*Asaini huku akijiandaa kung’atuka kazini

*Kampuni ya ulinzi yabainika utata mtupu

*Walinzi wake watuhumiwa wizi wa mali

MKATABA tata wa Sh milioni 742 kati ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Kampuni ya Ulinzi ya Supreme International Limited, umeanza kuwatokea puani viongozi wa TTCL, JAMHURI imethibitishiwa.

Mkataba huo ulisainiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TTCL, Said Amir, Mei 14, mwaka jana; wakati muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ukiwa ni Agosti 30, mwaka jana. Licha ya muda wake wa utumishi kumalizika, bado anaendelea kushikilia wadhifa huo. Muda wa kwisha kwa mkataba huo ni Aprili 30, 2015.

JAMHURI imefanikiwa kupata baadhi ya nyaraka zinazoonyesha kwamba baadhi ya viongozi ndani ya TTCL walipinga kampuni hiyo kuingia mkataba wa ulinzi na Supreme, lakini uongozi wa juu ulishinikiza na kufanikisha mpango huo.

 

Hoja ya kupinga mkataba baina ya kampuni hizo mbili ilijikita kwenye utata wa Supreme International Limited, hasa kwenye suala la mahali zilipo ofisi na kama kweli kulifanyika ukaguzi kujiridhisha kama ina uwezo wa kufanya kazi ya kulinda TTCL.

 

Utata mwingine wa mkataba huo upo kwenye idadi ndogo ya walinzi wanaoshiriki ulinzi kwenye vituo wanavyopangiwa, tofauti na idadi inayoonyeshwa kwenye mkataba.

 

Taarifa zinasema pia kuwa kampuni ya Supreme haina vitendea kazi kama bunduki, jambo linalosababisha kuwapo hatari ya usalama wa mali za TTCL.

 

Pia kuna tuhuma kuwa baadhi ya walinzi wa kampuni hiyo si waaminifu kwa mujibu wa matukio ya karibuni yaliyoripotiwa katika vituo vya Masaki, Ubungo Maziwa, Magomeni, Oysterbay na Sinza.

 

Historia ya mkataba/utata idadi ya walinzi

Ulisainiwa Mei 14, mwaka jana kati ya Said Amir, akiwakilisha TTCL; na Mkurugenzi Mtendaji wa Supreme International Limited, Deogratias Muganda; na kushuhudiwa na mwanasheria aliyejitambulisha kwa jina la Anita Samwel Mushi. Muganda ameitambulisha Supreme International Limited kuwa inapatikana kupitia Sanduku la Barua 61614 Dar es Saalam. Anuani hiyo hiyo pia ndiyo inayotumiwa na kampuni yake nyingine ya Utdager Consultant and Business Investment ya Dar es Salaam.

 

Utata unajitokeza kwenye idadi ya walinzi ambao kampuni hiyo inapaswa kuwaweka kwenye vituo kama walivyofikia makubaliano na TTCL.

 

Kwa mujibu wa mkataba huo, kila ‘kichwa’ kinapaswa kulipwa na TTCL Sh 180,000 kwa mwezi.

Imebainika kuwa katika vituo kadhaa, idadi ya walinzi si ile iliyoelezwa kwenye mkataba, hiyo ikiwa na maana kwamba kampuni inalipwa fedha nyingi kwa “walinzi hewa”.

 

Baadhi ya vituo ambavyo vinaonyeshwa kwenye mkataba kwamba wakati wa mchana vinapaswa kuwa na walinzi wawili, imebainika kuwa mlinzi mmoja tu hufanya kazi hiyo. Kwa usiku, baadhi ya vituo vinavyoonyeshwa kwenye mkataba kuwa na walinzi wanne, mara nyingi kampuni hiyo imekuwa ikipeleka mlinzi mmoja au wawili.

 

Kwa upande wa silaha, imebainika kuwa mkataba unaitaka kampuni hiyo iweke walinzi 113 kwa mgawo kulingana na kanda tatu za Dar es Salaam Kati, Dar es Salaam Kaskazini na Dar es Salaam Kusini.

 

Kwa mchanganuo huo, malipo kwa Dar es Salaam Kati yanapaswa kuwa Sh 99,000,000 (walinzi 15); Dar es Salaam Kusini Sh 212,760,000 (walinzi 32); na Dar es Salaam Kaskazini Sh 431,280,000 (walinzi 66).

 

Kwa idadi hiyo, malipo yanapaswa yafanywe kwa askari 113, lakini JAMHURI imejiridhisha kuwa kampuni hiyo haina idadi hiyo ya askari wanaopelekwa kwenye malindo. Hii ina maana kwamba fedha nyingi zimekuwa zikiishia mikononi mwa kampuni hiyo ya ulinzi pamoja na maofisa kadhaa wa TTCL.

 

Said amekuwa hataki kutoa ushirikiano kwa JAMHURI. Mara kadhaa anapopigiwa simu, amekuwa akikata baada ya mwandishi kujitambulisha. Hata anapopelekewa ujumbe mfupi wa maandishi, amekuwa hajibu. Hali ni hiyo hiyo kwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Mrisho Shabani ambaye hataki kupokea simu.

 

Wamiliki wa Supreme International Limited

Kwenye usajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inaonyesha kuwa makazi yake ni mkoani Mwanza. Ilisajiliwa Novemba 24, 1995 kwa namba 38363; na kufanyiwa marekebisho ya usajili mwaka 2009.

 

Katika anuani yao, Supreme inaonyesha kuwa mdhamini wake mkuu ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

 

Ilianza kwa mtaji wa Sh 30,000,000 kwa kila mwanahisa kuwa na hisa 3,000 zikiwa na thamani ya Sh 10,000 kila moja.

 

Wanahisa hao ni Charles Kazana Munubi anayemiliki hisa 1,000; Utdager Consultant and Business Investment Limited inayomilikiwa na Deogratias Gabriel Muganda (1,000) na Vedastus Kalwizara Lufano (1,000).

 

Wakurugenzi  wa kampuni hiyo ni  Charles Kazana Munubi anayepatikana kupitia Sanduku la Barua 7657, Mecco Kitalu FF kiwanja Na. 522 Nyakato,  Mwanza; Utadger Consultant and Busness Limited Sanduku la Barua 61614; Kiwanja Na. 520 /A, Sinza, Dar es Salaam.

 

Mwingine ni Vedastus Kalwizira Lufano anayepatikana kupitia Sanduku la Barua 7657, Mecco Kitalu FF, Kiwanja Na. 520 Nyakato, Mwanza.

 

Katika Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Machi 10, 2005 uliamua kumuongeza mwanahisa mwingine, Deusdet David Muhanuzi aliyenunua hisa 3,000 kwa thamani ya Sh 10,000 kwa kila hisa; hivyo kuifanya kampuni kuwa na wakurugenzi wanne.

 

Kwa mujibu wa BRELA, kampuni hiyo haijapeleka taarifa za marejesho yake ya mwaka kwa miaka 10 sasa kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka jana. Taarifa nyingine zinasema kwamba Supreme imewasilisha taarifa hizo, lakini zina upungufu.

 

Hata hivyo, uchunguzi wa Jamhuri umebaini kuwa Supreme imepata mikopo kutoka benki mbalimbali za hapa nchini. Imekopa kutoka NMB, CRDB, Kenya Commercial Bank; na mkopo wa karibuni kabisa waliupata kutoka Barclays ambako walipata Sh milioni 120 mnamo Oktoba 29, mwaka jana, ingawa hawajawasilisha taarifa hizi BRELA.

 

1589 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!