Air Tanzania ndilo  Shirika  la  Ndege  la  Taifa  (national flag  carrier)  ambalo linastahili  kumiliki  huduma  zote  muhimu  katika  Viwanja vya Ndege  vyote vya  Tanzania, lakini hali iko kinyume.

Huduma zinazotolewa katika viwanja vya ndege ni pamoja na miziggo (Cargo  handling), wasafiri (Passengers handling), huduma ya chakula (Catering), mfumo wa kukata tiketi (Booking  system) na kazi nyingine.

ATC si  kampuni  binafsi  kama  ilivyo kwa Swissport, Precision  Air, Fast  Jet na mawakala  wengine. Utaratibu  uliopo kwa sasa  ni Watanzania wachache wenye uchu wa kujinufaisha  binafsi (ufisadi) na si  kulinufaisha Taifa.

Naomba kuchukua fursa hii kumuomba Rais John Pombe Magufuli, kuwa mikataba  yote iliyopo pale Uwanja wa Ndege na ndani ya ATC ipitiwe  upya  na  kuangaliwa kwa makini taifa linafaidika nini na mikataba hiyo.

Kwa kiasi kikubwa mikataba hiyo imeidhoofisha ATC  kwa faida ya makaburu wa South African Airways  ya  Afrika  Kusini. Kampuni ya Precision  Air  iliamua  kushirikiana na Kenya  Airways badala  ya  kushirikiana  na Air  Tanzania, nayo yakaifika.

Mambo  yote  haya  yamefanyika mbele ya viongozi  wa serikali bila kukemewa na hasa Wizara  ya Mawasiliano na Uchukuzi ambayo ni Wizara  mama.

 

Historia ya Swissport

DAHACO Ilianzishwa Mwaka 1985 October chini ya uongozi wa meneja mkuu Lindgard likiwa na mgawanyo wa hisa na nchi za Scandinavia, SAS na Air Tanzania.

Baada  ya miaka kadhaa menejimenti kuu ilihamishwa na kuletwa utawala mpya. Baadaye ilitokea zabuni Zanzibar ya Handling, ambayo DAHACO ilishinda na kufanya kazi Zanzibar makao makuu yakiwa Dar es Salaam. Miaka kadhaa baada ya zabuni hiyo DAHACO walinyanga’nywa na kupewa kampuni ya ZAT kutoa huduma za ndege Zanzibar.

 Katika mabadiliko hayo kati ya miaka 1990 na kuendelea DAHACO ilipata meneja mpya raia wa Sweden, kwa jina maarufu SANSITROM, aliyemwajiri Gaudence Temu kuwa mwanasheria wa kampuni kwa kipindi chote.

 Hatimaye uongozi wa Wazungu ulitolewa na kuwaacha wazawa wakati huo Temu akiwa mwanasheria akapewa madaraka kuwa Mkurugenzi Mkuu baada ya kwenda kusoma mambo ya Airlines.

 Ulizuka uadui kutokana na zabuni za kununua vifaa vya CARGO HANDLING. Temu alikuwa anataka ashirikishwe katika ununuzi wakati si mtaalamu wa vifaa hivyo.  Vifaa vilivyoleta sintofahamu ni pamoja na:- 1. Ground Power Units (2) High Loader (3) Tow Tractor (4) Dollies (5) Baggage Trollies (6) . Tow Bars.

 Shirika kama British Airways wana idadi ya ndege zipatazo 2500 kwa siku. BA ndiyo hutafuta wakala wa shughuli zote za viwanja vya ndege nchini Uingereza.

 Hivyo gharama zote za huduma za viwanja vya ndege nchini humo hutolewa na British Airways. Hiki ni chanzo kikuu cha mapato na chimbuko la unafuu wa gharama ya mizigo kwa Waingereza. ATC ilitakiwa kuwa kama BA kuepusha malipo yasiyo na kichwa wala miguu kwenda kwa wakala kama Swissport na hivyo kupata faida. Mawakala katika viwanja vya ndege waangaliwe upya.

 Zipo taarifa kuwa chini ya ungozi wa Awamu ya Tatu wa Rais Benjamin Mkapa, mkewe mama Anna Mkapa na Bassil Mramba akiwa Waziri wa Fedha; na mzee wengine, walichangia kuidhoofisha ATC. Hawa ndiyo wakuu waliokuwa na hisa kwenye Precision Air hivyo, kufanikisha kuididimiza ATC kutofanya kazi kwa maslahi ya taifa kutokana na masilahi binafsi.

 Kati ya miaka 1999 – 2000 DAHACO iliuzwa kwa SWISSPORT, ambayo makao yake yalikuwa NAIROBI, ikifanya HANDLING  katika viwanja vya Kenya.

Baada ya uongozi wa uanzilishi wa DAHACO kuondoka, kiongozi mkuu wa wakati huo Lindergard, raia wa Sweeden aliomba na kuishauri Board ya DAHACO kuwa kitengo cha Handling kirudishwe AIR Tanzania kwa kuwa ATC ndiyo iliyotakiwa kutoa huduma hiyo katika viwanja vyote hapa nchini.

Wazo hilo lilikataliwa na viongozi wa DAHACO kwa maslahi yao binafsi.

CARGO handling (ATC) ingepata mapato. Katika viwanja vya ndege kuna huduma tofauti. ATC kama ingepata kitengo hiki ingeweza kujiendesha na kulipa mishahara ya watumishi pasipo tabu.

Vyanzo halisi vya mapato yasiyotegemea gharama kubwa za uzalishaji ni pamoja na malipo ya maegesho, maduka, tozo kwa wasafiri na huduma nyingine nyingi tu.

Kwa mfano ATC wangechukua SWISSPORT basi gharama za Handling zote ambazo ndege zinazokuja Dar ATC ingepata fedha za kigeni nyingi ukizingatia kuwa ndege za abiria ziko nyingi na zinalipa kila mwezi kwa Swissport, malipo yanayowafanya kutangaza faida kila mwaka. Kwenye kitengo hicho kuna gharama za usafi ndani ya ndege. Upakiaji na upakuaji wa mizigo vyote vikiwa vyanzo vya mapato. ATC ingepata mapato mengi ambayo yangelifanya shirika kujiendesha bila shida.

 Natoa ushauri kuwa Swissport mkataba wake uvunjwe na huduma zote zirudishwe kwa ATC ambalo ndilo Shirika la Ndege la Taifa, lenye uhalali wa kumiliki huduma hizo zinazofanywa na Swissport.

 ATC ilibanwa na watu wachache kwa maslahi yao na kutoa upendeleo kwa kampuni binafsi. Hii ililifanya shirika kufilisika na kuachisha kazi wafanyakazi wengi bila kupata mafao yanayostahili.

 Kwa ufasaha zaidi naomba atafutwe ndugu Willson Ndossy. Huyu anaweza kuwa msaada mkubwa kwa serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu mwenendo mzima wa utoaji zabuni katika viwanja vya ndege.

 Mashirika ya ndege duniani hayatoi huduma za viwanja vya ndege kwa mawakala. Bali hufanywa na Shirika la Ndege la Taifa kama ATC, hivyo viongozi waliofanya mikataba hiyo walifanya kwa maslahi binafsi na si kwa maslahi ya taifa. Serikali ya Awamu ya Tano ihakikishe Air Tanzania inarudishiwa vitengo hivyo kwa ajili ya kujiimarisha katika ushindani wa biashara ya ndege hapa duniani.

By Jamhuri