Siku chache baada ya Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Theresa May, kutangaza Baraza jipya la Mawaziri, amewaacha watu wengi na mshangao kwa kumteua Boris Johson kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Ikumbukwe kuwa Johnson ndiye aliyekuwa kiongozi wa kampeni kuelekea mchakato wa kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya (EU) mara baada ya nchi hiyo kujiondoa ndani ya Jumuiya hiyo, makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi yalianza kumtupia lawama Boris na wenzake.

Johnson aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la London, baada ya uteuzi huo anasema nchi yake sasa ina nafasi kubwa ya kujenga upya uhusiano wake na nchi za Ulaya na ulimwengu mzima.

Wakati akitoa matamshi hayo, Waafrika bado wanamkumbuka kiongozi huyo kama mtu mwenye dharau ndani ya bara hili. Kwa mfano, mwaka 2002 wakati aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Tony Blair, alipozuru Bara la Afrika alisema:

 “Lazima Blair anahisi afueni kuu kwamba hatimaye amepata fursa ya kutoka Uingereza. Inasemekana malkia siku hizi anapendelea sana masuala ya Jumuiya ya Madola, mojawapo ya sababu zinazompa fursa za mara kwa mara kuona tu umati wa watu wazima kwa watoto wanaomshangilia wakimpeperushia vibendera.”

Kisha Boris akaongeza kusema, “Baadaye ataelekea nchini Congo. Sina shaka hizo AK47 itabidi zinyamaze, mapanga yanayotumiwa na Waafrika kuuana yatasitishwa kwa muda na wapiganaji wao wa kikabila watatoa tabasamu zinazofanana na tikitimaji wakati wakimuona Chifu Mkuu wa Kizungu, Blair, akitua na kuteremka kutoka katika ndege yake kubwa iliyonunuliwa na walipa kodi wa Uingereza.”

Pamoja na jitihada za Johnson kuomba radhi kwa matamshi yake, mwaka 2008 alipopata cheo cha Meya wa Mji  wa London, kauli hiyo haijasahaulika.

 Na si hayo tu, Machi, mwaka huu wakati maafisa wa Marekani wanaohusika na masuala ya ofisi ya Rais Barack Obama walipoamua kuiondoa picha ya Winston Churchill kutoka ofisi yake ya Oval, Boris alisema, “Hakuna uhakika iwapo Obama mwenyewe alihusika katika uamuzi huo wa kuiondoa picha hiyo.

“Baadhi ya watu wanasema ni kwa sababu yeye ni nusu Mkenya, alichukizwa na kumbukumbu ya picha ya Churchill ambaye aliunga mkono kwa dhati utawala wa Uingereza ulioikalia Kenya kwa mabavu enzi za ukoloni.”

Kuhusu uhusiano wa Serikali ya Syria na Urusi  baada ya majeshi yao kukomboa mji wa hifadhi wa kumbukumbu za kale, Palmyra, Boris alinukuliwa akisema; “Mtu yeyote mwenye akili timamu anapaswa kufurahi kwamba Palmyra imekombolewa na majeshi ya Assad; lakini wakati huohuo asibadili msimamo kwamba Assad ni dikteta na zimwi.”

Kisha akamshutumu Putin akisema operesheni zake za kijeshi zimekuwa zikilenga hospitali na shule za Syria, lakini wakati huohuo akamsifu Putin na utawala wake huko Urusi.

Hapo May alihoji sera ya EU huko Ukraine ambako Urusi inashutumiwa kuwaunga mkono waasi wa Mashariki wa Ukrain, lakini Boris akasisitiza kuwa ni mfano wa uamuzi wa EU uliofeli kutatua mzozo huo unaoendelea hadi leo.

Msemaji wa Serikali ya Urusi, Dmitry Peskov, amesema anatumaini uteuzi wa Boris kama Waziri wa Mambo ya Nje, unatoa fursa ya mwanzo mpya baina ya mataifa hayo, akiongeza kusema kuwa anatumaini nafasi hiyo itamfanya Boris kuwa na msimamo mpya wenye mwelekeo wa kidiplomasia.

Mwaka 2007 hivi ndivyo Boris alivyomwelezea Hillary Clinton kwamba; “Ana nywele zilizopakwa rangi, midomo yake ilivyo na anavyokodoa macho yake ya bluu, utafikiri ni nesi mwenye roho mbaya ndani ya hospitali ya watu wenye matatizo ya kiakili.”

Huyo ndiye Waziri mpya wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Uingereza, mtu mwenye dharau kwa watu. Je, nini hatima ya nchi hiyo juu ya diplomasia ya uchumi kwa mataifa ya nje?

Wakati nchi hiyo ikichukua uamuzi wa kujiondoa ndani ya Umoja huo, tayari baadhi ya viongozi kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya wametoa onyo kwa nchi hiyo.

Kwa mfano, katika siku za hivi karibuni Waziri Mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy, ameionya Uingereza kwamba kujiondoa kwake katika Umoja wa Ulaya kunaweza kusababisha wananchi wake kupoteza haki ya kuishi na kufanya kazi kwa uhuru ndani ya Umoja wa Ulaya.

“Inaonekana kwangu kwamba kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya itakuwa mbaya kwa Uingereza, kwa Uhispania na kwa nchi zote za Ulaya,” anasema Rajoy katika video iliyorushwa hewani na Shirika la Habari la EFE.

“Ulaya ilijengwa kwa msingi ya watu kuwa na uhuru wa kutembea popote wanapotaka barani humo, kuwa na mitaji popote pale na uhuru wa kuingiza bidhaa popote pale.

“Kama Uingereza imejiondoa katika Umoja wa Ulaya, wale ambao wataathirika zaidi ni wananchi wa taifa hilo ambao hawatakuwa na uhuru wa kutembea, au kutuma mitaji na bidhaa.

“Watu 100,000 kutoka Uhispania wanaofanya kazi nchini Uingereza wataathirika zaidi, lakini kuna raia 400,000 kutoka Uingereza wanaofanya kazi nchini Uhispania ambao watajikuta katika hali ya kutisha,” anasema Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy Brey.

Watu 283,000 kutoka Uingereza wameorodheshwa rasmi kuwa wanaishi nchini Uhispania, lakini idadi halisi inakadiriwa kuwa kati ya 800,000 na 1,000,000.

Wataalamu wengi wa masuala ya kiuchumi wanamuona waziri huyu kama mtu mwenye msimamo mkali, anayeweza kuharibu uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hiyo na nchi nyingine hasa za Kiafrika.

Lakini pengine swali kubwa la kujiuliza ni moja tu; nini hatima ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Ulaya na Afrika wakati huu ambapo kuna wimbi kubwa la wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali wakijaribu kukimbilia Ulaya?

By Jamhuri