Umiliki wa Ziwa Kitangiri unafanana na mgogoro uliopo sasa wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa. Wakati mgogoro wa Malawi ukipewa kipaumbele, huu wa Ziwa Kitangiri linalotenganisha wilaya za Meatu na Iramba haujapewa msukumo wa kutosha.

Katika Mkutano wa Nane wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, Mbunge wa Meatu, Meshack Opulukwa, aliibua suala hilo la mgogoro kupitia swali lake na. 154.

Meshack Opulukwa (Chadema) aliuliza:-

Ziwa Kitangiri linapakana na wlaya za Meatu na Iramba, lakini Serikali ilitoa ramani inayoonesha kuwa ziwa hilo liko Wilaya ya Iramba, je, Serikali haioni kuwa sasa kuna umuhimu wa kurejea ramani hiyo ili wilaya zote mbili ziwe na umiliki wa Ziwa Kitangiri?

 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, alijibu. Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza migogoro ya usimamizi wa Mamlaka za Mikoa na Wilaya, Serikali wakati wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hutangaza mipaka ya maeneo hayo katika Gazeti la Serikali. Mkoa wa Singida ulianzishwa mwaka 1963 ukiwa na wilaya za Iramba, Manyoni na Singida. Kwa upande wa kaskazini magharibi ndiko ilikokuwa Wilaya ya Iramba ambayo inapatikana na Mkoa wa Shinyanga.


Mpaka kati ya Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Singida umefafanuliwa kwa maelezo yaliyotolewa na tangazo la Serikali Na. 266 la Desemba 14, 1973 lililoanzisha Wilaya ya Maswa na tangazo la Serikali Na. 137 la Mei 27, 1988 lililoanzisha Wilaya ya Meatu ambayo maelezo yake yanahusisha mpaka na Wilaya ya Iramba.


Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ya Tangazo la Serikali Na. 266 la mwaka 1973 yanafafanua kuwa eneo la Ziwa Kitangiri liko katika Wilaya ya Iramba. Aidha, maelezo hayo yanawiana na maelezo ya mpaka wa iliyokuwa Central Province kupitia ramani iliyochorwa kwa Tangazo la Serikali Na. 471 la  Novemba 16, 1962 kuonyesha mipaka husika.

Swali la nyongeza

Meshack Opulukwa: Mheshimiwa Naibu Spika asante, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kijiografia Ziwa Kitangiri lipo sehemu zote mbili – Halmashauri ya Wilaya ya Iramba pamoja na Halmashauri ya Meatu; na kwa kuwa kulikuwa na ‘beacons’ ambazo ziliwekwa na mkoloni ambayo zinaingia upande wa Mto Manonga na kutokea upande wa Mto Sibiti, mto unapotoka, ambazo zilivunjwa.


(a) Je, Serikali sasa itakubaliana na wananchi wa Meatu kwamba ni wakati mwafaka wa kukaa na kupitia upya ramani hiyo, ili angalau hilo ziwa liweze kuwa shared na pande zote mbili?


(b) Kwa kuwa mazingira ya kuanzisha Mkoa wa Singida mwaka 1963 yameshapitwa na wakati, imekuwa ni zamani sana na mazingira ya sasa yamebadilika, je, Waziri atakubaliana na mimi kwamba sasa imefikia wakati mwafaka kama kuna uwezekano wa kukaa na Halmashauri zote mbili –  Halmashauri ya Meatu pamoja na Halmashauri ya Iramba ili kuweza kutatua mgogoro huu ambao umekuwa ni wa muda mrefu?

Majibu ya Mwanri

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mnisikilize vizuri, na Mheshimiwa Opulukwa nakuomba unisikilize vizuri. Mimi ninachokizungumza hapa. Ni kweli anasema hili ziwa linahama wakati mwingine unalikuta lipo Singida wakati mwingine unalikuta lipo Shinyanga.

Lakini wilaya inayozungumzwa hapa, sasa hivi wala haipo tena Shinyanga ipo Simiyu.

When you look at these things in historical perspective, you are trying to be scientific.

