Dk. Steven Ulimboka

 

*Ni Kamanda Msangi anyeongoza Tume ya kuchunza utekaji ulivyotokea

*Ujumbe wasambazwa kuwa ndiye alimpora simu ya mkononi na ‘wallet’

*Yeye asema amekatishwa tamaa, Professa Museru aeleza alichosikia

Dk. Steven Ulimboka

Askari anayetuhumiwa kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Stephen Ulimboka, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP), Ahmed Msangi, amehojiwa na kuzungumzia kilichotokea kuhusiana na tuhuma kwamba aliambiwa arejeshe simu ya mkononi na pochi ya Dk. Ulimboka.

 

Akizungumza na Jamhuri, ACP Msangi alikiri kwenda katika wodi ya wagonjwa mahututi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa nia ya kumhoji Dk. Ulimboka, ila akaeleza mshangao wake kutokana na habari zilizochapishwa mwishoni mwa wiki kuwa aliambiwa arejeshe pochi na simu ya Dk Ulimboka kwa maana kuwa alivipora walipomteka.

 

Vyombo vya habari mwishoni mwa wiki vilichapisha taarifa bila kutaja jina la askari anayetuhumiwa, lakini pia ukawa unasambazwa ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi ambao ulisema hivi:

“Kamanda Msangi aliyemkamata na kumtesa Dr. Ulimboka yuko katika jopo la kuchunguza nini kilimtokea Dr. Ulimboka. Alipofika kumhoji Dr. Ulimboka alimwambia ‘Nirudishie simu na wallet yangu’. Kamanda Msangi taratibu akaondoka wodini kichwa chini. Kama wewe ni mpenda haki na unapinga ujinga na dhuluma watumie ujumbe huu watu wengi kadri uwezavyo ili wamjue dhalimu aliyeongoza unyama huu,” ulisema ujumbe huo unaosambazwa kupitia simu za mkononi.

Tume ya Jeshi la Polisi iliyoundwa kuchunguza tukio la Dk. Ulimboka kutekwa nyara, kwa mujibu wa Kamanda Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, inaongozwa na Kamanda Msangi.

 

Kamanda Msangi azungumza

 

Jamhuri: Afande umetangazwa kuongoza hii Tume ya Polisi kuchunguza suala la Dk. Ulimboka, lakini taarifa zilisosambaa zinaonyesha Ulimboka alikwambi umerejeshee simu na wallet yake. Unalizungumziaje hili?

Kamanda Msangi: Hata mimi nimesikikia hizi taarifa, na zimenisikitisha mno. Naamini taarifa hizi zina malengo ya ziada. Sio kweli kwamba nilishiriki kumteka Dk. Ulimboka na wala sijawahi kuwa na wazo hilo.

Jamhuri: Ikiwa hukushiriki kumteka iweje wodini akwambie nirudishie simu yangu?

Kamanda Msangi: Kwanza ifahamike mimi huyu Dk. Ulimboka na mwenzake Dk. Deo nimewafahamu siku nyingi sana. Kwa maana hiyo ni mtu anayenifahamu vizuri tu. Kuna upotoshaji wa makusudi umefanywa, ambao mimi nadhani una msukumo wa kisiasa.

Alichosema Dk. Ulimboka nilipozungumza naye, ni kwamba simu moja ilidondoka, nyingine wale watu waliomteka wameichukua pamoja na wallet yake. Hivyo alikuwa ananitajia vitu vilivyopotea. Nilipomuuliza iwapo anakumbuka namba ya simu, aliniambia nikamuulize Dk. Deo. Sasa nashangaa mtu aliyepenyeza uongo huu kwamba alisema mimi ndiye nimempora hivyo vitu sielewi ni nani na ana malengo gani.

Jamhuri: Haya unayasema wewe, hivi unadhani jamii itakuamini kwa kauli hizi haitaonekana unajitetea tu?

Kamanda Msangi: Wakati anazungumza maneno haya, alikuwapo profesa Museru ambaye ni Mkurugenzi wa MOI. Sina cha kuficha kamuulize tu, atakwambia alichosema Dk. Ulimboka. Yupo pia Dk. Deo, huyu ananifahamu na Dk. Ulimboka anasema walikuwa wote wakati anatekwa. Dk. Deo ananifahamu, akaulizwe iwapo mimi ndiye nilimteka Dk. Ulimboka.

