Wiki iliyopita, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, aliwasilisha bungeni Ripoti ya Mwaka ya CAG ya mwaka ulioishia Juni 30, 2015. Kama ilivyo ada, ripoti hiyo imesheheni mambo mengi. JAMHURI inawaletea wasomaji baadhi ya mambo muhimu yaliyo kwenye ripoti hiyo bila kuyahariri. ENDELEA…

 Tathmini ya Machakato wa Ubinasfishaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)

 Mnamo mwaka 2002 kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya ubinafsishaji na uchumi huria, Serikali ya Tanzania iliweka asilimia 49 ya hisa zake kwenye Shirika kwa wakati huo likiitwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na kukabidhi usimamizi wa hisa hizo kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini. Baada ya hapo Kampuni ya Ndege Tanzania ilianzishwa chini ya sheria ya makampuni namba 212 kama kampuni binafsi.

Wakati wa ubinafsishaji, Shirika la Ndege lilikuwa na ndege mbili ambazo ni B737-200 iliyokuwa ikimilikiwa na shirika hilo na B737- 300 ikiwa imekodishwa chini ya mkataba wa matengenezo kuwa juu ya anayekodi. Zoezi la ubinafsishaji lilipelekea upunguzaji wa rasilimali watu kutoka nguvu kazi ya wafanyakazi 493 mpaka kufikia 251 ili kuhakikisha muundo mpya wa uendeshaji unaanza kampuni ikiwa na rekodi safi za fedha. Serikali ya Tanzania ilichukuwa madeni yote ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kwa kuyaweka madeni hayo chini ya Shirika Hodhi la Ndege (ATC) linalomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali. Shirika Hodhi la Ndege liliundwa kwa ajili ya kuchukuwa rasilimali zote za Shirika la Ndege Tanzania ambazo hazihusiani moja kwa moja na biashara ya kampuni pamoja na madeni yake yote ambayo hayajalipwa.

Ukaguzi umegundua kuwa, ingawa iliaminika kwamba mabadiliko haya ya kimuundo yangeleta ufanisi na kuongeza tija ndani ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kama ilivyothibitika na kuonekana katika baadhi ya mashirika machache yaliyobinafsishwa, matokeo yalikuwa ni kinyume na matarajio.

 Matokeo ya ubinafsishaji huu yalipelekea kampuni kupata hasara kupitia:

 Kuongezeka kwa gharama za usimamizi kwa njia ya ada ya usimamizi iliyotozwa na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA;

 Kuongezeka kwa gharama za matengenezo zinazolipwa kwa Kampuni ya Ufundi ya Afrika Kusini (SAT), ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) ;

 

 Kuongezeka kwa gharama za uendeshaji

 Kuwacha kazi kwa wafanyakazi wengi tegemezi wenye uwezo hasa wahandisi ; na

 Gharama kubwa za kukodi zilizolipwa kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa ajili ya ndege zilizokodishwa.

 Kampuni iliendelea kupata hasara mpaka mwaka 2006 Serikali ilipoamua kununua tena hisa kwa asilimia 49 kutoka Shirika la Ndege Afrika Kusini (SAA). Kwa mara nyingine tena Serikali iliendelea kuwa mdau pekee kwenye umiliki wa Shirika la Ndege la Taifa. Wakati huo, Kampuni ya Ndege ya Taifa (ATCL) ilikuwa na mtaji hasi wa thamani ya Shilingi bilioni 6.9.

 Ni dhahiri kwamba ubinafsishaji wa chombo hiki haukuzingatia kwa kina malengo mafupi ya ubinafsishaji na jinsi yanavyohusiana na malengo ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na maendeleo ya mahitaji ya soko ndani ya sekta ya usafiri wa anga.

