Hatimaye timu maarufu ya Barcelona, leo inashuka dimbani kupepetana na timu ngumu ya nchini Italia – AC Milan, katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA).

Barcelona inaingia uwanjani ikiwa na deni la mabao mawili iliyonyukwa na AC Milan wiki kadhaa zilizopita.

 

Inakumbukwa kwamba katika kipindi hicho pia Barcelona imejikuta ikiambulia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Real Madrid.

 

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya soka, wanasema huenda timu hiyo ikaendelea kuwa kibonde kwa AC Milan, na wengine wanajipa matumaini kwamba leo itafuta uteja huo.

 

Kwa muda mrefu Barca imekuwa timu maarufu na tishio dhidi ya nyingine kutokana na kusheheni wachezaji wenye vipaji vya soka, lakini kandanda yake imeonekana kudorora msimu huu kinyume cha matarajio ya wengi.

 

Wachezaji mahiri wa Barcelona kama vile Alex Song, Pedro Redesma na Carles Puyol wameonekana kushindwa kukabili wapinzani wao katika mechi kadhaa zilizopita.

 

Timu hiyo sasa iko katika hatari ya kujiweka kwenye nafasi mbaya katika mashindano hayo ya UEFA, kama haitajikakamua kwa kupata ushindi katika mechi zilizo mbele yake.

 

Ikiwa Barcelona itanyukwa na AC Milan leo, basi itakuwa imezidi kujipotezea matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano hayo.

 

Mashabiki wengi na wapenzi wa soka wanasubiri kwa shauku kuu kushuhudia mechi hiyo leo, huku baadhi wakitarajia matokeo mazåuri kwa upande wa Barcelona na wengine kwa upande wa AC Milan.

 

Wakati Barca wakikwaana na AC Milan, kwa upande mwingine, Schalke inashuka dimbani kumenyana na Galatasaray katika mashindano hayo.

 

Kesho Bayern Munic, wakali wa Ujerumani, watachuana na Arsenal – watoto wa Emirates huku Malaga ikikabiliana na FC Porto.


By Jamhuri