Moyo wa binadamu uwanja wa mapambano

Wiki iliyopita, JAMHURI imefanya mahojiano maamulu na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebins Nzigilwa, ambaye ametoa mtazamo na ushauri wake kuhusu matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi.

Yafuatayo ndiyo mahojiano yenyewe:

Swali: Hivi sasa nchi yetu inaandamwa na matatizo mengi ya kutisha yakiwamo mauaji ya viongozi wa dini, chuki za kisiasa, ushirikina na wananchi kujichukulia sheria mkononi. Je, unafikiri chanzo cha haya ni nini hasa?


Jibu: Chanzo ni uasi wa mwanadamu dhidi ya muongozo wa Mwenyezi Mungu, utii wa binadamu katika muongozo wa shetani na ubinafsi wa hali ya juu wa baadhi ya watu kukandamizi zaidi haki za wengine.

Swali: Unadhani serikali yetu inachangia uwepo wa matatizo nchini? Kama jibu ni ndio, inachangia kwa namna gani?


Jibu: Pengine upo uwezekano kwamba baadhi ya watu katika serikali wameshindwa kutekeleza majukumu yao. Ni udhaifu katika kusimamia sheria na taratibu.


Swali: Je, kuongezeka kwa maovu nchini ni ishara ya viongozi wa dini kushindwa kazi ya kuhubiri Neno la Mungu, amani na upendo katika jamii?


Jibu: Siyo kwamba viongozi wa dini wameshindwa kazi yao, isipokuwa mwanadamu amekaidi kama Adam na Eva walivyomkaidi Mungu.


Moyo wa binadamu ni uwanja wa mapambano kati ya sauti mbili zinazopingana; yaani ile inayoelekeza kutenda mema kwa upande wa Mungu, na ile ya ibilisi inayoelekeza kutenda maovu.


Ni kweli kazi ya viongozi wa dini ni kuhubiri mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu, lakini mwenye jukumu la kufuata mafundisho na maelekezo hayo ni muumini.


Mtu asipotekeleza tunayofundisha hatuna vyombo vya dola vya kumlazimisha ayatekeleze. Kama unaambiwa unakataa utahukumiwa kwa kiburi chako.


Binadamu asijiondolee wajibu wake. Matendo mabaya ya baadhi ya viongozi wa dini yasiwe kisingizio cha mwanadamu kujipunguzia hatia.


Swali: Tunashuhudia siku hizi karibu madehebu yote ya dini yameanzisha na kuendesha miradi ya kiuchumi kama vile shule, vituo vya afya na maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali. Pengine miradi hii inawapunguzia viongozi wa kiroho muda wa kuhubiri Neno la Mungu?


Jibu: Lengo la miradi hii ni kujiongezea uwezo wa kukidhi gharama za shughuli zetu za kiroho badala ya kutegemea kusaidiwa kila kitu. Lakini miradi hii inastahili kusimamiwa na waumini, si viongozi wa dini.

Kazi ya viongozi wa dini ni kupokea ripoti za utekelezaji. Miradi hii inaweza kumpunguzia kiongozi wa dini muda wa kufanya kazi za kiroho pale anapojikita katika kuisimamia.


Swali: Ubadhirifu wa fedha na mali nyingine za umma ni moja ya matatizo yanayochangia kuwanyima Watanzania maendeleo ya kweli. Je, ungependa kuona hatua gani zinachukuliwa dhidi ya viongozi wanaojihusisha na uovu huo?


Jibu: Hili ni suala la kisheria na maadili ya uongozi. Niseme kwa kifupi tu kwamba sheria ichukue mkondo wake.


Swali: Siku hizi tunaona madhehebu mapya ya dini yanaibuka kwa kasi kubwa nchini. Unadhani hali hii inasababishwa na nini hasa Askofu Nzigilwa?


Jibu: Hata mimi nashuhudia hilo lakini sijafanya uchunguzi kujua sababu yake, kwa sasa sitalisemea labda mpaka nitakapojua chanzo.


Swali: Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo watu wachache nchini wanavyozidi kujilimbikizia utajiri mkubwa wa mali, huku walio wengi wakizidi kukabiliwa na umaskini kupindukia. Unaitazamaje taswira hii katika misingi ya kiroho?


Jibu: Neno la Mungu linasema uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu [mali] anavyomiliki. Hata Yesu aliishi duniani katika hali ya kawaida.


Wanaotumia utajiri kujipatia usalama wajue huo ni usalama bandia. Usalama wa kweli ni kuishi kwa amani, kushirikiana na wengine, kusaidiana na kupendana.


Tunaona watu wa maana waliokuwa na utajiri mkubwa kama Sadam Hussein [aliyekuwa Rais wa Iraq] lakini waliishia kukimbilia kujificha mashimoni [ingawa hilo nalo halikuwasaidia].


Swali: Katika kuhitimisha mahojiano haya, ungependa kutumia nafasi hii kutoa wito gani kwa serikali na Watanzania kwa jumla kuhusu masuala ya amani na uchaji wa Mungu?


Jibu: Mwenyezi Mungu alituweka duniani tukae katika hali ya amani na maelewano. Watu wote tuisikie sauti ya Mungu tuikubali, maisha yetu yatakuwa mazuri hapa duniani.


2810 Total Views 15 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!