Miaka 20 kifo cha Mwalimu Nyerere

Mei 16, mwaka huu Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT) ambacho ni chama cha kitume ndani ya Kanisa Katoliki kiliandaa kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Dhamira ya kongamano ilikuwa Maendeleo Jumuishi na yenye kujali ustawi wa maisha ya wananchi. Mada mbalimbali zilijadiliwa. Washiriki walitoka makundi na taasisi mbalimbali wakiwa ni wadau katika kujenga taifa na kuleta maendeleo jumuishi na yenye kuwajali watu na utu wao. Kongamano lilifanyika Msimbazi Centre, Dar es Salaaam. Mwandishi MANYERERE JACKTON alihudhuria kongamano hilo na kuchukua yote yaliyowasilishwa na kujadiliwa.

Ufuatao ni mchango uliotolewa na Mkurugenzi – Kurugenzi ya Uchungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, PADRI FLORENCE RUTAIHWA. Endelea…

Baba wa Taifa alitutoka kimwili, lakini tunapoendelea kufanya makongamano kama haya tunaona Nyerere bado anaishi. Ndiyo maana hata kwenye vyombo vya habari tunasikia kile kipindi cha “Wosia wa Baba” – kwamba alifanya mazuri ambayo kila mtu hana budi kuyaiga kama tunataka kujenga taifa lililo bora.

Mwalimu Nyerere kama tunavyojua katika falsafa yake alipenda sana maendeleo. Alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne; Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Ni mambo ambayo hakuna mtu anaweza kupingana nayo…kama wewe ni mpenda maendeleo. Kama wewe ni mwanaharakati hayo mambo manne ni mambo muhimu sana.

Mambo mengi tuliyozungumza yamejikita katika suala zima la kumjengea uwezo mwanadamu. Kumjengea uwezo Mtanzania. Mtanzania wa leo anahitaji kujengewa uwezo. Lakini hatuwezi kumjengea uwezo mtu ambaye hana maadili, ndiyo maana kuna bango [ukumbini] linasema: “Bila maadili hakuna utu – ‘tuanze safari yetu ya kuyahuisha.’”

Nawashukuru wote ambao mnazungumzia suala la maadili. Nikirudi katika falsafa ya Mwalimu Nyerere kwamba ili tuendelee tunahitaji Watu… sisi ni watu ambao tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu kama tunavyosoma katika Kitabu cha Mwanzo 1:26-27 – kwamba Mwenyezi Mungu alituumba kwa sura na mfano wake.

Mwenyezi Mungu anatutaka tuwe watu ambao tunaendeleza kile ambacho alikiumba. Katika Kitabu hicho hicho cha Mwanzo 1:28 Mwenyezi Mungu alimwambia mwanadamu: “Zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha.” Lakini sasa  tunaona jinsi mwanadamu anavyokiuka maadili badala ya kuzingatia kama ilivyo katika Amri ya Kwanza ya Mungu ambayo alimpa mwandamu.

Kabla ya vingine vyote aliwaambia hilo – zaeni mkaongezeke, mkaijaze dunia. Tunaona watu wanavyokiuka maadili. Wanafika hatua mpaka mwanamume na mwanamume wanakwenda kufunga ndoa. Hapo tayari umeshakiuka agizo la Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu anatuambia kwamba: “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.”

Sisi Wana CPT tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba watu hawaangamii kwa sababu ya kukosa maarifa. Watu wakiangamia kwa sababu ya kukosa maarifa, na sisi ambao tulikuwa tayari kuwasaidia hao watu, Mwenyezi Mungu atatuuliza. Katika kumjengea uwezo huyo mtu, mmojawapo katika ufunguzi [wa kongamano] alisema mwanadamu au sisi watu si maskini kwa sababu tunakosa pesa, lakini tunakuwa maskini kwa sababu tunakosa maadili.

