Katibu wa Bavicha, Julius Mwita.

 

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema (Bavicha) limesema limeshangazwa na kauli ya Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, kuhusu sakata la Mbunge, Tundu Lissu kupigwa risasi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi Januari 11, Katibu wa Bavicha, Julius Mwita amedai kuwa kauli ya Shaka kwamba Lissu anatumia tukio hilo kutafutia umaarufu ni ya kupotosha umma.

 

“Tumemtafakari sana Shaka, Serikali na CCM wamekiri hawawezi kujibishana na Mh. Tundu Lissu kwa sababu ni mgonjwa, Shaka anapata wapi ujasiri wa kuja kuzungumzia habari zinazomhusu Lissu?  Shaka anapingana na kauli ya Lissu kwa uongo na kwa ushahidi usiokuwa na uthibitisho wowote.

“Anawadanganya Watanzania kwamba katika nchi hii Lissu si wa kwanza kushambuliwa kwa risasi. Kleruu hakushambuliwa kwa sababu za kisiasa. Abeid Karume hakuuawa kwa sababu za kisiasa na wala hajawahi kuwa mpinzani wala mkosoaji wa Serikali iliyokuwepo madarakani wakati huo.  Huwezi kusema aliuawa kwa sababu za kisiasa.

“Tumekuwa tukiomba Serikali ipewe msaada katika uchunguzi wa shambulio la Lissu, sioSerikali, IGP, DCI wala Spika, hakuna yoyote aliyetoka akaeleza maendeleo ya uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Julius Mwita.

Shaka Hamdu Shaka.

Hivi karibuni Shaka alizungumza na wanahabari kuhusu tukio la kushambuliwa kwa Lissu.

“Madai ya Lissu kuwa kabla na baada ya Uhuru Tanzania haijawahi kushuhudia mwanasiasa akishambuliwa kwa Risasi, yanatosha kuthibitisha kuwa mwanasiasa huyo si mkweli.

“Lissu hafahamu kupigwa risasi kwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk. Wilbert Kleruu na Mbunge wa Morogoro Kaskazini, Nickas Mahinda, huku wote wakiwa viongozi waandamizi wa Serikali na hawakuwa wapinzani.

“Matamshi ya Lissu kudai tukio la kushambuliwa ulikuwa ni mpango wa kummaliza na kumuua ili kumziba mdomo asiikosoe Serikali ni maneno ya kusaka umaarufu kwa bei rahisi na kuziingiza katika uhasama Kenya na Tanzania mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

“Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM haiwezi kupanga njama dhidi ya Lissu ili kumziba mdomo kwa sababu ni mwanasiasa dhaifu, asiyejua mbinu za kukosoa wala kujenga hoja kwa weledi,  hivyo hawezi kusimama katika safu ya wakosoaji kama ilivyokuwa kwa wanasiasa kabla yake,”alisema Shaka.

1075 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!