 Hakukuwa na ushahidi kuwa Serikali ilifanya tathmini yoyote ya awali juu ya manufaa ambayo yangetokana na kuingia ubia kati ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Kampuni ya Ndege ya Afrika Kusini. Tathmini yetu iliyofanywa juu ya matokeo baada ya ubinafsishaji ilibaini kuwa Serikali, kupitia Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) haikufanya uchambuzi wowote wa kina ili kubaini gharama na vikwazo vitakavyopelekea kutofikiwa kwa malengo ya muda mrefu ya kampuni.

 Kutokuwepo kwa Mfumo wa Usimamizi wa Vihatarishi vya Kibiashara Mfumo wa usimamizi wa athari kwa kawaida huhusisisha kanuni za misingi ya utawala bora kwa kutambua kwamba usimamizi wa vihatarishi ni mbinu muhimu katika kufikia madhumuni na malengo ya taasisi.

 Nilibaini kuwa Kampuni haijaanzisha mfumo wa sera ya usimamizi wa viashiria vya hatari za kampuni. Pia nilibaini kuwa hakuna utaratibu wa kutathmini athari zinazoikabili Kampuni. Kampuni bado haijaanzisha majukumu yanayohusiana na usimamizi wa viashiria vya hatari na miundo yake inayojumuisha uundaji wa kamati ya usimamizi wa viashiria vya hatari kwa ajili ya kusimamia utaratibu mzima wa usimamizi wa viashiria vya hatari.

Kukosekana  kwa  mfumo  wa  usimamizi  wa  athari

unaoelezea kwa kina taratibu zote  za mfumo wa athari

zinazoikabili Kampuni  kunaathiri  uwezo wa   Kampuni

kutambua, kuchambua, au kudhibiti kiwango cha kukabiliwa na athari za kiutendaji na kimfumo ndani ya mfumo mzima wa utendaji wa Shirika.

 

Ukodishaji wa Ndege Usiokuwa na Faida

 Ukaguzi umebaini kuwa tarehe 9 Oktoba, 2007, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ilisaini mkataba wa ukodishaji wa ndege (Airbus namba A320-214 yenye usajili namba MSN630) kutoka Kampuni ya Wallis Trading Co. Ltd. Hata hivyo, mkataba wa kukodi haukufuata utaratibu muhimu na rasmi wa uendeshaji wa kampuni.

 Kwa mujibu wa taratibu hizi, Kitengo cha Ufundi ndani ya Kampuni kinawajibika kufanya uchunguzi wa ubora na kupata maelezo yote ya ndege kabla ya kuingia katika makubaliano yoyote ya kukodisha. Kwa upande mwingine, TCAA pia ni inawajibika kuchunguza na kukagua ndege ili kuhakikisha kwamba inaendana na viwango vya sayansi na ufundi wa vyombo vya anga vya kimataifa kabla ya kusajili ndege husika katika nchi.

Nilibaini kuwa vitengo vyote viwili vya ufundi cha Kampuni ya Ndege Tanzania na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania lifanya uchunguzi wao kati ya tarehe 14 na 22 Januari, 2008 wakati mkataba wa kukodi ulikuwa umekwisha kusainiwa. Matokeo ya ukaguzi yalionyesha kuwa ndege haikufikia viwango vinavyohitajika hivyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga ilimpa maelekezo mkodishaji kurekebisha mapungufu yaliyoonekana kabla ya kukabidhi ndege hiyo kwa Kampuni ya Ndege Tanzania. Aidha, nilibaini kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo tarehe 8 Oktoba, 2007 aliishauri Kampuni kupitia barua yake yenye kumbukumbu no.JC/I.30/308/3 lakini ushauri wake haukuzingatiwa wakati mkataba wa kukodi ndege unasainiwa.

 Ili kutimiza matakwa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga kufuatia ukaguzi wao waliofanya, kampuni ya Wallis Trading Co LTD ilifanya matengenezo yaliyoelekezwa mwezi Februari, mwaka 2008. Hata hivyo, Mkodishaji hakukabidhi ndege kwa Kampuni ya Ndege Tanzania mpaka ilipofika mwezi Mei, mwaka 2008 baada tu ya Serikali kutoa barua ya dhamana ya thamani ya Dola za Marekani milioni 60 tarehe 2 Aprili mwaka 2008.

