Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) inamsubiri mwendesha baiskeli wa Marekani aliyepatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini, Lance Armstrong, arejeshe medali ya shaba aliyoshinda kwenye mashindano ya Olimpiki ya mjini Sydney, mwaka 2000, amesema Mkuu wa Tume ya Sheria ya IOC.

Kamati hiyo ilimwandikia Armstrong barua Januari, mwaka huu kumtaka arejeshe medali hiyo, ingawa kuna taarifa kuwa mwendesha baiskeli huyo alikiri makosa yake na kwamba kilichobaki ni kutimiza ahadi yake ya kurudisha medali kwa IOC.

 

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ilichelewesha kumuadhibu Armstrong hadi shirika linaloongoza mchezo wa mashindano ya baiskeli (International Cycling Union-UCI) lilipoidhinisha hatua ya Armstrong kuchukuliwa hatua baada kipindi cha wiki tatu, ambapo mtuhumiwa alikuwa na fursa ya kukata rufaa.

 

Kilichofuata ni hatua ya kumnyang’anya Armstrong medali zote saba alizoshinda kwenye mashindano ya mbio za nchini Ufaransa, maarufu kama Tour de France na kupigwa marufuku asishiriki tena mashindano mengine maishani mwake. Haya yalifuatia ushahidi wa shirika la Marekani linalopambana na matumizi ya dawa za kuongezea nguvu mwilini (USADA).

 

Baada ya ubishi mkali, marafiki wa Armstrong walitoa ushahidi uliombana yeye na baadhi ya washirika wake kuwa ni kweli alitumia dawa za kuongeza nguvu mwilini.

By Jamhuri