Miaka mitano iliyopita Rais wangu, Dk. Jakaya Kikwete, wakati akijinadi na kuomba kura kutoka kwa wapigakura, aliahidi mambo mengi kwa Watanzania.

Kwa siku ya leo nitagusa ahadi moja tu ambayo ni changamoto kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, na ahadi iliyobadilika na kuwa silaha kubwa inayotumika kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete aliahidi ajira kwa vijana ikiwa ni karata nzuri iliyotumika kuongeza kura za kuingia kwake madarakani kutoka kwa vijana.

Miaka imekimbia kweli kweli, siku zinayoyoma na hatimaye rais wetu amebakiza siku chake kumaliza ngwe yake ya uongozi, huku ahadi hiyo ikiendelea kuelea hewani bila utekelezaji wowote uliotarajiwa na vijana nchini.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliwahi kusema hadharani ya kuwa ajira kwa vijana nchini ni ‘bomu, bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote’. Wapo waliombeza kutokana na kauli yake hiyo ya tahadhari kwa Serikali na chama kwa ujumla.

Katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia ni kwa kiasi gani ukosefu wa ajira kwa vijana wa Taifa letu unavyogharimu maisha ya vijana, ndugu zetu wanapotezwa na ajira walizoamua kujipachika bila kujali athari zake.

Tunawashuhudia vijana wengi walivyoamua kujiajiri katika madampo na majalala ya kila aina hapa nchini hasa katika mikoa mikubwa. Wanashinda majalalani wakiokota makopo kiasi cha kukosa hata muda wa kukoga na kufua, wananuka taka kutokana na kuishi majajalani ambako kunawaingizia kipato cha kusogeza siku.

Kutokana na maisha hayo ya majajalani, wamejikuta kila siku tunapoteza vijana wetu kutokana na mazingira ya ajira hiyo ya majalalani, inayosababisha wengine kuwa na uwendawazimu unaotokana na ugumu wa kazi zao na maisha kwa ujumla.

Wale vijana wengine wanaojiona ni wajanja wameamua kufanya biashara inayowaingizia fedha za haraka haraka huku maisha yao yakiwekwa rehani.

Wanasafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine, wamegeuzwa punda wanaosafirisha biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kile kinachoitwa ‘mzigo ufike hata kama punda atakufa’. Kutokana na maisha magumu na ukosefu wa ajira, wengi wao wako mikononi mwa dola katika nchi mbalimbali.

Vijana wajanja wamekuwa ‘wazungu wa unga’, kazi yao kusambaza ‘unga’ nchi moja baada ya nyingine, wanapata pesa, wanasaidia familia zao huku wakiishi maisha ya kujificha.

Ahadi hii iliyotolewa na CCM wakati ule imekuwa mwiba; mwiba unaotumika kukiadhibu chama kutokana na kutotekelezeka kama ilivyotarajiwa. Vijana nchini wamekasirika, wamekichukia chama kwa kile wanachodai kuwa ni kuwahadaa na sasa wanataka kukiadhibu kwa kuwapuuza.

Vijana wanakasirishwa na kauli zinazotolewa na wanasiasa nchini, ambazo zimekuwa zikiwadhalilisha na kuwabeza kwa kuwaita ‘wanywa viroba’.  Chama changu kinatakiwa kianze kwa kuwaomba radhi vijana nchini, kiwaombe radhi kwa kuwacheleweshea ajira zao walizowaahidi ili kuweza kupoza makali ya hasira zao.

Huu si wakati wa kuwabeza vijana kama ilivyofanyika, vijana wana nguvu; nguvu ya uamuzi na nguvu ya pamoja katika wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Sipendi kukiogopesha chama changu, sipendi kuona kikibezwa na vijana kutokana na ahadi hiyo iliyoyeyuka kutokana na ongezeko la joto la ukuaji wa uchumi nchini, uchumi unaosemekana kukua kwa wenyewe huku sisi tukishindia mlo mmoja.

Kila mmoja wetu anatambua ni kwa jinsi gani maisha yanavyozidi kuwa magumu, huku suala la ajira kwa vijana likizidi kuwa kitendawili kilichokosa mteguaji siku nenda siku rudi.

Vijana sasa wamechoka kulaghaiwa na wanasiasa, wamechoka kutumiwa kutokana na njaa yao, hawataki tena kuwa bendera fuata upepo. Wanaojitokeza kuwapa matumaini sasa ndiyo mkombozi wao na kimbilio lao. Bomu la ajira sasa limelipuka, limelipukia kwa vyama vya upinzani.

CCM wana deni la kutegua bomu hilo lisilipuke wakati huu wa uchaguzi; bomu lililotegwa na chama miaka mitano iliyopita. Vijana wanataka kukiadhibu chama kutokana na kutotimiza ahadi.

Lowassa ni mgombea nafasi ya urais kupitia Ukawa, hivi sasa anaaminiwa na vijana. Hii yote ni kutokana na yeye kuonekana kuwa ni mkombozi wao anayetambua umuhimu wao na upatikanaji wa ajira.

Ukawa wamejiwekeza kwa vijana kwamba ndiyo mtaji kwao katika kipindi hiki cha uchaguzi, karata wanayoitumia vyema kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi. Bomu la ajira kwa vijana sasa limelipuka, limelipukia Ukawa na athari zake zinaonekana zikiiadhibu CCM.

Vyama vya siasa viwe makini na ahadi zake katika kipindi hiki ili kuepuka uundwaji wa idadi kubwa ya mabomu yanayoweza kuligharimu Taifa letu katika miaka ijayo.

By Jamhuri