 ATCL ilikuwa ikigharamika kodi ya mwezi ya Dola za Marekani 370,000 kiasi kwamba kati ya Oktoba mwaka 2007 na Mei mwaka 2008 Kampuni ilikuwa ikidaiwa limbikizo la kodi la kiasi cha Dola za Marekani 2,590,000 kabla ya ndege kukabidhiwa rasmi kwa Kampuni ya Ndege Tanzania. Ndege ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita hadi mwezi Novemba mwaka 2008. Ilipofika mwezi Disemba mwaka 2008 ndege ilitupelekwa katika Kampuni ya Ndege ya Mauritius kwa uchunguzi mkubwa wa kiufundi ambapo ilikaa hadi mwezi wa Juni mwaka 2009. Mwezi Julai mwaka 2009 ndege ilihamishiwa kwenye Kampuni ya Ndege ya Ufaransa kwa uchunguzi wa C+12. Makadirio za matengenezo yaliyofanyika yalikuwa Dola za Marekani 593,560 dhidi ya gharama halisi ambapo iliongezeka kufikia Dola za Marekani 3,099,495 baada ya matengenezo ya kina kufanyika. Mmiliki alitoa dhamana ya kuchangia Dola za Marekani 300,000 tu na gharama nyingine kubebwa na Kampuni ya Ndege Tanzania.

 Matengenezo yalikamilika mwezi Oktoba mwaka 2010 lakini ndege haikuweza kurudishwa Tanzania kutokana na Kampuni ya Ndege Tanzania kushindwa kulipa gharama husika. Ndege ilikaa Ufaransa kwa kipindi chote cha mkataba wa kukodi hadi tarehe 17 Oktoba 2011 mpaka mkataba ulipositishwa. Wakati mkataba wa kukodi unasitishwa, gharama za kukodi kwa muda wa miezi 43 ambayo ndege hiyo ilikuwa chini ya matengenezo zilifikia Dola za Marekani 15,910,000. Jumla ya gharama ikijumuishwa na ada ya kila mwezi ya kukodi na gharama nyingine kama vile riba ilifikia Dola za Marekani 42,459,316.

 

Kukosekana kwa Mkakati Mahususi wa Kufufua Shirika

 Mkakati wa kufufua taasisi inayotetereka kiutendaji ni mchakato wa kubadilisha kampuni inayopata hasara kuwa kampuni inayopata faida. Mkakati huo ni wa kiutawala na kimuundo, uliopangwa vizuri. Katika kufufua kampuni na kuiletea mafanikio kwa kufuata mpango huo hatua kwa hatua mpango huo unahitaji muda, uwekezaji na ushiriki wa nguvu kazi yenye ufanisi wa hali ya juu.

Sababu nyingi za kushindwa kwa makampuni mengi, mara nyingi, si za moja kwa moja kama vile: washindani wapya katika soko, ongezeko la bei ya malighafi, na mabadiliko katika mahitaji ya soko. Kwa upande mwingine, mambo yanayosababisha kampuni kutofanikiwa ni kama vile menejimenti kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo; kuwa na maamuzi mabaya ya kifedha na kushindwa kukabiliana au kujua mwelekeo mpya uliopo katika sekta husika. Tathmini ya utendaji wa Shirika inaonyesha kwamba Kampuni ya Ndege Tanzania haina uwezo wa kulipa madeni pamoja na kuwa na nguvu kazi yenye watu wenye umri mkubwa kwenye vitengo muhimu kama vile Kitengo cha Ubora na Usalama, wahandisi wa ndege; marubani; na kuwa na uwezo duni wa rasilimali.