Jamhuri: Tuhuma hizi zilianza kusambaa mapema tu Ijumaa. Je, wewe hukuwa na hofu kwenda pale MOI kumhoji Dk. Ulimboka?

Kamanda Msangi: Ndugu yangu, nchi hii ina askari wengi mno. Hivi mimi kwa akili ya kawaida naweza kushiriki kumteka Dk. Ulimboka kisha nikaenda wodini kumhoji? Hata katika akili ya kawaida ya binadamu hilo haliwezekani.

Jamhuri: Hizi tuhuma zilizoelekezwa kwako ni nzito. Wewe ndiye umeteuliwa kuongoza Tume ya Uchunguzi wa tatizo hili. Je, unadhani uchunguzi utakaofanya utaaminiwa na wananchi ukitoa ripoti?

Kamanda Msangi: Mimi ninachokuhakikishia sikushiriki kumteka na sio kweli kwa kila hali. Mambo kama haya yanakatisha tamaa. Kama tunaanza kuzushiana uongo kwa kiwango hiki, nchi hii sijui inaelekea wapi? Kimsingi imenikatisha tamaa mno. Wapo wanaosema nijiuzulu katika Tume hii mimi nasema wakubwa wangu wamenipa kazi hii na watakaloamua nitalipokea.

Hivi wewe gazeti lako likituhumiwa unaacha kuendelea kutafuta habari? Nitaendelea kufanya kazi hii kama nilivyoapa siku nilipohitimu mafunzo kwamba nitalitumikia taifa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu katika kiapo changu cha utii. Na hilo ndilo nitaendelea kufanya. Watu wanapenda kuharibiana maisha tu.

 

Profesa Museru asema alichokisikia

 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, amezungumza na Jamhuri kuhusiana na sakata kwamba Dk. Ulimboka alimweleza Kamanda Msangi arejeshe simu na wallet yake.

Jamhuri: Profesa nimezungumza na Kamanda Msangi juu ya tuhuma zinazomkabili kuwa aliambiwa na Dk. Ulimboka amrejeshee simu na wallet yake, na akakutaja wewe kuwa ulikuwapo wakati wa mazungumzo hayo. Wewe nini ulichokisikia kuhusiana na tuhuma hizi.

Profesa Museru: Mimi ndiye niliyempeleka pale wodini. Ni bwana mzuri tu. Nilim-introduce (nilimtambulisha), akaanza mahojiano. Mimi hilo sikulisikia kwamba ameambiwa arejeshe simu na wallet hilo sikulisikia.

Jamhuri: Kuna habari kuwa Kamanda Msangi, baada ya kuambiwa kauli hiyo alitoweka wodini bila kuaga akikwepa kipigo kama ilivyomtokea askari mwenzake siku mbili kabla. Je, unalizungumziaje hilo profesa?

Profesa Museru: Nini? Kwamba alikimbia? Jamani nchi hii inakwenda pabaya. Mimi nilimsindikiza hadi nje ya wodi akapanda gari lake na kurejea ofisini kwake, sasa hilo la kukimbia limetokea wapi? Jamani ehee, mimi niseme katika hali kama hii sintofahamu zipo nyingi. Ni vyema kuchuja taarifa tunazozipata.

 

Daktari aisisitiza polisi wanahusika

 

Gazeti la Jamhuri lilichukua jukumu la kumtafuta mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, ambaye kwa sababu za kiusalama alikataa jina lake lisitajwe gazetini, lakini yeye alisisitiza kuwa polisi wanahusika na utekaji huo kwa asilimia 100.

“Hivi unategemea leo Kamanda Msangi kwa akili ya kawaida ya binadamu anaweza akakiri kuwa alishiriki kumteka? Taarifa tulizonazo ni kwamba polisi ndiyo waliomteka Dk. Ulimboka na kumfanyia unyama huu.

“Ndiyo maana tunasema polisi tayari wanatuhumiwa hivyo hawana haki ya kuchunguza suala hili. Tunataka ateuliwe Jaji, na Tume iwe na wajumbe huru wasiofungamana na chama, taasisi au siasa za nchi hii wachunguze kwa kina na kutoa taarifa huru,” alisema Daktari huyo.

Alisema mbinu iliyotumika kumtesa Dk. Ulimboka hutumiwa na majasusi wenye mafunzo ya hali ya juu, ambayo hata majambazi wa kawaida hawawezi kuzifahamu.

“Unapomg’oa mtu kucha au jino bila kumpiga ganzi, unashitua mishipa ya fahamu kumfanya anayeteswa afahamu kuwa kinachofuatia dhahiri ni kifo na hivyo kulazimika kusema ukweli wote anaojua juu ya suala analohojiwa. Mtu akiishang’olewa jino au kucha na asiseme chochote, basi unajua fika kuwa hakuna anachokifahamu zaidi ya alichokisema.

“Hii inatokana na nini? Hicho kinatokana na ukweli kwamba baada ya kung’olewa kimojawapo kati ya hivyo, kinachofuata ni kupoteza fahamu. Sekundi chache kabla ya kupoteza fahamu nati za mishipa ya fahamu huwa zinafunguka na kusema kila kilicho cha kweli bila wewe unayeteswa kujua. Ndiyo maana nasema vyombo vya dola ndivyo vimehusika. Haya ni mateso ya kitaalam,” alisema daktari huyo.

Rais wa Chama cha Madaktri Tanzania, Dk. Namala Mkopi, alipopigiwa simu na Jamhuri kueleza chochote anachokifahamu katika sakata hili, alipokea simu akasikiliza kisha akakata bila kujibu na hata alipopigiwa simu tena hakutaka kuipokea tena.

 

Dk. Ulimboka apelekwa nje matibabu

 

Madaktari inaelezwa kuwa wameamua kumpeleka Dk. Ulimboka katika matibabu nchini Idia, ingawa kwa sababu walizosema ni za kiusalama hawakutaka kutaja ni hospitali ipi aliyopelekwa.

Jumanne wiki iliyopita, Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiofahamika hadi sasa na kupigwa, akang’olewa meno mawili na kucha mbili, kisha akatupwa katika msikiti wa Mabwepande baada ya kuwa ameteswa kupita kiasi.

Dk. Ulimboka baada ya kuokotwa na wasamalia wema, alikaririwa na Radio Clouds akisema kuwa walipokuwa Kinondoni, ndiko alikotekwa usiku wa saa 5:30.

“Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka),” alieleza na kuongeza.

“Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba.”

 

Wananchi wataka uchunguzi huru

 

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Jamhuri, huku wakionyesha hofu ya kutaja majina yao, walilituhumu jeshi la polisi kuwa linahusika moja kwa moja na tukio hili hivyo wakuu wa jeshi hilo wawajibike kuhakikisha ukweli unapatikana.

“Ndugu yangu nawahurumia nyie wenye kutafuta habari hizi. Mnafanya kazi ya hatari. Tutazidi kuwaombea tu, muishi milele na Mungu awalinde. Hivi leo kwa mfano unaweza kwenda kumhoji Msangi kuwa unatuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka? Ukitoka hapo anatuma vijana wake nao wanakuteka na wewe pia.

“Naamini polisi walihusika kwa kiwango kikubwa na hivyo hawapaswi kushiriki uchunguzi huu. Hawa wanapaswa kupanda kizimbani kujitetea hivyo ni makosa kushiriki uchunguzi wao,” alisema Mkazi wa Dar es Salaam.

Mwananchi mwingine alisema chimbuko la mgogoro wa madaktari liko wazi. “Hawa wanadai mishahara mizuri na marupurupu sawa na wanavyopata wabunge wasiofanya kazi yoyote. Leo unadhani serikali inaona imeshikwa pabaya itawaacha waendelee kutamba tu? Thubutu. Kimsingi polisi wametumiwa. Hao waliowatumia ndiyo tunataka uchunguzi huru utueleze ni kina nani na kwa nia ipi,” alisema Mkazi wa Arusha kwa njia ya simu.

Hadi sasa madaktari katika hospitali za umma wamegoma kuendelea na kazi kutokana na mgogoro wa malipo kati yao na serikali na hivi karibuni mgogoro huo umeshika kasi baada ya Dk. Ulimboka kutekwa na kuumizwa vibaya.

 


 

By Jamhuri