa zote ni jamii zisizo na usawa.  Ni kwa sababu jamii ni maskini, ndiyo maana haina usawa. 

Licha ya sababu za vikwazo vya kikweli vilivyopo, ni kwa kuwa mu watu maskini, na kwa hiyo baadhi yenu ni wajinga na mnatumia njia za kizamani za uzalishaji mali, na kwa hiyo baadhi ya watu wenu hawatatoshelezwa kwa kuwa hamna vya kuwatosha wote.

Licha ya hayo yote, uwezo wa kuchagua lengo unawaangukia viongozi. Uongozi unaweza ukasema tutachukua ile njia ngumu, njia ya kujenga ujamaa.

Chaguo hili halijafanywa na baadhi ya viongozi, lakini mimi ninasema ingawaje wamechukua njia ya kibepari, njia hiyo si rahisi kweli kwao. Siamini kuwa nchi yao inaweza ikajenga Ujerumani nyingine Afrika au Amerika nyingine Afrika au Ujapani nyingine Afrika.

Hii haiwezekani kabisa siku hizi. Ubepari umefika Ujapani kiwango ambacho nchi ya Kiafrika kuwa ya kibepari ni kuwa kikaragosi tu cha kibepari, na si nchi ya kibepari halisi.

180 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!