BABA MZURIWatanzania wamelipokea kwa furaha tamko la Rais John Magufuli kuamua kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATC) lililopotea kwa miaka zaidi ya miaka 16 sasa.

ATC ilianzishwa mwaka 1977 baada ya shirika la ndege la East African Airways (EAA) kuvunjika kutokana na tamaa za baadhi ya viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, akiwemo Mkenya, Charles Njonjo. Njonjo alionyesha wazi nia ya kutaka kulivunja shirika hilo ambalo makao makuu yalikuwa Nairobi, Kenya.

Huduma muhimu za ndege kama karakana kuu ya kuzifanyia ndege matengenezo ilikuwa Nairobi Kenya. Jumuiya ilipovunjwa akina Charles Njonjo walihakikisha ndege muhimu ziko Nairobi siku hiyo na si Dar es Salaam na Entebbe. Wakenya walichukua ndege aina ya Super VC10, B707, DC9 na Fokker friendship. Wafanyakazi wa Kitanzania warudi Tanzania bila kupata haki zao.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baada ya kuona nchi yake haina shirika la ndege la kuhudumia Watanzania akaamua kuanzisha ATC kwa kununua Boeing 737-200 mbili, F27 Fokker friendship nne na Twin otter DHC- 6 tatu.

Nyerere alipeleka vijana nchini Uingereza, Finland, Uholanzi, Australia, India, Ethiopia na Soroti Uganda kwa ajili ya kwenda kufanya mafunzo ya uhandisi na urubani wa ndege hizo kuongezea nguvu kwa wafanyakazi waliotoka East African Airways na wengine waliotoka Jeshi la Anga-JWTZ kuanzisha shirika hilo la Taifa.

ATC iliendelea vizuri katika awamu Kwanza ya Mwalimu Nyerere hadi mwaka 1985 ailipong’atuka na kumwachia mzee Ali Hassan Mwinyi. Shirika lilianza kupoteza mwelekeo miaka ya  tisini.

Kabla ya Rais mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela kutoka gerezani Februari 11, mwaka 1990, Makaburu wa nchini humo walikuwa wamefikia uamuzi wa kudhoofisha maishirika ya ndege ya nchi jirani kwa nia ya wao kubaki wenyewe na Shiria la Ndege la Afrika Kusini na hivyo kutawala anga ya biashara ya ndege kusini nwa Jangwa la Sahara.

Mkakati ulilenga kudhoofisha mashirika ya Zambia Airways, Air Tanzania, Air Botswana, Royal Swazi, Air Zimbabwe na Uganda Airlines. Walilenga baada ya kuua mashirika hayo wafanye biashara kupitia kampuni ya Alliance Air, ambayo walianzisha kama kiini macho kuwachanganya viongozi wetu kuwa ni Shirika la Ndege la Umoja kati ya nchi hizo za kusini na kati ya Afrika na kutoa ndege aina ya B747SP (Special performance).

Ndege hizo ilikuwa wanazitumia wakati wa utawala wa ubaguzi wakiruka kutoka Johannesburg, South Africa kueleka Ulaya  na Marekeni bila ya kutua katika nchi yoyote ya Kiafrika kutokana na vikwazo walivyokua wamewekewa na nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Ndege hizo aina ya B747SP zilikuwa zinatumia mafuta mengi kuliko mizigo inayosafirishwa kuleta faida katika biashara ya ndege hivyo, nchi zilizokubaliana nao zililainishwa ku share hasara hiyo kubwa iliyozingiiza serikali za Tanzania na Uganda mkenge katika biashara hiyo ya kihuni chini ya Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe.

Mpungwe alipewa cheo cha Mwenyekiti wa Bodi ya mashirika ya ndege ya nchi za Kanda ya Kusini mwa Afrika, Zimbabwe na Kenya (Air Zimbabwe na Kenya Airways) walikataa uhuni huo.

