Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, nakusalimu kwa salamu za heshima. Salamu hizi zinakujia kutoka kwangu mwananchi mwaminifu kwa nchi yangu ambaye nimeamua kukupa mkono wa shirika katika eneo la kuujenga uchumi.

Baada ya salamu hizo ninatumia mwanya huu kukupongeza kwa kufanikiwa kupenya na hatimaye kuwa Rais, katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa sana na ambao pengine ulikuwa mgumu. Bila kujali maoni ya upande wowote; ukweli ni kwamba wewe ndiye uliyepewa rasmi mikoba ya kuiongoza Tanzania kwa awamu hii. Wewe kuwapo Ikulu maana yake ni kuwa wananchi wana imani nawe.

Nakuandikia barua hii ukiwa bado hujachagua Baraza lako la Mawaziri na ukiwa unajiandaa kuzindua rasmi Bunge letu. Natambua kuwa kichwani mwako ama mkononi mwako huenda umeshashika orodha ya mawaziri na watendaji wengine ulio na mamlaka ya kuwateua. Hilo mimi halinisumbui kwa sababu maudhui ya barua yangu yanaweza kuwa na tija kabla ya uteuzi na hata baada ya uteuzi wako.

Mheshimiwa Rais, kiini cha barua yangu kwako ni kukuomba ujenge Serikali ya kijasiriamali. Ninaposema Serikali ya kijasiriamali ninamaanisha ambayo itakuwa na uwezo wa kutumia vichache kuzalisha vingi, itakayokuwa na uwezo wa kuongeza thamani katika mifumo na ambayo inaweza kufanya jambo lolote kwa kutumia chochote kilichopo.

Mheshimiwa Rais, nadhani unafahamu kuwa mambo yote duniani yana pande mbili na pande mbili ndizo zinazofanya dunia isimame na iendelee kwenda. Kuna kuuza na kununua, kuna kutoa na kupokea, kuna kusema na kusikiliza, kuna kuona na kuonwa,  kuna kufikiri na kufikiriwa pamoja na pande nyingine nyingi sana.

Mtu ama Taifa likijkita katika upande mmoja pasipo na kuleta usawazisho wa pande hizi mbili basi kunakuwa na anguko ama mkwamo. Mathalani, katika uchumi ikiwa unanunua tu pasipo kuwa na kitu cha kuuza maana yake ni kwamba utaanguka. Kutokana na kutokuwa na viwanda, kutokuwa na ubunifu na kutokuwa na mikakati; Taifa letu kwa muda mrefu tumejikuta tunanunua mfululizo kutoka kwa wenzetu. 

Tunanunua vijiko, tunanunua kalamu, tunanunua viberiti hadi sindano na njiti za kuchokonolea meno vyote tunanunua kutoka ng’ambo. Katika awamu yako ninatarajia uliwezeshe Taifa letu lipunguze sana kiwango cha kununua na liongeze kiwango cha kuuza.

Umaskini wa Taifa hili umetokana na sababu kubwa moja ya kwamba tumekuwa walafi wa kupokea kuliko kutoa. Ulafi wetu umepelekea mataifa yanayojitambulisha kama wafadhili na marafiki, kuturundikia madeni ambayo ni mzigo mkubwa. 

Katika kanuni za uchumi na kiroho ni kwamba mtoaji ndiye hubarikiwa, hii ina maana mpokeaji eidha anachangia kumpa baraka mtoaji ama anajitafutia laana kwa ulafi wa kupokea. Mtoaji huwa na sauti kuliko mpokeaji. Ndiyo maana Taifa letu limekuwa halina sauti, halina uwezo wa kusema na kusikika kimataifa badala yake tunalazimika kusikiliza tu. 

Wanatupa misaada lakini wanatusemea na kutupangia cha kufanya. Tumekuwa wanyonge mno. Ukishakuwa huna uwezo wa kusema na ukasikika maana yake utakuwa ukipuuzwa, yaani huonwi japokuwa wewe unaona. Ndiyo maana tuna bidii kubwa ya kufunga safari na kwenda kuomba misaada, yaani tunawaona wa kutusaidia badala ya kujiweka kwenye nafasi ya kuonwa na wale ambao tutafanya nao mambo ya kunufaishana badala ya kunyonywa. 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri