Madudu, kero Hospitali ya Bagamoyo

Hivi karibuini nilikwenda kumjulia hali jamaa yangu aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo. Niliyoyaona yanashangaza sana kwa kuzingatia kuwa huko ni nyumbani kwa Mheshimiwa Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete. Katika mantiki ya kawaida, kihuduma Bagamoyo ingekuwa ya kupigiwa mfano.

Nawasilisha malalamiko haya kutokana na viwango na aina ya madudu yanayofanywa na idadi kubwa ya watumishi wa taasisi hiyo hasa wauguzi (nurses). Yanayotokea ni kweli kinzani (paradox) lakini ni kweli tupu. Yafutayo ni baadhi tu ya yale niliyobaini:

 

1. Wizi wa dawa: Wauguzi hawatoi dawa kwa wagonjwa kwa mujibu wa maelezo ya madaktari. Kama mgonjwa ametakiwa kujinunulia dawa, wauguzi humlazimisha mnunuzi awape wauguzi dawa hizo wakae nazo. Wakipewa hazionekani tena. Ukiwauliza unapata majibu ya kifedheha na kibabe.

 

2. Utovu wa uwajibikaji: Wauguzi hutumia muda wao mwingi wakisogoa nje ya mawodi, wakati mwingine (na hii ni nadra sana) huwatuma wasaidizi wao kwenda kuwachungulia wagonjwa.

 

3. Uvunjifu wa maadili ya taaluma: Mgonjwa anapofariki wauguzi huwaambia ndugu na jamaa wa marehemu wampeleke maiti mochwari (wengi hawajui sehemu hiyo ilipo). Ni jambo la ada kuwa mtu anapofariki hawekewi pazia au kufunikwa shuka, hubakia akiwa wazi na hali hiyo huleta fadhaa kwa wagonjwa wengine, maiti hubakia kitandani kwa zaidi ya saa  sita, hiyo ni hali ya kawaida sana.

 

4. Hospitali haina shuka kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa na wauguzi wamepiga marufuku wagonjwa kutumia shuka zao binafsi. Wagonjwa hulala wazi huku wakitetemeka. Wodi ya watoto ina shuka lakini zinapochafuka wauguzi huwalazimisha wazazi wakazifue.

 

5. Ushirikina umekithiri: Wagonjwa wengine wafikapo kupata tiba kitaaluma, wauguzi huwaelekeza waende kupata tiba kwa waganga wa jadi. Kwa mfano, katika wiki ya pili ya Juni 2013, mzee aitwaye Peter alifika hospitalini kumwona jamaa yake, hali mbaya ya mgonjwa ilimshtua Peter alianguka, nduguze wakampeleka wodini.

 

Huko wauguzi wakaagiza wakanunue (drip), hawakuitumia mara moja, baada ya muda usiopungua nusu saa wauguzi wakasema Peter apelekwe kwa waganga wa kienyeji. Mzee huyu aliaga dunia bila kupata tiba. Ndugu wa marehemu wakaambiwa na wauguzi wampeleke maiti mochwari.

 

Wiki hiyo hiyo, mama mmoja alifika hospitali aliweweseka (bila shaka malaria ilipanda kichwani). Wauguzi wakashauri apelekwe kwenye tiba za jadi, mgonjwa huyu alitekeleza aliyoambiwa. Je, watumishi hawa ni waajiriwa wa serikali hapo hapo wakiwa mawakala wa waganga wa jadi?

 

6. Ubabe/ujeuri/ufedhuli: Hizo ni sifa ambazo wauguzi wa hospitali hiyo wanazo. Hawana kauli nzuri kwa wagonjwa, ndugu na jamaa zao wanapofika kuwajulia hali. Wana kasumba ya kukaripia na kutoa majibu ya kifedhuli na kibabe wanapoulizwa jambo linalomhusu mgonjwa.

 

Mambo wawili makuu niliyoyagundua kuwa ndiyo kiini cha utovu wa nidhamu na uwajibikaji kwa wauguzi: Moja, kuna upogo katika uongozi na utawala katika taasisi hiyo. Pili, wauguzi wameselelea hapo Bagamoyo, hali iliyowapa nguvu ya kujiamini kupita kiasi, na hivyo kukengeuka maadili ya kazi. Kuna umuhimu malalamiko/madudu yaliyopo yakafanyiwa kazi ili hospitali hiyo itoe huduma stahiki.

 

Nawasilisha.


Mwananchi mzalendo,

Bunju, Kinondono

1919 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!