Kampuni ya Ndege Tanzania ina wafanyakazi 231 ambao kati yao 127 (sawa na asilimia 55) ni wafanyakazi wa kudumu; 54 wafanyakazi wa mkataba (ambao ni sawa na asilimia 23); na wafanyakazi 50 (sawa na asilimia 22) ni wenye mkataba wa muda. Kati ya wafanyakazi 127 wa kudumu, 39 (sawa na asilimia 31) wako karibu na umri wa kustaafu (yaani zaidi ya miaka 55). Nilibaini kuwa Idara zina idadi kubwa ya maafisa wenye umri unaokaribia kustaafu. Mfano, Idara ya Ufundi ina Wahandisi watano (5) kati ya wahandisi saba wana umri wa zaidi ya miaka 55.

Tathmini ya orodha ya wafanyakazi wenye vyeo vya juu wa Kampuni ya Ndege Tanzania imebaini kuwa baadhi ya idara zinaongozwa na wafanyakazi ambao hawana ujuzi sahihi kulinganisha na nafasi zao kazini. Kwa mfano, katika Kurugenzi ya Biashara, baadhi ya wafanyakazi wana sifa za chini za kitaaluma ambazo hazilingani na nafasi za kazi walizonazo kwa sasa.

Kampuni ina madeni makubwa kiasi cha kushindwa kukidhi gharama zake za uendeshaji. Kampuni hasa inategemea mgao wa fedha kutoka Wizara mama ambazo hautabiriki. Kampuni inakabiliwa na gharama kubwa za matengenezo; kushindwa kuzingatia kanuni za lazima kama vile Chama cha Usafiri wa Anga wa Kimataifa (IATA) ya Ukaguzi wa Usalama wa Usafiri wa Anga (IOSA), ugumu katika kuendesha mafunzo ya lazima kwa marubani na wafanyakazi wa Idara ya ufundi, ugumu katika kufanya ukarabati wa hanga za kutengenezea ndege (airport hangars) na jengo la makao makuu kwa ajili ya kuongeza

kipato kutokana na kodi na huduma za matengenezo ambazo zingetolewa.

Kuwepo kwa uhaba wa kifedha kunaathiri uendeshaji wa Kampuni na kushindwa kutimiza malengo yake kifedha kwa ajili ya kupata muundo sahihi utakaoiwezesha kampuni kutoa huduma zenye ushindani kwenye sekta ya usafiri wa anga.

Nilibainisha kuwa Menejimenti ya Kampuni ya Ndege Tanzania haijaandaa mkakati wowote wa kuifufua kampuni kutoka kwenye hali yake ya sasa ya kupata hasara na kushindwa kulipa madeni na kuwa kampuni inayopata faida. Mapitio ya Mpango Mkakati wa Kampuni kwa vipindi viwili vya mwaka 2007 -2012 na mwaka 2015- 2020 havionyesha dalili zozote za kuitoa kampuni katika hali yake ya kutokuwa na uwezo wa kulipa madeni.

Kushindwa kupata vyeti muhimu vya usafiri wa anga

 Nimebaini kwamba Kampuni ina uhaba wa vyeti muhimu vya usafiri wa anga vinavyotakiwa. Kwa maelezo ya uongozi, zoezi la haraka na muhimu linalotakiwa kukamilika mapema ni ukaguzi wa usalama wa usafiri wa anga wa Chama cha Usafiri wa Anga wa Kimataifa. Kulingana na taratibu na kanuni za uendeshaji, makampuni yote ya ndege yalitakiwa kufuata taratibu za ukaguzi wa usalama za usafiri wa anga (IOSA) kufikia mwisho wa Disemba mwaka 2008. Hata hivyo kutokana na vikwazo vya uhaba wa fedha, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) halikuweza kulipia gharama ambazo zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 1,000,000 kwa mwaka 2008 ili kuwezesha utekelezaji wa ukaguzi huo.

