Bei za vyakula zapandisha mfumko wa bei

Kupanda kwa bei za vyakula kumesababisha kupanda kwa kiasi kwa mfumko wa bei, Benki Kuu (BoT) imeeleza katika ripoti yake ya hali ya uchumi kwa mwezi Oktoba.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa mwezi uliopita inaonyesha kuwa mfumko wa bei kwa mwaka ulifikia asilimia 3.6 ukiongezeka kwa asilimia 0.2 kutoka asilimia 3.4 iliyorekodiwa mwezi uliotangulia.

Kiasi hicho pia kilikuwa ni zaidi ya asilimia 3.2 ya ambacho kilirekodiwa mwaka mmoja uliopita.

Hata hivyo, licha ya kukua, mfumko wa bei ulikuwa chini ya lengo la muda wa kati la serikali la asilimia 5.0 na ndani ya lengo lililowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) la asilimia 8.0 na lengo la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) la kati ya asilimia 3 na 7.

Kwa mujibu wa BoT, ongezeko la bei za vyakula na vinywaji laini ndizo zilisababisha ongezeko hilo la mfumko wa bei katika mwezi Oktoba.

Katika kipindi cha mwaka, mfumko wa bei ulikuwa asilimia 5.1 mwezi Oktoba 2019 ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwaka mmoja uliopita na asilimia 1.2 katika mwezi kama huo mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kupanda kwa bei za nafaka kama vile mahindi na mchele kutokana na kushuka kwa uzalishaji katika baadhi ya maeneo ya nchi na kupanda kwa mahitaji katika nchi jirani, ndiko kulisababisha kupanda bei ya bidhaa hizo, hivyo kuathiri kiwango cha mfumko wa bei.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa mfumko wa bei wa miezi 12 ulishuka hadi asilimia 2.7 mwezi Oktoba 2019 kutoka asilimia 3.1 ya mwezi uliotangulia, hivyo, kwa kiasi kidogo kupunguza kasi ya kupanda kwa mfumko wa jumla.

Udhibiti wa bei za bidhaa zisizo za vyakula kama vile petroli, mafuta ya taa, dizeli, kuni na vifaa vya habari kulisaidia pia kutopanda sana kwa mfumko wa bei.

Mfumko wa bei za nishati na mafuta kwa mwaka ulishuka hadi asilimia 3.0 mwezi Oktoba 2019 kutoka asilimia 19.5 mwezi kama huo mwaka 2018, kufuatia kushuka kwa bei rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa.