Bodi ya Korosho imetakiwa kulipa haraka deni la Sh milioni 16 kwa Kijiji cha Kimanzichana Kaskazini, wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani baada ya kukodi ghala la kijiji hicho kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo za korosho.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, wakati wa ziara yake kukagua shughuli za maendeleo katika vijiji vya Kimanzichana Kaskazini na Kilimahewa.

Ulega ni Mbunge wa Mkuranga ambako vijiji hivyo vipo.

Akizungumza katika mikutano na wananchi wa vijiji hivyo, Ulega ameutaka uongozi wa Bodi ya Korosho kulipa fedha hizo ili vijiji hivyo viweze kuzitumia kwa shughuli za maendeleo.

Aidha, akizungumza na wanafunzi katika shule za msingi Kimanzichana Magharibi, Kilimahewa na Shule ya Sekondari Mkamba, Ulega amewataka wanafunzi hao kuweka bidii katika masomo yao.

Mbali na kuzungumza na wanafunzi hao, Naibu Waziri Ulega ametoa zawadi ya madaftari katika shule hizo, ikiwa ni sehemu ya ahadi aliyotoa ili kuongeza tija kwa wanafunzi hao waweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.

Halikadhalika Ulega ametembelea pia jengo la ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kilimahewa ambalo ujenzi wake hadi sasa umegharimu Sh milioni 40 na kutoa mchango wa Sh 500,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo na kupanda mti.

By Jamhuri