BARUA ZA WASOMAJi

Polisi Biharamulo wanatumaliza

Kwa kawaida tunajua kuwa mtu akiwa mikononi mwa askari polisi atakuwa yuko kwenye usalama, lakini huku wilayani Biharamulo, Kagera hilo halipo.

Huku askari polisi wengi badala ya kulinda usalama wa raia na mali zao, wao wamegeuka kuwa maadui wa raia na mali zao! Wanapita vijijini kukamata watu na kuwapiga hadi kuua wengine bila sababu!

 

Wananchi wengi huku wanakamatwa bila sababu na kupelekwa kituoni huku wakipigwa sana. Hasa wasiyo na hela za rushwa kwa polisi ndiyo hunyanyaswa hadi kujuta kuzaliwa na kuishi Biharamulo.

 

Hivi karibuni, Mheshimwia Rais Jakaya Kikwete alikuja huku Kagera na kutoa tamko kwamba majambazi warudishe silaha kwa hiari zao. Tamko hilo sasa limekuwa biashara ya askari polisi wa huku.

 

Polisi wakiona mtu mwenye uwezo wa kiuchumi wanambambikia kesi ya ujambazi au ya silaha na kumshikilia kituoni muda mrefu huku wakimlazimisha atafute wadhamini watakaomlipia Sh milioni tano!

 

Kwa mfano, hivi karibuni kijana mmoja alikamatwa na polisi wakampiga mpaka wakamuua. Pia polisi hao hao walimkamata mzee mmoja aitwaye Kupanda Makenika wiki tatu zilizopita, hajawampeleka mahakamani, yuko kituo kidogo cha polisi Chakende, kila anapoomba dhamana anaambiwa atoe Sh milioni saba, kisa anaambiwa ana ng’ombe wengi.

 

Wakazi wa Miharamulo tunauliza: Je, huo ndiyo ulinzi wa usalama wa raia na mali zao? Je, hiyo ndiyo polisi jamii ? Sisi tunaiona ni polisi biashara!

 

Tunaomba viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vya habari vimulike askari polisi wa huku, wanatumaliza!

 

Ni sisi wakazi wa Nyakanazi, Biharamulo

 

Wauza ‘unga’ wameiweka mahakama mfukoni

Wauza ‘unga’ na mafisadi wameshika mahakama ndiyo sababu kesi nyingi zenye maslahi kwa taifa Jamhuri haishindi, na baadhi ya watoa hukumu (majaji na mahakimu) wamekuwa miungu-watu!

 

Tunawalaumu sana askari polisi ilhali mahakama ndiyo tatizo letu. Baadhi ya askari polisi nao wamefika mahali sasa wamekata tamaa na kuamua kushirikiana nao.

 

Majaji na mahakimu wengi ni matajiri wasio na viwanda wala maduka. Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakichunguza suala hilo watashangaa.

 

Naomba Gazeti JAMHURI mtumie njia zenu kumjulisha Rais formally (rasmi) na kisha mzichapishe gazetini ili ajue mambo yameanikwa wazi. Wauza unga wanatamba sana. Ni aibu kubwa!

 

Mpenzi wa JAMHURI

0764 932 549