“Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa taifa moja linategemea misaada na mikopo ya taifa jingine kwa maendeleo yake. Hata kama pangetokea taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazozihitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo, isingekuwa sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu.”

Nimenukuu maneno hayo kutoka kitabu Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea (Uk. 19). Hata kama Watanzania tumelikataa na kulitupilia mbali Azimio hilo, ukweli bado upo pale pale kuwa maneno yake bado kwetu ni falsafa makini na jadidi.

Ukweli ni ukweli hauna sifa ya woga wala unafiki. Una sifa ya ujasiri na haki. Hata kama utauficha ndani ya mkwiji kama pesa au utauzika kaburini kama maiti, iko siku utajichomoza hadharani ubainishe kilichomo kwenye mkwiji au kaburini.

Ni miaka 49 sasa (1967-2016) tangu Azimio la Arusha lilipotuelimisha na kututanabahisha kuhusu misaada na mikopo inavyoweza kuhatarisha Uhuru wetu. Hakuna nchi hata moja duniani ambayo iko tayari kutupa misaada au mikopo kwa kiasi cha kuiwezesha nchi yetu kutimiza shabaha zake zote za maendeleo.

Hakuna serikali duniani yenye uwezo wa fedha kuweza kutoa misaada na mikopo kwa kila nchi yenye dhiki. Fedha ambayo nchi zenye neema hutoa huwa kwa wema wao, au hiari yao au kwa manufaa yao wenyewe.

Ni dhahiri utaratibu kama huo unauza na unadhalilisha utu na uhuru wa watu wanaopokea kitu msaada au mkopo. Tambua, kujitawala kwa kweli ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa taifa moja linategemea misaada na mikopo ya taifa jingine kwa maendeleo yake.

Tangu wiki iliyopita falsafa ya Azimio la Arusha imejichomoza na kutudhihirishia kuwa maendeleo ya nchi hayaletwi na misaada au mikopo kutoka nchi tajiri au yenye neema pale taifa la Marekani lilipotangaza na kukata misaada yake kwa taifa la Tanzania, ambalo sehemu ya mipango yake ya maendeleo ni tegemezi kwa mataifa mengine yenye neema.

Hivi sasa kila pembe ya nchi yetu  awe mkulima, mfanyakazi, mfanyabiashara, mwanasiasa au msomi, mke kwa mume, kijana kwa mzee – wote wanazungumzia shuo lililobwagwa la kukatwa msaada wa fedha kwa Serikali ya Tanzania na taifa kubwa duniani lenye nguvu kiuchumi na kiulinzi la Marekani.

Wapo baadhi ya watu wanafurahia uamuzi huo na kuimba eti tumeyataka yatupate kwa kutofuata masharti ya ‘Mbabe’.Wengine wanashangaa na kusikitika huku wakinena wananchi wataumia kwa kukosa huduma muhimu kama maji, afya na barabara.

Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto la Milenia (MCC) limefuta kuipa Serikali ya Tanzania msaada wa dola milioni 472.8 za Marekani zenye thamani ya shilingi trilioni moja hivi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika awamu ya pili ya mkataba wa Shirika hilo.

Sababu zinazoelezwa mosi, Tanzania imeshindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka jana. Pili, Shirika hilo lilihitaji kupata uthibitisho kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao kutumika kukwaza uhuru wa kujieleza na kuwakamata watu kipindi cha mchakato wa uchaguzi huo.

Wahenga wamesema kamba hukatikia pabovu. Si bure wana lao jambo. Nimetanguliza methali hizo uzitafakari kabla ya kueleza hasa nini kilichowakasirisha wababe hawa wa dunia! Kumbuka, nia na hamu ya kuinyima misaada Tanzania ilianza kabla ya uchaguzi huo wanaoutaja. Maelezo subiri wiki ijayo.

Napenda kusema Tanzania ni nchi huru na ina uwezo wa kuamua mambo yake ya msingi kwa mujibu wa mila, tamaduni na demokrasia ya kweli iliyojiwekea. Aidha, msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano unampa Marekani jaka moyo na hasa pale anapoona vitamu vyapelekwa barazani na vichungu vyabakizwa uwani.

 

>>ITAENDELEA>>

By Jamhuri