Na Charles Ndagulla, Arusha

Halmashauri ya Jiji la Arusha imezidi kuandamwa na tuhuma za ugawaji holela wa ardhi inayomilikiwa na watu wengine, hivyo kuzidisha kero na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Hali hiyo imebainika ikiwa ni takribani wiki moja baada ya gazeti hili kuandika mkanganyiko wa umiliki wa kiwanja kilichopo kitalu ‘J’ namba 116, eneo la Njiro.

Mgogoro huo unawahusisha watu wawili wenye hatimiliki za kiwanja hicho – Bunto Juma Bunto wa sanduku la barua 57 na Karoline Reginald Mariki wa sanduku la barua 6136 – wote wakazi wa jijini humo.

Safari hii, jiji hilo lililo kivutio cha utalii nchini, limelalamikiwa na familia tano za jamii ya wafugaji wa Kimaasai katika kata ya Osunyai, wanaodai eneo lao ‘kuporwa’ na kukabidhiwa kwa mkandarasi wa Kijerumani aliyekuwa akijenga mradi wa maji jijini humo.

Mkandarasi huyo, kampuni ya M/S Josef Riel Bau-AG Limited(JR), anadaiwa kumilikishwa ardhi  hiyo mwaka 1989 kwa Letter of Offer ya mwaka 1989 na baadaye kuandaliwa hatimiliki ya miaka 66.

Mwaka 1985, kampuni hiyo ilishinda kandarasi ya kusambaza maji safi na salama katika mji wa Arusha, na ilipofika 1990 ilimaliza kandarasi hiyo na kuondoka nchini.

Baada ya kushinda kandarasi hiyo, wananchi hao waliombwa kutoa eneo lao ili kumwezesha mkandarasi huyo kuweka vifaa vyake kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa wa maji.

Lakini katika mazingira yanayotiliwa shaka, kampuni hiyo ikamilikishwa eneo hilo la zaidi ya ekari 12 kwa ajili ya makazi, kiwanda na matumizi mengine.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa, baada ya kampuni hiyo kumilikishwa ardhi hiyo na kuondoka nchini mwaka 1992, ilihamisha umiliki wake kwenda kwa Mtanzania mwenye asili ya Asia, Kulwant Singh, na uhamisho huo uliidhinishwa na kusajiliwa kwa msajili wa hati.

Kwa sasa eneo hilo linamilikiwa na kampuni ya Sunvic Express baada ya Singh kufariki dunia. Amerjit Singh na Gurdev Kaur waliteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi ya Singh ikiwa ni kabla ya kujimilikisha eneo hilo.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI linazo, Gurdev Kaur alifariki dunia na jina lake kufutwa kwenye umiliki, chini ya kifungu namba 69 cha Sheria ya Usajili (cap 334) ya mwaka 2008.

Kufariki kwa Kaur kulimwezesha Amerjit Singh kubaki katika umiliki huo na mwaka huo (2008) alihamisha umiliki kwenda kwa kampuni ya  Sunvic Express.

Hata hivyo, familia hizo zimepinga hatua ya jiji la Arusha kummilikisha mkandarasi huyo ardhi yao, kutokana na kile wanachodai umilikishwaji huo ‘umezingirwa na harufu ya rushwa’.

Moses Mtema Mollel, Mwenyekiti wa Boma Tano amesema utoaji wa ardhi ulilenga kuweka karakana na kwamba baada ya kandarasi hiyo kumalizika, lilitakiwa kurudishwa kwa wananchi.

Pamoja na kampuni hiyo kumaliza kandarasi yake mwaka 1990, wananchi hao hawakurejeshewa ardhi yao na kwamba baada ya kufuatilia kwa mamlaka za Serikali, ikabainika kumilikishwa.

“Hapa kuna maswali mengi yanayohitaji majibu sahihi, kwanza huyo alikuwa mkandarasi na hakuwa mwekezaji ni lini aliomba kumilikishwa ardhi hiyo?” anahoji Mollel.

Amedai kuwa licha ya eneo lao kuchukuliwa na jiji la Arusha, hawakulipwa fidia, hali inayoibua wasiwasi wa ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kata hadi jiji la Arusha.

Familia hizo zimeandika barua kwa ofisi ya Waziri Mkuu, kuomba iingilie kati suala hilo ili haki yao ikiwamo fidia ipatikane.