Pia nilibaini kwamba, kutokana na kutofuata kanuni za usafiri wa anga (IOSA), Kampuni ya Ndege Tanzania ilisimamishwa kuwa mwanacahma wa IATA Disemba mwaka 2008 na kubakia mwanachama wa kupitishia wasafiri tu. Uchunguzi zaidi umebaini kwamba, Kampuni ya Ndege Tanzania haifuati taratibu zinazohitajika za Cheti cha Uendeshaji wa Usafiri wa Anga (AOC). Kampuni inaendeshwa kwa taratibu za uendeshaji wa usafiri wa anga zilizomalizika muda wake toka tarehe 31 Machi mwaka 2010. Ili Kampuni ya Ndege Tanzania ipate Cheti cha Uendeshaji wa Usafiri wa Anga kiasi cha Dola za Marekani 1,400,000 kilitakiwa mwaka 2010. Hii ilikuwa hasa kwa ajili ya kununua kiwango cha chini cha mahitaji ya vipuri ili kuwa na uwezo wa kufanya matengenezo muhimu ya ndege ya shirika aina ya Dash 8; ununuzi wa programu ya matengenezo ya ndege nakuwapatia mafunzo marubani na wahandisi wa ndege ambao Shirika haliwezi kuwapata kutoka wizarani.

Bila kukidhi mahitaji ya vyeti vya usalama wa usafiri wa anga, Shirika linahatarisha usalama wa usafiri kwa ndege zake na kuongeza ugumu kwa Shirika kupanua wigo wa safari zake ili kujikwamua kutoka kwenye hali mbaya ya kifedha ambayo imekuwa ikilikabili kwa muda mrefu sasa.

 

Kuporomoka kwa Hali ya Kifedha ya Shirika

Moja ya changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni uhaba wa fedha. Changamoto ambayo imelikabili Shirika hili kwa miaka mingi sasa. Kutokana na taarifa za fedha ambazo hazijakaguliwa, nimegundua kuwa shirika limekuwa likipata hasara kwa miaka 9 mfululizo.

Sehemu kubwa ya mapato ya Shirika yanatokana na mauzo ya tiketi. Mapato ya Shirika yamekuwa yakishuka mwaka hadi mwaka tangu mwaka 2007. Mfano; Kati ya mwaka 2008 na 2013, mapato ya Shirika yalishuka kwa kiwango kikubwa. Kati ya mwaka 2014 na 2015 mapato ya shirika yaliboreka kwa kiwango fulani kufikia mauzo ya Shilingi bilioni 16.24 kwa mwaka 2014 na Shilingi billioni 15.01 kwa mwaka 2015, ikilinganishwa na wastani wa mauzo ya Shilingi bilioni 4.77 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2013.

Matumizi ya Shirika yamekuwa yakiongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2008 yalifikia kiwango kikubwa kuliko miaka yote cha Shilingi bilioni Mwenendo wa hali ya kifedha wa Shirika la Ndege   Tanzania    (ATCL)

Moja kati ya vikwazo vilivyochangia kuporomoka kwa hali ya kifedha na kutokukopesheka kwa Shirika ni madeni makubwa yaliyopelekea kutokuwa na ufanisi. Mfano, mwaka 2014, Shirika lilikuwa na deni la Shilingi bilioni 140 na baada ya mazungumzo na wadai, deni likapungua hadi kufikia Shilingi bilioni 111.

Mapitio ya mpango mkakati wa Shirika kuwanzia mwaka 2015 mpaka mwaka 2020; mpango na makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2015/2016; pamoja na makisio ya fedha yaliyoandaliwa na Shirika kama mojawapo ya masharti ya kupata mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 20 yameonesha kuwa kulikuwa na tofauti kati ya taarifa hizo ukilinganisha na mpango mkakati unaotekelezwa na shirika katika kufikia malengo yake. Mpango mkakati wa shirika wa 2015/2020 unaainisha kwamba ili Shirika liwe na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake, linahitaji kununua ndege mpya au karibu na mpya ambazo ni Bombadier DHC8Q400 moja kwa gharama ya Dola za Marekani 24,500,000 na Boeing B737NG kwa gharama ya Dola za Marekani 80,000,000.

