Biashara zinahitaji akili za kisasa

Wiki mbili zilizopita, nilipata wasaa wa kuongea kwa kirefu kwa njia ya simu na mjasiriamali kutoka mkoani Singida. Katika mazungumzo yetu mjasiriamali huyu wa miaka mingi alilalamika namna biashara zilivyobadilika nyakati hizi na namna ushindani unavyotishia mustakabali wake.

Mjasiriamali huyu alinipa mifano ya namna zamani alivyokuwa akipata faida kubwa katika bidhaa mbalimbali. Anaeleza, “Zamani nilikuwa nakwenda Dar es Salaam na kununua unga wa ngano kwenye mifuko ya kilo 50, nikija hapa Singida nikiuza kwa jumla ninapata faida ya hadi shilingi elfu tano. Leo hii mfuko wa unga wa kilo 50 huwezi amini, ninapata faida isiyozidi shilingi mia tano!

“Kwa zamani maisha yalikuwa hayajapanda, hivyo faida ya shilingi elfu tano niliyokuwa naipata kwenye mfuko unaweza kuona namna ilivyokuwa na thamani ikilinganishwa na hii mia tano ninayoipata leo ambapo gharama za maisha ziko juu sana.

“Zamani nilikuwa ninauza sana kwa sababu wafanyabiashara tulikuwa wachache, lakini siku hizi kuuza hata mifuko kumi kwa siku ni bahati nasibu kwa sababu kila kona watu wanafungua maduka.”

Kimsingi hofu aliyokuwa nayo mjasiriamali huyu imeanza na inaendelea kuwatafuna wajasiriamali wengi wa zamani na wanaoingia sasa. Miaka ya zamani watu walizoea kupata faida za mara mbili hadi mara tatu. Lilikuwa ni jambo la kawaida kwa mfanyabiashara kununua bidhaa kwa Sh 10,000 na kuiuza kwa Sh 20,000 au zaidi.

Kwa zamani haikuwa kazi ngumu sana kukuza mtaji kama ilivyo leo. Siku hizi wafanyabiashara wengi watakubaliana nami kwamba kutokana na udogo wa faida zilizomo kwenye biashara nyingi tunazofanya; ni rahisi sana kupoteza mtaji kuliko hata kuukuza.

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba siku hizi hakuna bidhaa ambazo watu wanapata faida mara mbili au tatu; isipokuwa sote tutakubaliana kwamba idadi ya bidhaa hizi inazidi kupungua kwa kadiri wigo wa mawasiliano unavyozidi kupanuka. Na hata ikitokea ‘umeotea’ kuuza bidhaa za aina hii, washindani wako wanakusoma upesi na kesho utashangaa wameleta bidhaa zile zile na wamevunja bei kabisa.

Pia kuna wafanyabiashara wachache ambao wanaendelea kupata faida kubwa kutokana na sababu za miundombinu mibovu ya wanakofanyia biashara.

Mfano, kabla ya kujengwa kwa barabara ya Dodoma-Iringa kupitia Mtera kwa kiwango cha lami, kuna wafanyabiashara wa maeneo inakopita barabara hiyo walikuwa wakiuza bidhaa mbalimbali kwa bei kubwa kutokana na ubovu wa barabara uliokuwapo.

Hata wafanyabiashara wa mabasi walikuwa wakipata faida kubwa sana kutokana na kujaza abiria kupindukia kwa sababu ni magari machache yalikuwa yakipita katika barabara hiyo.

Kwa sasa Serikali imeshajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami; magari mengi yanapita barabara hiyo, bidhaa zinafika kiurahisi. Kilio kimewafikia wafanyabiashara wa magari na wale wa bidhaa ambao hawakuiona hatari ya mabadiliko yaliyokuwa yanawajia.

Kama ulikuwa unapata faida maradufu, upende ama usipende lazima ukubaliane na hali ya kushuka kwa faida. Kama basi lako lilikuwa linajaza watu kupindukia na kama halikuwa la kisasa, upende ama usipende lazima utaondoka katika biashara.

Hizi ndizo zama tulizonazo ambapo mabadiliko katika biashara yanaenda kwa kasi ya ajabu sana usiku na mchana. Biashara inayokupatia faida nono leo usishangae kuona kuwa kesho inakukataa.

Hizi siyo nyakati ambazo unaweza kumudu kufanya biashara ya aina moja miaka zaidi ya kumi pasipo kufanya maboresho halafu utarajie kuendelea kupata faida, haiwezekani!

Unapoanza biashara leo lazima kichwani mwako utengeneze mpango kazi kuhusu biashara husika. Ujiulize, je, ni kwa muda gani biashara yangu itanizalishia faida? Je, ikiwa mambo yataenda vibaya kabla sijarudisha mtaji wangu nitafanyaje?

Kama biashara hii ikiingiliwa ama ikifa nitafanya nini kingine? Je, ni mikakati gani niliyonayo kukabiliana na ushindani uliopo au unaoweza kujitokeza?

Jambo kubwa ambalo linatugharimu wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wa Kitanzania ni uvivu wa kujifunza. Ni wachache wenye utamaduni wa kujisomea vitabu vinavyohusu namna ya kuboresha mitazamo na biashara zao. Ni wachache wanaochukua muda kwenda kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wengine waliofanikiwa. Tunataka kuishi kwa “surprises” za kutaka wengine waje kuona tu tumefanikiwa.