Barua hiyo ya Januari 5 mwaka huu iliyosainiwa na Katibu anayewakilisha maboma matano ya jamii hiyo ya wafugaji, Lomnyaki Mevaashi Timayo.

JIJI WAJIKANGANYA

Halmashauri ya Jiji la Arusha imesema wananchi hao hawastahili kulipwa fidia kwa vile hakuna sheria inayohusiana na fidia iliyotumika wakati wa kumkabidhi mkandarasi eneo hilo.

Barua hiyo ya Januari 19, mwaka huu iliyosainiwa na Dickley Nyato, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji hilo, imetumwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Imeeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1966 iliyokuwapo, ardhi ilikuwa mali ya umma na ilikosa thamani kutokana na kutokuwa na mali juu yake.

Kwa mujibu wa barua hiyo,  ya Halmashauri ya Jiji la Arusha  ya Januari 19 mwaka huu iliyosainiwa na Dickley Nyato kwa niaba ya mkurugenzi wake kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Arusha, ilikuwa ikifafanua umiliki wa kiwanja namba 135 Kitalu ‘DD’ kilichopo eneo la Sombetini.

Barua hiyo inaeleza kuwa mmiliki wa ardhi kwa kipindi hicho, alikuwa na haki ya maendelezo yaliyopo chini ya ardhi na si vinginevyo.

“Hivyo kwa kipindi ambacho wananchi wa eneo hili wanadai kuwa eneo lao lilichukuliwa, hapakuwa na sheria yoyote ya kulipa fidia,” imeeleza barua hiyo.

Hivyo, barua hiyo ikaeleza kuwa kwa kuzingatia sheria iliyokuwapo wananchi hao hawana madai ya msingi isipokuwa kwa kuzingatia mahusiano ya Serikali, inaweza kuwafikiria wakapewa maeneo mbadala.

Hata hivyo, Meneja wa  kampuni ya Sunvic Express wanaomiliki eneo hilo kwa sasa, Zainabu Athuman,  amesema suala hilo lilihitimishwa na mamlaka za Serikali mkoani Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Dakaro, hakutaka kuzungumza kwa kina suala hilo wakati akihojiwa na JAMHURI wiki iliyopita kwa madai ya kuwa kwenye vikao vya kikazi.

Hata hivyo, baada ya jitihada za kumfuata ofisini kwake kushindikana, JAMHURI ilimtumia ujumbe mfupi wa maneno na mawasiliano yalikuwa hivi:-

JAMHURI: DC (Mkuu wa Wilaya) ninaitwa Charles Ngadulla, Mwandishi wa Habari wa Gazeti la JAMHURI, nimekupigia kupata kauli yako kuhusu malalamiko ya familia tano katika kata ya Osunyai-JR wanaolalamikia ardhi yao kuchukuliwa bila kulipwa fidia.

MKUU WA WILAYA: Salama? Walichukuliwa lini na nani?

JAMHURI: Wanadai iligawiwa kwa mkandarasi kampuni ya M/S Josef Riel Bau-Ag aliyekuwa akijenga mradi wa maji Arusha na baadaye naye akaiuza kwa kampuni ya Sunvic Express.

MKUU WA WILAYA: Nina kikao nitarudi week end (mwisho wa wiki) hii kituoni uje ofisini.

JAMHURI: Sawa Mkuu.

Baada ya mawasiliano hayo, jitihada za kumpata tena zilishindikana licha ya kumpigia simu bila kupokewa.

Kwa upande mwingine, imebainika kuwa Mkuu wa Wilaya huyo aliunda kamati iliyotoa mapendekezo kadhaa ikiwamo kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuwalipa wakazi hao.

Katika taarifa yake ya Oktoba 25, mwaka jana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya huyo, kamati hiyo iliyoongozwa na Ofisa Tarafa ya Elerai, Titho Cholobi, ilieleza kwamba eneo hilo kwa asili lilikuwa mali ya familia tano.

Taarifa hiyo ambayo nakala yake tunayo, inaeleza kuwa halmashauri ya jiji inatakiwa kuangalia namna ya kuwalipa fidia wananchi hao mapema iwezekanavyo, kwa vile ilihusika katika kulitwaa eneo lao.

mwisho

1731 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!