Tuangalie ni watu wangapi ambao wanapata pesa lakini kama hujui namna ya kutumia pesa hiyo utaendelea kuwa maskini. Nakumbuka kuna shule moja inaendeshwa na Wazungu –pale walikuwa wanamwambia mzazi: “Usimwachie mtoto zaidi ya Sh 20,000 sisi tutamfundisha namna ya kutumia pesa.” Lakini siku hizi mtoto anaachiwa nini…anaachiwa nini na katika kukua kwake anaona hivi vitu vipo, lakini siku moja vikija kwisha ghafla anakuwa maskini wa kutupwa kwa sababu hakuwa na maadili ya kutumia pesa.

Ndugu zangu, tumesema kwamba maendeleo hayatokani na vitu zaidi, yanatokana na sisi wenyewe jinsi tunavyoboresha kile ambacho Mwenyezi Mungu ametujalia. Cha kwanza ambacho Mwenyezi Mungu ametujalia ili kifanye tuwe na maendeleo ni FIKRA. Sisi wakati tunasoma shule za msingi nakumbuka tulikuwa tunamuenzi Mwalimu Nyerere – wakati bado tunasoma lile somo la siasa. Tulikuwa tunafundishwa “Zidumu Fikra Sahihi” na tuzidumishe. Kwa hiyo unaona kwamba tusipodumisha fikra sahihi kila mtu atakuja na fikra zake. Kuna kipindi cha “Busara za Mlevi”, ni kulembesha lugha kwamba huyu amelewa, lakini bado ana busara! Lakini tungekuwa tunaweza kudumisha “fikra sahihi”…mimi nilikuwa napenda sana somo la siasa.

Tuweze kuepuka tabia ya kupongeza na kuenzi tabia mbaya. Kuna mmoja alisema kwamba unakuta mtu ni fisadi wanamwita mwanamume wa shoka! Sisi Watanzania Kiswahili chetu tunajua walau kulembeshalembesha mambo – pengine labda ni tafsida.

Mwalimu Nyerere alisema tunahitaji Uongozi Bora. Mwaka huu ni wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wana CPT naomba tusaidie katika kuwasaidia watu waweze kuwa na uongozi bora.

Jambo jingine ni Elimu Dini. Tupige kelele, tuwe na sauti ya kinabii katika kuhakikisha kwamba elimu dini shuleni inafundishwa. Kama sikosei wengi ambao ni maprofesa, wengi ambao ni watu mashuhuri katika nchi hii – sitaki kwenda katika nchi nyingine – wengi ni matunda ya elimu dini. Ama, mmesomea kwenye shule za misheni mkafundishwa dini – hata kama ulitoka kwenye familia ya kipagani, lakini uliona mahali fulani kuna watu wa dini – ukaenda kule wakakuendeleza.

Kuna wazee wastaafu hapa, na bila shaka serikali bado inawasikiliza. Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera [Philip Mangula], mimi nikiwa kijana, tunaomba na kwa kuwa mmekubali kuwa pamoja na sisi, pale ambako mnaona kwamba mnaweza mkawa jicho letu, mkawa mdomo wetu, kwa kweli bila watoto kufundishwa dini, yote yatakuwa kazi bure.

Tuangalie ni vitu gani tunavipa kipaumbele. Mimi nimesomea Kenya katika masomo yangu ya juu. Vilevile nilikuwa nakwenda kufanya kazi za uchungaji maparokiani. Tunashukuru sana Wakenya wakati fulani walikuwa wananiita – wana misa ya harambee kwa ajili ya kuchangia mtu fulani anaumwa. Wanasema tuna misa ya harambee kwa sababu tunataka kuchangia mtu fulani amekosa karo. Watanzania vitu kama hivi utasikia wanaomba “uje utufungulie kikao cha michango ya harusi”. Harusi moja waliniita nikaenda kwa kweli nilishiriki. Harusi ilitumia Sh milioni 80. Siku moja tukanywa na kula halafu kesho tukawa kama tulivyokuwa.

Mwalimu Nyerere nafikiri vitu vya aina hii alikuwa havipi kipaumbele. Tujaribu kuangalia ni kitu gani tunakipa kipaumbele.

Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuipatia elimu kipaumbele – hasa elimu dunia na elimu dini. Elimu ndiyo itakayotukomboa katika mambo yote. Mwingereza anasema: “If you think education is expensive, try ignorance.”  Tumsifu Yesu Kristu.

669 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!