Baada ya kununua hisa nyingi za ATC, Makaburu waliiamuru menejimenti ya ATC kupunguza marubani 15 na wahandisi 30 na wafanyakazi wengine, ingawa lengo lao zaidi ilikuwa ni kuondoa wataalamu wazalendo kuifuta ATC katika biashara ya Airline za Afrika.

Makaburu Waliilazimisha memenjiment kuuza ndege za B737 –200 (5H – ATC/5H –MRK) Serengeti na Kilimanjaro kwa makampuni ya Afrika ya Kusini kwa bei ya kutupa. Kila ndege moja haikuzidi dola milioni tano. Hapo ndipo walipomaliza mipango yao kuiua ATC na kuanza kufanya kama wanavyotaka. Wakaamua kuleta ndege zao ndogo za ndani, wakaiondoa alama ya Twiga kama alama ya Air Tanzania na kuweka bendera ya Afrika Kusini.

Njia zote za Air Tanzania wakawa wanazitumia kwa faida yao na baadhi ya maafisa wa serikali yetu wakishirikiana nao kulihujumu shirika letu katika eneo la anga. Walipoona wametimiza malengo yao ya kuiuwa ATC wakaamua kuachana nayo na kurudi kwao Afrika Kusini. Lakini shirika lao la ndege South African airways waliendelea kufanya shughuli zao za kibiashara kama kawaida wakiendelea kuruka kutoka Dar/Johannesburg.

Precision Air, shirika la wazalendo, baada ya kuona kuwa haina mshindani katika biashara ya ndege ikaongeza idadi ya ndege na kuongeza wafanyakazi ambao wengi wao walitokea ATC. Hawa ni wataalamu wa ndege wazoefu (Experienced pilots and Engineers) kwa hiyo hawakuwa na gharama ya mafunzo kwa kuwa Serikali ya Tanzania tayari ilishawagharamia kwa lengo la kulitumikia shirika la Taifa ATC.

Baada ya msukosuko huo mkubwa kwa ATC wajanja wakaanza kunyofoa vitega uchumi vya ATC kama Cargo handling, catering, passengers handling, galileo, hangar la Kia – Kilimanjaro Air craft maintenance facilities (KIMAFA) likafanywa  kuwa jumba la kuhifadhia maua badala ya kutengenezea ndege.

Viongozi wengi walioteuliwa kuliongoza shirika la ndege ATC na wao pia walichangia kulidhoofisha shirika  hilo kwa kutokuwa na vision ya uongozi wa airline na kuchelewa kutoa uamuzi wa kuibinafsisha katika  mashirika ya maana kama KLM, Lufthansa, British Airways, Delta Airlines, Trans World Airlines na si South African Airways ya makaburu.

Ni aibu kwa taifa kubwa kama Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kutokuwa na Shirika la ndege lenye kueleweka badala yake nchi ndogo kama Rwanda, Seychelles, Ethiopia, Sudan, Kenya na Mauritius wanakuwa na mashirika kubwa ya ndege kuliko sisi na tunaona sawa tu.

Ni aibu kwa taifa letu nchi hizo zinatushangaa. Shirika la Ndege la Taifa mbali na biashara, huipa heshima nchi mbele ya mataifa mengine kwa kuwa hupeperusha bendera ya Taifa husika katika miji mikubwa ya mataifa mengine.

Hapa nyumbani katika Uwanja wetu wa Kimataifa Julius Nyerere International Airport ndege au bendera tunazoziona ni za kigeni kama vile Emirates Airlines, Ethiopian Airlines, Qatar Airways, Turkey Airways, Kenya Airways, Rwanda Air, KLM, South African Airways, Fly Dubai, Indian Airlines, Egypt Air, Oman Air na sasa El-Ithad ya Abu Dhabi.

Air Tanzania imewafanyia nini Watanzania? Serikali ya Tanzania imeitumia kwa masuala mangapi ya kitaifa ambayo ni nyeti kama vile kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichotokea Saint Thomas Hospital – London, 1999? Usikose sehemu ya pili ya makala hii wiki ijayo.

 

Mwandishi wa Makala hii wanajeshi mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania  0785 042078.

By Jamhuri