Kinyume na mpango mkakati huo, baada ya majadiliano na uongozi wa Shirika pamoja na mapitio ya andiko la mkopo, ilibainika kuwa Shirika limedhamiria kununua ndege nne zilizotumika ambazo ni Boing 737-500B mbili kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 4 kwa kila moja na CRJ200 mbili kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 3 kwa kila moja. Ndege hizi zitanunuliwa kwa kutumia fedha za mkopo wa Dola za Marekani milioni 20 unaotarajiwa kupatikana kutoka benki ya Benki ya Uwekezaji Tanzania.

Hakukuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa Shirika lilifanya tathmini na uchambuzi wa ndani ili kutambua athari za kubadilisha malengo kati ya yale yaliyoainishwa katika taarifa hizo mbili.

Kutofautiana kwa taarifa hizo mbili kunaweza kupelekea mkanganyiko ndani ya shirika katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Inatia shaka kutokana na mkwamo wa hali ya kifedha unalolikumba Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) tangu mwaka 2007. Hii inaashiria kuwa kuna udhaifu ndani ya Shirika katika kuweka mpango mkakati utakaopanua biashara yake ili liweze kufufuka kutoka kwenye mkwamo huo wa kifedha.

 

Mapendekezo

i. Serikali inashauriwa kufanya upembuzi yakinifu kati ya faida na hasara zinazoweza kupatikana kutokana na shughuli zozote za kibiashara zinanazohusisha ubinafsishaji pamoja na ushirikiano na sekta binafsi kabla ya kuingia mkataba wowote na sekta binafsi ili kuhakikisha maslahi ya umma yanalindwa.

 ii. Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inatakiwa kutengeneza mfumo, sera na mkakati wa usimamizi wa athari zinazoweza kujitokeza. Pia inapaswa kuwanzisha na kuendeleza regista ya vihatarishi ikiwa ni pamoja na mapitio ya kila mwaka ili kuimarisha muundo wa uongozi unaoshughulikia vihatarishi. Pia, uongozi wa Shirika unashauriwa kuwandaa mpango wa utelelezaji ambao utaboresha utendaji kazi wa Shirika na kuwa wa kisasa zaidi.

 iii. Kampuni ya Ndege Tanzania itengeneze mkakati utakaoliwezesha kurudi katika hali nzuri ya kifedha kwa kufanya tathmini ya kina kubaini sababu na matatizo yaliyopelekea kuwa na matatizo ya hali ya kifedha iliyopo, pamoja na kuboresha mifumo na namna ya kuendesha biashara hiyo ili kuwa na Shirika jipya lenye ufanisi na kujiendesha kwa faida.

 iv. Kampuni ya Ndege Tanzania iweke utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi au kuwajiri watumishi wapya wenye sifa stahiki pamoja na kuwa na mpango wa kurithishana ujuzi kwa nafasi muhimu za uongozi wa Shirika ili kuwa na watumishi wasomi, wazoefu, waliohamasika na wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani katika soko linalokuwa kwa kasi la usafiri wa anga.

 v. Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) linatakiwa kupata vyeti vyote kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kimataifa (IATA) pamoja na ukaguzi wa usalama wa usafiri wa anga. Kulingana na taratibu na kanuni za uendeshaji wa makampuni yote ya ndege kufuata taratibu za usalama za usafiri wa anga.

 vi. Ninapendekeza kuna ulazima Serikali iangalie changamoto zinazolikabili Shirika na kutafuta njia nzuri za kufanyia mageuzi Shirika la Ndege la Taifa na kuweka mfumo ambao utaliwezesha shirika kutoa huduma za kiushindani na pia kujiendesha kwa faida.

 vii. Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) inatakiwa kufanya Tathmini ya kina na uchambuzi ili kutambua athari za kubadilisha malengo kati ya yale yaliyoainishwa kwenye mpango mkakati wa mwaka 2015/2020 na kwenye andiko la mkopo kabla ya kuchukuwa mkopo huo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania ili kununua ndege.

2134 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!