Hapa nataka kusema kwamba tunaleta habari ya sheria ya nchi inavyozungumza hapa. Much as na-share na Mheshimiwa Opulukwa, hiki anachokizungumza hapa, ninamwomba sana atakapozungumza chochote ndani ya hapa na nje, kibebe wajibu kwa wananchi wote wa Tanzania na kibebe wajibu kwa wananchi wote wa Meatu na wale wa kule Iramba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunachozungumza ni sheria iliyounda hizi Halmashauri. Halmashauri hii ya Wilaya ya Iramba tunayoizungumza hapa ilianza toka mwaka 1958 ilikuwepo. Mwaka 1963 ndipo Mkoa wa Singida ulipoanzishwa.


Halmashauri ya Wilaya ya Meatu haikutokana na Singida ilitokana na Shinyanga, ilikuwa inatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa. Mipaka ilipobadilika ya wilaya ilikuwa ndani ya Mkoa wa Shinyanga wakati ule, kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.


Mheshimwia Naibu Spika, ukichukua GN hii ninayoizungumza hapa, hakuna mahali popote inaposema kwamba wakati ilipokuwa inaundwa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mipaka ya mkoa ule ilipanuka ikaenda mpaka Singida kwa maana ya Iramba.


Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba ili tusije tukaleta utata hapa niisome hiyo sheria inayozungumzwa hapa. Tafsiri ya Tangazo Na. 266 la mwaka 1973 kwamba Ziwa Kitangiri lipo Wilaya ya Iramba ni hii ifuatayo:-


Fence Westwards and Southwards along Northern and Western shores of lake to the boundary of Sibiti River, ambayo anaizungumzia Mheshimiwa Opulukwa (which marks the common boundaries of Shinyanga, Singida and Arusha regions), Fence the Sibiti to the Northern shore of Lake Kitangiri, fence along the Northern shore of Lake Kitangiri to the SRA of Sanga River.


Hii hapa ndiyo inayozungumzwa haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachozungumzwa hapa kama na AG upo hapo wewe unajua mambo ya sheria zaidi kuliko mimi. Tunazungumza habari ya utamaduni, tunazungumza habari ya desturi tunazungumza habari ya historia ambayo imeulizwa hapa kwamba imepitwa na wakati.


Mheshimiwa Spika, historia utamaduni ndiyo unaanza halafu inakuja sheria. Sheria kazi yake ni kulinda utamaduni, kazi yake ni kulinda sheria pamoja na historia ndicho ninachokielewa hapa.


Tukitoka hapa tukaenda tukawaambia wale wananchi wa Singida pale Iramba kwamba leo ziwa halipo kwenu hawatatuelewa.


Mheshimiwa Naibu Spika, lakini moja ambalo nataka Mheshimiwa Opulukwa aondoke nalo hapa akiwa amelielewa ni kwamba, ni kweli kabisa kwamba kuna haja kama anavyosema ya wananchi wa pande zote mbili kukaa kwa pamoja na kuzungumza namna nzuri ya matumizi bora ya Ziwa Kitangiri pale.


Kama Waziri Mkuu unayekaimu sasa hivi, kama tunaweza tukazungumza namna ya kutumia Ziwa Tanganyika kati ya Rwanda na Burundi na Uganda na Kenya wote kwa pamoja tukawa na mamlaka moja ambayo inatuunganisha tunazungumza, iweje leo hapa kwetu nchini Tanzania sisi wenyewe kwa wenyewe hapa tushindwe kuwa na utaratibu mzuri wa kukaa tukazungumza, tukaona jinsi ambavyo tunaweza tuka-share mambo haya?

 

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Mbunge, nimewaagiza ma-RAS (makatibu tawala wa mikoa) wamekwenda wamekutana na juzi walikutana twende tukakae wote kwa pamoja tukaangalie vizuri hiki kinachozungumzwa hapa. Lakini narudia tena lolote tutakalolifanya libebe wajibu kwa wananchi wetu wa Tanzania.


Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mwananchi anayezuiwa kukaa mahali popote katika nchi hii. Ukitaka leo kwenda Meatu, ukitaka kwenda Singida, ukitaka kwenda Mtwara, Kilimanjaro unaweza ukaenda.


Ninataka nikuthibitishie katika hili niko tayari tukashirikiana na wewe kwa niaba ya Waziri Mkuu ili tusaidiane tuondokane na tatizo hili kwa maana ya kulinda masilahi ya wananchi wetu.

2035 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!