Tunaanguka na kujikwaa sana, tunadumaa sana na tunatoka jasho jingi lisilo na sababu wakati tungeweza kupunguza makosa kwa kujifunza kutoka kwa waliotutangulia. Wakati mwingine ni hofu ya kuoneana wivu, lakini sehemu kubwa ni ujinga wetu!

Wengi ni mabingwa wa mtindo wa ‘funika kombe mwanaharamu apite’ au utamaduni wa kesho itajisumbukia yenyewe. Wengi hawana utamaduni wa kufanya utafiti kabla na baada ya kuanzisha biashara zao ili kutambua hatari, umuhimu na namna ya kukabiliana na mabadiliko. Ndiyo huu mtindo utaona kuwa watu wengi wanaanzisha biashara kwa kuigana.

Wajasiriamali wengi hawapendi kujishughulisha kubuni bidhaa na huduma mpya ndiyo maana mabadiliko yanapokuja yanaishia kuwatoa machozi wasijue cha kufanya.

Nimepata kueleza namna biashara zinavyobadilika na hatari inayowakabili wajasiriamali. Nilitoa mfano wa wajasiriamali waliolivamia soko la shule za sekondari kuanzia miaka ya 1990 hadi ya 2000 kutokana na ‘gepu’ la uhaba wa sekondari uliokuwa ukilikabili Taifa letu.

Hata hivyo, katikati ya miaka ya 2000 Serikali ikaibuka na mpango wa shule za kata nchi nzima. Hadi muda huu shule nyingi za binafsi zimeathirika kwa sehemu fulani kutokana na shule hizi za kata, kwa sababu wazazi wengi ambao ndiyo waliokuwa wateja watarajiwa, sasa wanawapeleka watoto wao kwenye shule hizi za hali ya mtu [za kata].

Kama unafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa biashara katika sekta ya elimu, utagundua kuwa hadi muda huu kinachosaidia shule binafsi kuendelea kupata wanafunzi; si kingine bali ni kutoboreshwa kwa shule za kata.

Lakini tunafahamu kuwa Serikali inapiga jaramba kujenga mabweni kwenye shule zote za kata, kujenga maabara na pia tumeendelea kushuhudia ikimwaga walimu kwenye shule hizi kila mwaka.

Uwe na uhakika kwamba siku shule za kata zitakapoboreshwa kwa kuwa na mabweni, kuwa na maabara na walimu wa kutosha; hicho kitakuwa kitanzi kingine kikubwa kwa shule za binafsi.

Zipo biashara nyingi ‘zinazopumulia mashine’ kutokana na mabadiliko ya zama hizi, baadhi yake ni biashara ya teksi kuingiliwa na biashara ya bajaj na bodaboda, biashara ya ‘internet cafes’ kuingiliwa na utitiri wa simu za kisasa za mikononi zenye internet, biashara za maduka ya kuuza magari kuingiliwa na mapinduzi ya internet (badala ya kununua gari dukani kwako, mtu anaagiza gari kwa urahisi kutoka nje ya nchi, na tunakoelekea biashara ya usafirishaji abiria itatikiswa na kuingia kwa ndege za jumuia (ndege za bei nafuu).

Swali la kujiuliza ni hili: mjasiriamali na mfanyabiashara unafanyaje katika zama hizi? Jibu ni jepesi: Lazima uwe ni mtu wa kujifunza na kuongeza maarifa yako kila siku. Kujifunza kutakusaidia kufanya uamuzi kabla au hata wakati wa hatari na changamoto za mabadiliko. Kujifunza ni kujiandaa kwa ajili ya mabadiliko na kuyapokea mabadiliko kwa furaha na kwa utayari. Kujifunza kutakusaidia kuwa na akili inayoona mbali, inayobuni na inayotafuta kukua kila siku.

Mjasiriamali anayesema sina muda wa kuwasikiliza wataalamu au anayesema sina muda wa kujisomea ni sawa na kusema sina muda na mabadiliko au sina muda na maendeleo. Kufuatilia sera na mipango ya Serikali na namna inavyoweza kuathiri biashara yako ni suala la muhimu.

Tuchukulie mfano wa mjasiriamali mwenye ndoto ya kuanzisha shule yake ya sekondari. Kama asipochukua hatua za kufuatilia na kujifunza mambo mengi kuhusu sekta hii ya elimu, anaweza kujikuta anafungua shule ambayo haina utofauti na viwango vya shule za kata.

Kimsingi ni vigumu kwa mzazi kumleta mwanaye katika shule yako unayotoza ada ya laki nane ilhali haina utofauti wowote na shule ya kata anakoweza kulipa ada na michango isiyozidi laki moja.

Nini maana yake? Maana yake ni kwamba unapoanzisha biashara yoyote katika zama hizi, lazima uhakikishe inakuwa na utofauti na ihakikishe inajibu mahitaji ya kundi fulani la wateja unaowakusudia.

Vile vile lazima uwe na mikakati ya kuboresha biashara yako, kuachana na biashara hiyo inapobidi, kubadilisha muundo wa biashara yako; katika muda uliojipangia na katika nyakati unapolazimishwa na mazingira ama mabadiliko ya kufanya hivyo.

Wajasiriamali tunahitaji ushindi wa kimtazamo.

 

[email protected]

0719 127 901