Andres Iniesta Atandika Daluga Barcelona

Andres Iniesta amekamilisha huduma yake ya kuichezea Barcelona katika mechi ambayo Barcelona imewaadhibu Real Sociedad wakati wa mechi za mwisho za La Liga.

Iniesta ameagwa kishujaa kwani mashabiki waliunda maandishi ya kumuaga, uwanja ukawashwa taa maalumu kwa ajili yake na akajitokeza machozi yakimtoka akasema, nilifika hapa nikiwa mtoto sasa ninaondoka nikiwa mwanaume, nitawaweka katika moyo wangu milele.

Sherehe za kumuaga zimefana na kuwaacha hata wachezaji wenzake akiwemo Messi wakibubujikwa na machozi huku mashabiki wakiwasha taa za Simu zao na vifaa vingine katika Giza la Uwanja ili kuonesha heshima kwa mchezaji huyo. Wachezaji wote walivalia Jezi namba nane yenye jina la Iniesta.

Mashabiki walijiunga pamoja kuunda neno INFINIT INIESTA yaani INIESTA MILELE, naye alipopewa kipaza sauti amesema, “asante kwa wachezaji wenzangu, kila mmoja. Nitawakumbuka kila mmoja wenu. Na asante sana mashabiki, kwa mapenzi yenu, kila kitu mlichonifanyia tangu nilipofika hapa nikiwa mvulana mdogo. Ninaondoka nikiwa mwanaume. Nitawaweka moyoni mwangu milele”

Iniesta mwenye miaka 34 amekaa Barcelona kwa miaka 22 na kutwaa mataji makubwa 22 katika miaka 16 aliyochezea Timu ya wakubwa kwani alianzia katika timu ya watoto klabuni hapo.